The House of Favourite Newspapers

YANGA Kufumua Kikosi Kusajili 7 Wapya

YANGA haitaki masihara imepanga kufumua kikosi kizima kwa kusajili wachezaji wapya saba kwenye usajili wa dirisha dogo la msimu huu wa Ligi Kuu bara linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 16, mwaka huu kabla ya kukutana na watani wao Simba, Januari 4, mwakani.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo iondolewe kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na Pyramids FC ya nchini Misri baada ya kufungwa ugenini mabao 3-0 zikiwa ni siku chache baada ya kupata kichapo cha mabao 2-1 hapa nyumbani.

 

Wachezaji wanaotajwa hivi sasa katika usajili wa dirisha dogo ni beki wa timu ya taifa ya Rwanda na klabu ya Rayon Sports, Erick Rutanga, mshambuliaji wa Coastal Union, Ayoub Lyanga, Haruna Niyonzima anayecheza AS Kigali na Haji Mwinyi ambaye kwa sasa yupo KMKM.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Kamati ya Ufundi ya Yanga tayari imekamilisha ripoti yake ya mapendekezo ya usajili kwa kuhakikisha inasajili wachezaji saba wapya, huku ikiwaacha baadhi kutokana na kutokidhi viwango katika timu hiyo.

Mtoa taarifa alisema kuwa katika usajili wao wa wachezaji, wataanzia safu ya ushambuliaji ambayo ndiyo tatizo lililosababisha wao waondolewe kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kutokana na kutokuwa na viwango.

 

Aliongeza kuwa baada ya kuifanyia maboresho safu ya ushambuliaji watahamia kwa kiungo kwa kusajili wachezaji wenye uwezo wa kuchezesha timu ikiwemo kupiga pasi za mwisho za kufunga mabao na Niyonzima akitajwa kurejeshwa kucheza nafasi hiyo. “Lipo wazi usajili uliofanywa na kocha wetu Zahera haujakidhi viwango tulivyokuwa tunavihitaji na hilo limeonekana uwanjani katika mechi za kimataifa na ligi ambazo tumezicheza.

 

“Wachezaji wameshindwa kuitumikia timu ipasavyo, hivyo upo uwezekano wa kuwapunguza nusu ya wachezaji wapya tuliowasajili katika usajili mkubwa kwa maana ya kuachana nao kabisa wakiwemo washambuliaji.

 

“Wapo baadhi ya wachezaji wa kimataifa kama Lamine (Moro), Shikalo (Farouk) ni kati ya waliotimiza majukumu yao vizuri, hivyo ni ngumu kuachana nao zaidi tutawangalia washambuliaji pekee,” alisema mtoa taarifa huyo. Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alilizungumzia hilo juzi mchana kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar mara aliporejea na timu hiyo akitokea Misri kucheza na Pyramids FC.

 

“Timu inatakiwa iwe katika mfumo bora wa uendeshaji, mfumo wa hisa, usajili mzuri wa wachezaji wenye ubora kitaifa na kimataifa. Nadhani tutafanya kitu kwenye dirisha dogo pia mchakato wa kuingia katika hisa ukiendelea. “Hivyo kama viongozi tunahitaji muda zaidi wa kukiimarisha kikosi chetu na hilo lipo wazi kabisa, lazima tufanye usajili dirisha dogo utakaoendana na hadhi ya Yanga,” alisema Mwakalebela.

STORI NA WILBERT MOLANDI | CHAMPIONI JUMATANO

Comments are closed.