The House of Favourite Newspapers

UKITAKA PENZI LAKO LIDUMU, FANAYA HAYA TANGU MWANZO!

HAKUNA muda ambao hisia za mapenzi na msisimko huwa mkubwa kama kipindi ambacho ndiyo kwanza mnaanzana. Ukiwauliza watu wengi leo ambao wanateswa na mapenzi, wanatamani siku zirudi nyuma ili warudie kufaidi mapenzi kama ilivyokuwa siku za mwanzo wakati wanaanzisha uhusiano. Hata hivyo, ni wachache wanaojua nini cha kufanya unapoanzisha penzi jipya ili hisia na msisimko unaoupata, vidumu kwa muda mrefu na uendelee kuyafurahia maisha ya kimapenzi. Mapenzi ni kama nyumba, ukijenga msingi imara, nyumba yako itakuwa imara na ukijenga msingi legelege, usitegemee nyumba yako kuja kudumu baadaye.

Kama upo kwenye mapenzi mapya na unatamani raha na msisimko unaoupata leo udumu, yapo mambo kadhaa ya muhimu ya kuzingatia. Kujengeana heshima; Wanandoa, wachumba au wapenzi wengi, hulalamika kwamba wenzi wao hawawaheshimu, hawana shukrani na ndiyo maana hawafurahii maisha yao ya kimapenzi.

Unapokuwa kwenye hatua za mwanzo za mapenzi, jenga heshima kwa mwenzi wako bila kujali umri, cheo au hali ya kiuchumi. Hata kama mwenzi wako ana udhaifu fulani, kwa sababu umempenda na kuamua kuwa naye, jifunze kumheshimu.

Pia jifunze kuwa na shukrani hata kwa yale mambo madogo anayokufanyia. Wengi huwa hawaoni umuhimu wa kuwashukuru wenzi wao na matokeo yake wanajenga ufa ambao baadaye unasababisha matatizo makubwa.

Hata kama mwenzi wako amekununulia pipi, akikupa shukuru kwa sababu amekufikiria ndiyo maana akakununulia. Hata kama mwenzi wako amekupa zawadi au kitu ambacho hujakipenda, badala ya kukimbilia kukosoa, onesha kwanza shukrani, kesho na keshokutwa atapata nguvu ya kukutafutia vitu vizuri zaidi.

Chunguzaneni kwanza; Kuchunguzana ninakomaanisha hapa, siyo kutaka kujua kabla yako alikuwa na nani au amewahi kutoka na nani, wahenga wanasema bata ukimchunguza sana huwezi kumla. Kuchunguzana ninakokuzungumzia hapa, ni vizuri kufuatilia kwa kina ili ujue mwenzi wako anapenda nini, hapendi nini, kitu gani kinamfurahisha na kitu gani kinamtia hasira.

Mchunguze akiwa na hasira anakuwaje na akiwa na furaha anakuwaje, anapenda sana kufanya mambo gani (hobi) au anapenda sana zawadi za namna gani. Ukishamjua, ni rahisi sana kuishi naye hata pale anapokasirika au anapokerwa na jambo fulani kwani tayari utakuwa unajua kwamba akiwa hivi, ujue amekasirika au akifanya hivi ujue jambo fulani halipendi.

Pia itakusaidia kwenda naye sawa kwa sababu akikasirika, utajua ufanye nini afurahi kwa sababu tayari unavijua vitu vinavyomfurahisha. Ni makosa makubwa kufanya jambo wakati unajua kabisa mwenzi wako hapendi.

Unapokosea omba msamaha; Wanaume wengi wanaamini kwamba hata wakikosea, hawatakiwi kuomba msamaha kwa sababu kuomba msamaha ni ishara ya udhaifu, matokeo yake wanaendekeza mfumo dume bila kujua kwamba mapenzi ni demokrasia!

Bila kujali kwamba wewe ni mwanaume au mwanamke, mkubwa au mdogo, una fedha au huna, inapotokea umeziumiza hisia za mwenzi wako, iwe kwa jambo dogo au kubwa, ni lazima uombe msamaha na kuahidi kutorudia makosa.

Ukishajenga utaratibu huu, hata kama mwenzi wako hakuwa na kawaida ya kuomba msamaha, taratibu utambadilisha. Utashangaa na yeye anaomba msamaha na huo unakuwa mfumo wa maisha yenu. Kuwa makini kwamba ukiomba msamaha leo, siyo kesho unarudia tena kosa lilelile, ataona unamfanyia makusudi.

Ukizingatia mambo haya machache, ukazidisha mapenzi na kumjali mwenzi wako, ukawa mwaminifu na mkweli, hisia tamu za mapenzi unazozihisi leo, zitadumu na utayafurahia maisha yako ya kimapenzi. Kwa leo niishie hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Comments are closed.