The House of Favourite Newspapers

Wazungu Waleta Kufuru Yanga, Kujenga Uwanja

Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga Dk Mshindo Msolla.

KUNA kitu cha kushtua kinakuja Yanga kutoka kampuni moja ya Ulaya inayojihusisha na ishu za ujenzi ikielewana na Yanga kuna bonge la sapraizi linakuja kwa mashabiki. Huenda kikatokea kitu ambacho hakikuwahi kutokea ndani ya ardhi ya Tanzania tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

 

Uchunguzi wa timu ya Spoti Xtra umebaini kwamba Yanga ina ofa ya kufuru mkononi kutoka kwa kampuni moja ya ujenzi ya Ulaya inayoitwa Patel Engeneering.

 

Habari zinasema kwamba kampuni hiyo maarufu ya England kwa ujenzi wa viwanja vyua michezo, imeomba kazi Yanga na makadirio yao ni kuwa ujenzi huo utagharimu Sh Trilioni 1, Bil 147 na ushee sawa na Dola Milioni 500.

Mmoja wa viongozi wa Yanga aliidokeza Spoti Xtra kwamba Septemba 23 walipokea barua kutoka kwa kampuni ya Patel Engeneering ikiomba kuingia makubaliano na Yanga juu ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa mazoezi na mechi pale Jangwani.

 

Mbali na hivyo kiongozi huyo anasema kwamba ujenzi huo wa kisasa utahusisha hosteli na hoteli inayoweza kulaza mamia ya watu tena pamoja na maduka ya maana.

 

Kubwa kuliko ni kwamba Spoti limedokezwa kwamba Patel Engeneering wanataka Uwanja huo wa Jangwani uingize mashabiki 65,000 ikiwa ni 5000 zaidi ya Uwanja wa Taifa ambao ndio mkubwa na wa kisasa zaidi nchini.

 

“Hiyo kampuni ya ujenzi wanasema imesajiliwa Uingereza na inaonyesha ipo kwenye nchi nyingi za Ulaya mpaka Afrika ipo Msumbiji na Eritrea,”kilisema chanzo chetu ndani ya uongozi huku akionyesha kwa mbali nakala ya barua waliyotumiwa huku akigoma kuisoma ndani kwa madai ni siri kubwa ya sekretarieti mpaka wakapokubaliana.

“Wao wanaomba kazi ya kufanya ujenzi wa kisasa pale Jangwani, watajenga Uwanja mkubwa zaidi ya Taifa, Hoteli ya maana lakini yote hayo yatakuwa kwenye makubaliano maalum ya miaka zaidi ya 20.

 

Wao wataendesha Uwanja na kila kitu kibiashara kwa makubaliano maalum mpaka fedha irudi. “Wao watasimamia kila kitu,lakini na klabu itanufaika kimapato pia.

 

Sisi tukishakubaliana nao na kuwapa kazi ndio watakuja Tanzania kuweka sawa hayo mambo mengine ya kimkataba na kampuni yao kila kitu kitakuwa hapa,”alisema kiongozi huyo.

 

Kiongozi huyo ameongeza kuwa Wazungu hao wamewapa masharti kwamba kama wameipenda ofa hiyo ya ujenzi mpaka Novemba 30 wawe wamethibitisha kwa maandishi vinginevyo itakuwa imemalizika muda wake.

 

Hakuna kiongozi yoyote wa juu wa Yanga aliyekuwa tayari kufafanua kwa kina ishu hiyo jana, lakini Spoti Xtra limejiridhisha kwamba bado wanatafakari kwavile ni kitu kipya na kinachohitaji umakini kwavile ni ya miaka mingi. Kama dili hiyo ya Yanga ikikamilika inamaanisha kwamba klabu hiyo itaingia kwenye historia ya kuwa klabu ya kwanza kumiliki uwanja, hosteli na hoteli za kisasa zaidi Barani Afrika.

MWANDISHI WETU, Dar es Salaam

Comments are closed.