The House of Favourite Newspapers

UTAJIRI WA HARMONIZE TISHIO!

DAR ES SALAAM: WAZUNGU wana msemo usemao; ‘hard work pays’! Msemo huu unaweza kuwa na maana kubwa katika maisha ya bwa’mdogo kutoka Kruu la Wasafi Classic Baby (WCB), Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ ambaye jitihada zake zinaelezwa kumpa mafanikio makubwa na kuwa tishio, Ijumaa lina stori kamili. 

 

Harmonize au Harmo ambaye ana takriban miaka mitano kwenye tasnia ya muziki wa Bongo Fleva tangu ajiunge na WCB na kuungana na vijana wengine wa kundi hilo, anatajwa kuwa na ukwasi wa kutosha huku ikielezwa kuwa mtu anayeongeza chachu ya utajiri wake ni mchumba wake, Mzungu aitwaye Sarah Michelotti, raia wa nchini Italia.

TUJIUNGE NA MTANDAO WA KENYA

Kwa mujibu wa mtandao maarufu nchini Kenya wa HYPERLINK “http://www. technish.co.ke” www.technish. co.ke, msanii huyo ni miongoni mwa wasanii ambao wanalipwa fedha nyingi kwa shoo katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na nyumbani Tanzania.

 

Mtandao huo umeweka bayana kuwa, msanii huyo kwa sasa analipwa si chini ya Dola za Kimarekani 10,000 (zaidi ya shilingi milioni 23 za Kibongo) na ukiangalia orodha ya shoo zake utagundua ni nyingi na anakuwa ameshashikiliwa wakati mwingine na shoo hata za mwezi au miezi kadhaa mbele.

 

Mtandao huo kutokana na taarifa zake ulizozikusanya ulimtaja Harmonize kuwa na utajiri usiopungua Dola za Kimarekani milioni moja (zaidi ya shilingi bilioni 2 na ushee za Kibongo).

ANAMFUKUZIA MONDI KIMYAKIMYA

Kwa taarifa za miaka kadhaa iliyopita, bosi wa msanii huyo katika Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’ amewahi kutajwa kuwa na ukwasi usiopungua shilingi bilioni nane za Kitanzania hivyo kijana anaonekana kasi yake siyo mbaya, anajaribu kujitutumua ili kumkuta.

VYANZO VYA BONGO

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya Bongo, Harmonize anaakisi utajiri huo ambao umetajwa kutokana na mali anazomiliki ikiwemo ghorofa analolijenga maeneo ya Madale jijini Dar, achilia mbali kodi anayolipia ‘apartment’ anapoishi kwa sasa huko Masaki, Dar.

 

“Yuko vizuri, kijana unajua tangu ametua WCB amejiongeza, amekuwa akifanya shoo zake huku pia akiunganisha nguvu na mchumba wake, Sarah. Wewe unavyoona mtu anashusha ghorofa ujue kabisa kwenye akaunti yake kuna shilingi bilioni kadhaa, siyo kitu cha ajabu. “Lile ghorofa analolijenga hadi likikamilika linaweza kufika hata bilioni moja sasa unaweza kuona ni jinsi gani bwa’mdogo yuko vizuri,” kilieleza chanzo kilicho karibu na familia ya WCB.

MAGARI YA KIFAHARI

Chanzo hicho kilieleza kuwa, mbali na kulipa kodi kubwa katika nyumba anayoishi sasa, pia Harmonize anamiliki magari ya kifahari ikiwemo Toyota Prado, Benz na Mark X ambayo ameyapata kutokana na kazi yake ya muziki.

 

“Mtu ukishakuwa na ghorofa mjini, ukawa na magari yako ya kifahari kama hivi, kuna nini tena? Harmo mambo yanamuendea vizuri, kwa kweli anapaswa kumshukuru Mungu,” kilisema chanzo.

 

SHOO ZINAMBEBA

Gazeti la Ijumaa limechungulia na kubaini kwamba kijana huyo ana uwezo wa kutengeneza fedha nyingi zaidi kutokana na shoo alizonazo mkononi kwa mwaka huu. Shoo ambazo Harmonize anatarajia kuzifanya zimeongozana kuanzia Aprili 16, mwaka huu hadi Novemba 30. Hapo kuna shoo za ndani na nje ya nchi kama vile Dubai, Ujerumani, Uingereza, Australia, Sudan Kusini na Marekani.

MWENYEWE ANASEMAJE?

Gazeti la Ijumaa lilipomtafuta Harmonize ili kuweza kumsikia anazungumziaje utajiri wake halikuweza kufanikiwa kutokana na kuwa nje ya nchi. Hata hivyo, mara kadhaa kwenye mahojiano yake mbalimbali na gazeti hili amekuwa akieleza namna anavyomshukuru Mungu kwa kile alichomjalia.

 

“Nikitazama nilipotoka kijijini kwetu Mtwara, namshukuru sana Mungu kwa kunijalia maisha niliyonayo. “Pili sitaacha kumshukuru sana mtu ambaye ni mfano kwangu, Diamond maana amechangia mimi kuwa hapa nilipo leo,” anasema Harmonize.Harmonize amekuwa akimuomba Mungu azidi kumbariki, asiwe na kiburi na awe mnyenyekevu zaidi na aweze kuifikisha sanaa ya Bongo Fleva mbali.

Stori: MWANDISHI WETU, IJUMAA

Comments are closed.