Kartra

Yanga: Tunaanza Ligi Kibabe

YANGA imepania kwelikweli kuhakikisha msimu unaoanza kesho wanatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Jumapili iliyopita, Yanga ilimtambulisha kocha mkuu mpya Mserbia, Zlatko Krmpotic ambaye amechukua nafasi ya Luc Eymael aliyetimuliwa kutokana na mambo ya kibaguzi.

 

Yanga ambayo ina uchu wa kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kuukosa kwa misimu mitatu mfululizo, imeamua kufanya usajili wa kiwango cha juu ambapo itafungua dimba kesho kwa kuwakaribisha Prisons kwenye Uwanja wa Mkapa saa 1 usiku.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amefunguka kuwa, uongozi wa klabu hiyo umejipanga kikamilifu msimu huu kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ambao wameukosa kwa misimu mitatu mfululizo.

“Usajili tulioufanya msimu huu sio wa kitoto, umezingatia matakwa yote ya timu, wachezaji wapo katika kiwango kizuri tunachohitaji ni kuona tunafanikiwa kufanya vizuri kwenye ligi na kutwaa ubingwa mwisho wa msimu.

 

“Usajili ambao tumeufanya hatujaufanya katika kipindi cha misimu mitatu mfululizo, hivyo tunahitaji kufanya vizuri zaidi kwa kushirikiana benchi la ufundi, wachezaji na uongozi kwa ujumla ili pate matokeo mazuri,” alisema Mwakalebela.

 

KUWAKOSA WAWILI

Katika mechi ya kesho, Yanga itawakosa wachezaji wawili ambao ni beki wa kati, Lamine Moro aliyejitonesha goti na Balama Mapinduzi aliumia enka na sasa ameanza mazoezi ya kutembea.

Stori: Khadija Mngwai, Dar es salaam


Toa comment