Unagombana sana na mpenzi WAKO?

UHUSIANO wa kimapenzi ni kitu muhimu katika maisha ya binadamu! Mtu yeyote ambaye amekamilika, anahitaji kuwa katika uhusiano wa kimapenzi. Hakuna anayeweza kuvumilia maisha ya upweke, sote tunahitaji kupenda na kila mtu anahitaji kupendwa.  Hata hivyo, siyo mara zote mapenzi yanakwenda kama wengi tunavyotaka yawe. Unapoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, unakuwa na matarajio makubwa ya kuishi maisha ya raha mustarehe na umpendaye, kupeana mapenzi motomoto na kujenga familia bora.

Hata hivyo, baada ya muda mfupi, mambo huanza kwenda mrama, mapenzi hupungua, ugomvi huanza kuibuka na penzi huingiwa na shubiri na kusababisha hisia za huzuni kali ndani ya moyo.Wapo watu wengi wanaoteseka katika uhusiano wa kimapenzi, furaha kwao imetoweka kabisa, wengine wanafikia hatua ya kuyachukia mapenzi na kujiapiza kwamba hawatapenda tena. Kama na wewe ni miongoni mwa watu ambao wapo katika aina hii ya uhusiano wa kimapenzi, unatakiwa kuelewa jambo moja la msingi sana ambalo wengi huwa hawalielewi.

Uhusiano wa kimapenzi, mpaka kufikia ile hatua ya kushibana na kuwa mwili mmoja, huwa unapitia katika hatua kuu tano. Ukiona watu wanazeeka pamoja wakiwa bado wanapendana kwa dhati, jua wamefanikiwa kuzivuka hatua hizo zote tano na ndiyo maana  wameshibana.

Hatua tano zinazozungumziwa hapa, ni upofu wa mahaba, uhalisia na ugomvi, kujitathmini, kupatana na mwisho ni mahaba ya dhati. Kwa bahati mbaya, katika hatua hizo tano, ni hatua mbili au tatu tu ndiyo huwa zinakuwa tamu na za kufurahisha! Hatua ya kwanza na hatua ya nne na hatua ya mwisho.

Ndoa nyingi zinazovunjika, huwa zinaishia kwenye hatua ya pili na utafiti unaonesha kwamba katika kila ‘couple’ 100 zinaoanza uhusiano wa kimapenzi, ni ‘couple’ tano tu ndiyo huwa zinavuka mpaka hatua ya tano. Hii ina maana gani? Pale unapoanza uhusiano mpya wa mapenzi, akili yako huwa ni kama imepigwa na upofu, husikii wala huambiwi kwa huyo unayempenda. Hata kama mwenzi wako ana kasoro kibao, kwa sababu umempenda na moyo wako umepigwa na upofu wa mahaba, utaziweka kasoro pembeni na kuelekeza nguvu kutazama mazuri yake. Hii ni hatua ya kwanza.

Hata hivyo, baada ya muda fulani kupita, akili yako itaanza kurudi kwenye uhalisia wake, hapa unapiga hatua kutoka kwenye hatua ya kwanza kwenda kwenye hatua ya pili ya uhalisia na ugomvi! Hapa sasa ndipo moto unapoanza kuwaka.

Zile kasoro ambazo awali ulikuwa ukizipuuzia kwa mwenzi wako, sasa zitaanza kuonekana waziwazi na kuwa kero kubwa kwako. Utataka unayempenda awe kama wewe unavyotaka, utatamani kumrekebisha ili muendelee kufurahia mapenzi yenu, lakini hilo ni jambo lisilowezekana, na hapo ndipo ugomvi usioisha unapoanza kuibuka.

Mtapishana sana kauli, mtatoleana sana maneno machafu, mtapigana sana na msipokuwa makini huo ndiyo utakuwa mwisho wenu. Jambo la muhimu ambalo kila mmoja anapaswa kulijua, unapoona uhusiano uliopo umefikia kwenye hatua hii, lazima ujue kwamba mpo kwenye mapito na busara na uelewa wa kutosha kwenye mapenzi ndiyo kitu pekee kinachoweza kuwavusha. Nini cha kufanya unapokuwa kwenye aina hii ya mapenzi? Ni mbinu gani zinazoweza kulituliza penzi lililopigwa na dhoruba? Tukutane wiki ijayo ili tupeane mbinu mbalimbali.


Loading...

Toa comment