WIMBO MZURI HUMBEMBELEZA MTOTO

ENDELEA kuamini kopo la msalani wakati wenzako tunaliamini taulo, kwanza linatunza siri, hata urudie kujifutia sehemu hiyohiyo halisemi kitu, upo nyonyo? Wahenga wanasema kinywa cha mkubwa kinanuka lakini maneno hayanuki.  Shuuuutuuu dada mwanamke tabia babu wee, mwanamke kujua mumeo anataka nini, mwanamke kujituma kwenye kiwanja kifupi cha sita kwa sita.

Unasahau cha kumvutia mwanaume unakimbilia kuukoboa mwili, nani kakuambia weupe mali basi mkaa usingenunuliwa.Tena leo n’nakazi na wewe, nani kakuambia weusi ni laana. Basi leo nataka nikuambie wewe usio na haya uliyemaliza vipodozi mwisho wa siku uso unakuparama kama mchawi mzee, unalo hilo!

Siri ya weusi maana yake ni  utamu hata zambarau tamu ni nyeusi, zabibu tamu ni nyeusi na hata usingizi mtamu unapatikana usiku mweusi. Huoni Mzungu akimuonja mswahili anachanganyikiwa. Heeee heeeeiyaaaaa! Wewe unajikoboa mzungu ajipake masizi? Fyaaaaatuuuuu!

Nimejikuta hata nikisahau kuelezea nilichokikusudia kwa ajili ya malimbukeni wachache, jivunie weusi wako babu wewe! Tuachane na hayo ambayo kwa kiasi nimejikuta nikipandwa na mzuka na kujiingiza kwenye mada nyingine. Kama unabisha mwangalie jirani yako anayetumia mkorogo ngozi kama kuku wa mayai aliyezeeka badala ya kupendeza anabakia kituko mtaani.

Acha niendelee na kilichonitoa nyumbani, shoga leo nilitaka kukuelezea kitu kimoja kuhusiana na tabia za baadhi ya wanawake kukosa lugha tamu ndani ya nyumba zao kushindwa kuwalisha waume zao nyama ya ulimi. Mwanamke unakosa lugha tamu kwa mumeo hujui kusema asante, hujui kusema samahani, hujui hata kumsifia mumeo.

Mumeo akikuletea kitu unakipokea na kuamini ni wajibu wake kukuletea una hiyari ya anakuja baada ya kumpokea unabakia kama bubu, unabaki kama taa ya choo cha wapangaji haijulikani muda gani itazimwa! Haipendezi shoga yangu, tumia ulimi wako kumliwaza mumeo.

Mpo katika safari ya huba, mkifika pwani lazima mpeane pole na asante kwa kusafiri salama, pengine wewe umewahi mwenziyo naye anakufuata, msaidie naye afike na baada ya kufika mpe pole na asante kwa kukusafirisha vyema.

Usiwe mvivu wa kuomba msamaha unapokosa, hata kosa lenyewe liwe dogo, kumbuka kosa ni kosa na chanzo cha moto ni cheche. Wapo wachache lugha tamu huzitumia kwa muuza genge ili apunguziwe lakini kwa mumewe vitu hivyo havionekani. Shuuutuuuu!

Shoga tumia ulimi wako kujenga nyumba yako kumfanya mumeo aone tofauti ya mwanamke wa nje na mkewe ambaye kila neno tamu na zuri humwambia mumewe. Nyama ya ulimi ukiitumia vizuri itakufanya kila siku penzi lako lizidi kuwa tamu, si wajinga waliosema sauti tamu ilimtoa nyoka pangoni na kumtuliza simba mwenye njaa.

Yangu si mengi kwa leo, ila kumbuka wimbo mzuri humbembeleza mtoto akalala. Ni mimi Shangingi Mstaafu Anti Nasra!


Loading...

Toa comment