visa

UNAIKUMBUKA AHADI YAKO WAKATI UNAANZISHA UHUSIANO?

NI Alhamisi nyingine tunakutana tena kwenye ukurasa huu wa kupeana elimu juu ya uhusiano na mapenzi. Leo nazungumzia juu ya ahadi ambazo wenzi hutoleana wanapokutana mara ya kwanza.  Kwa bahati mbaya sana, wengi wanapokutana mara ya kwanza, hutoa ahadi yoyote ilimradi iwe ya kumvutia mhusika ili amkubali kuwa naye. Rafiki yangu mpenzi, hebu tuzungumze na uwe mkweli katika hili; siku ya kwanza kukutana na mpenzi wako ulimuahidi nini? Je, ahadi zako zimetekelezeka? Uhusiano wako ukoje sasa hivi?

Ngoja nikuambie kitu ndugu yangu, inawezekana upo katika uhusiano na mwenzi wako, lakini kila siku mnagombana, unajaribu kuweka mambo sawa, lakini baada ya siku mbili, tatu ugomvi unarudi pale pale, umejiuliza tatizo ni nini?

Subiri nikumegee siri, utafiti usio rasmi niliofanya kwa muda wa mwaka mmoja sasa, unaonesha kwamba, ugomvi mwingi wanandoa husababishwa na ahadi! Yaani unakuta mtu alipokutana na mpenzi wake mara ya kwanza alimpa ahadi kedekede, kwamba atamfanyia hili na lile au hatafanya hivi na vile, lakini wanapokuwa kwenye uhusiano anajisahau na kufanya kinyume na makubaliano, hapo unaibuka mtiti!

Hili ni somo ambalo litakuweka sawa wewe ambaye upo kwenye uhusiano kwa muda mrefu na mwenzi wako, kukufanya ukumbuke makosa yako ili upate nafasi ya kutuliza hali ya hewa katika penzi lenu.

Hata hivyo, itawasaidia zaidi wale ambao bado hawajaingia kwenye uhusiano, kujua madhara ya kuahidi ahadi za uongo.

Kwanza, hebu tuone mambo ya kuzingatia kabla ya kutoa ahadi kwa mpenzi wako unapokutana naye kwa mara ya kwanza, halafu baadaye tutaona ahadi ‘feki’ zinazotolewa na wenzi wanapokutana kwa mara ya kwanza, halafu zikaleta matatizo baadaye.

KWA NINI UNAAHIDI?

Eti marafiki, kwani lazima unapokutana na mwenzi wako kwa mara ya kwanza utoe ahadi? Unaahidi nini? Kwani unataka ubunge mpaka uanze kutoa ahadi? Kimsingi kuahidi, ni sawa na kuonesha jinsi ambavyo una mashaka ya kukataliwa, ndiyo maana unakimbilia kutoa ahadi.

“Kwa kweli nitabadilisha maisha yako… kwanza sisi kwetu mambo safi… nafanya kazi kwenye ofisi ya mdingi na mimi ndiye director. Nadhani itabidi nifanye mchakato uanze kazi pale! Hivi elimu yako kiwango gani vile?”

Mwingine anaweza kusema: “Nitahakikisha nakufungulia biashara yako, naomba unikubalie mpenzi, utafurahi nakuhakikishia.” Rafiki yangu, yote hayo ya nini? Baadhi ya ‘mbumbumbu’ au wapenda ahadi, watakuona wa maana na inawezekana kabisa ukapewa nafasi ya kuwa naye, lakini uliyosema ni ya kweli? Ataingia kwenye uhusiano akiwa na matarajio makubwa sana kichwani mwake, kumbe si kweli bali umemwingiza mwenzio chaka!

Mada yetu itaendelea wiki ijayo, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni mshauri wa maisha, uhusiano na ujasiriamali anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, kikiwemo Maisha ya Ndoa kinachopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni
Toa comment