WAFUNGWA saba kati ya 219 waliotoroka kutoka katika Gereza la Singila, Moroto, Kaskazini-Mashariki mwa Uganda wamekamatwa. Wafungwa hao walimpiga risasi na kumuua askazi ambaye alijaribu kuwazuia kutoroka, kabla ya kukimbilia kwenye mlima wa Moroto, Jumatano mchana.
Msemaji wa huduma za magereza nchini humo amesema wamepeleka helikopta tatu na askari wanaotembea kwa miguu kuwasaka wafungwa hao. Wawili kati yao wamepigwa risasi na kufa. Inasemekana wafungwa hao walitoroka na bunduki 15 pamoja na risasi. Jengo la gereza hilo liko kwenye eneo la mlima Moroto pembeni mwa mji huo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, wafungwa walivua sare zao za jela za rangi ya manjano na kukimbia uchi milimani kuepuka kubainika. Inaaminika kuwa wafungwa hao walikuwa wakijaribu kutumia njia ya milimani kuvuka ili waweze kuvuka mpaka waingie Kenya.
Gereza hilo ambao kwa kawaida huwahifadhi wafungwa 600, kwa sasa limefungwa huku uchunguzi ukiendelea kubaini ni vipi wafungwa hao walivunja gereza na kutoroka. Jeshi limetuma picha ya msako dhidi ya wafungwa hao.
