The House of Favourite Newspapers

Unaikumbuka ahadi yako wakati unaanzisha uhusiano?-3

LEO tunamalizia mada yetu iliyoanza wiki mbili zilizopita. Nitahitimisha kwa kuwaonyesha namna ya kukabiliana na matatizo ambayo yameshatokea kutokana na kutoa ahadi feki.  Niazime utulivu wako kwa muda, fungua ubongo wako, halafu chuja maneno yangu, nina imani yapo ambayo ukiyachukua yatatengeneza kitu fulani maishani mwako. Karibu…

UPO KWENYE MIGOGORO

Je, upo kwenye uhusiano? Kama jibu ni ndiyo unatakiwa kusafiri kidogo mbele zaidi ya hapo. Uhusiano wako una migogoro? Huelewani na mpenzi wako na hujui sababu? Rafiki zangu kujua tatizo ni mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye utatuzi.

Kitu kikubwa zaidi kutafuta chanzo cha migogoro, hata kama utakaa na mpenzi wako leo na mkayaongea na  kuyamaliza, haitasaidia kitu, ikiwa bado mwenzio anaendelea kusubiri ahadi ambazo ulizitoa ambazo kimsingi huwezi kuzitekeleza. Sasa twende katika hatua inayofuata.

ANZA KUCHUNGUZA SABABU

Fuatilia kwa makini ugomvi wako na mwenzako, zaidi chunguza kauli zake. Huwa anazungumzia nini zaidi? Anatamka nini? Lazima kuna vitu ambavyo atakuwa anapenda kuvirudia mara kwa mara, hivyo ndivyo vya kuvifanyia kazi. Maneno ambayo huyatamka mara kwa mara katikati ya mrushiano wa maneno, ndiyo hasa yanaweza kukuongoza katika kuelewa mwenzako anagombana na wewe kwa sababu gani.

“Mwanaume maneno mengi, mara utaninunulia gari, kila siku wimbo wako umebaki hivyo hivyo. Kila siku unasema utanitafutia kazi, mara nitakupa mtaji lakini hutimizi…sasa haya ni mapenzi gani,” kauli kama hii ni ya maana sana. Kumbuka rafiki yangu, wakati akitamka neno lolote lile ambalo lina mantiki katika kutafuta ninachokizungumzia hapa, huwa hakina uhusiano wowote na msingi wa ugomvi wenu. Ni maneno ya kuchomeka tu bila mpangilio.

AHADI YAKO ILIKUWA NINI?

Hapa ndipo unapotakiwa kuvuta kumbukumbu zako hadi katika kiwango cha mwisho. Kumbuka ahadi uliyotoa kwa mpenzi wako. Kitendo cha kukumbuka ahadi kitakufanya uanze kuchuja moja baada ya nyingine na kuunganisha na matukio yanayotokea hasa mnapokuwa katika ugomvi. Je, ulimuahidi nini? Ukishajua hapa, itakuwa rahisi kumaliza tatizo la msingi.

FUNGUKA…

Ikiwa utakuwa umekumbuka kila kitu juu ya ahadi zako, ni wakati wako wa kusema ukweli. Funguka! Kama unajua kabisa kuna mambo ambayo ulimuahidi lakini hujayatimiza na huenda huwezi kufanya hivyo, mwambie ukweli.

Siku zote ukweli ni silaha kubwa sana katika uhusiano. Kumwambia mwenzako ukweli na kukiri makosa kwamba ulifanya hayo kwa bahati mbaya au uliamini kwa kufanya hivyo ni njia rahisi ya kumpata, angalau utakuwa umemuondolea utandu mweusi machoni mwake. Ataujua ukweli na bila shaka atakusamehe na kuachana na ahadi zako hewa, kisha kuufuata ukweli wako.

JIFUNZE KUTOKANA NA MAKOSA

Kwa hakika, makosa ambayo utakuwa umeyafanya yatakuwa yamekuumiza, lakini pia yamekupa mwanga wa nini cha kufanya ili uendelee kuwa katika nafasi salama zaidi katika uhusiano wako. Achana na ahadi hewa, jifunze kuwa mkweli, uongo hauna maana. Kudanganya wewe bosi kazini, wakati ni mtu wa kawaida kama siyo wa mwisho hakuna maana yoyote. Inawezekana hata huyo mpenzi wako mwenyewe, anapenda zaidi kuwa na mtu wa kawaida kuliko anayejinadi kwa vyeo vyake.

Mapenzi yapo moyoni rafiki zangu, si kwenye fedha, mali au cheo chako kazini. Zungumzia mapenzi, ahidi kumpenda. Pendo ni hazina ambayo haiwezi kufutika moyoni, kumuahidi kumpenda, utakuwa unampa matumaini makubwa zaidi ya kuishi na wewe katika hali yoyote ile, tofauti na kudhani kwamba mali ndiyo kila kitu.

MWANAMKE ANATAKA KUPENDWA!

Naamini somo limeeleweka, siyo ahadi nyingi zisizotekelezeka. Tukutane wiki ijayo.

Joseph Shaluwa ni mshauri wa maisha, uhusiano na ujasiriamali anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, kikiwemo Maisha ya Ndoa kinachopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

Comments are closed.