The House of Favourite Newspapers

Zahera: Tunawalipua Lipuli na Tunachukua Kombe

Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongo mani, Mwinyi Zahera amesema kuwa ni lazima wawafunge wapinzani wao Lipuli FC watinge fainali na wachukue Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).

Yanga inatarajiwa kuvaana na Lipuli leo Jumatatu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho utakaopigwa kwenye Uwanja wa Samora huko Iringa.

 

Timu hizi katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara, Yanga ilifungwa bao 1-0 lililofungwa na beki, Haruna Shamte kwenye Uwanja wa Samora.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na kikubwa wanachosubiria ni pambano hilo na kikubwa zaidi wanahitaji ushindi.

 

Zahera alisema, katika mchezo huo tayari amewapa majukumu na mbinu za ushindi mabeki na mawinga wakati wakiwa na mpira na kikubwa amewataka kupiga krosi safi zitakazowafikia washambuliaji wake kwa ajili ya kufunga.

Aliongeza kuwa, katika mchezo huo anafurahi kumuona beki wake tegemeo, Kelvin Yondani akirejea uwanjani baada ya kumaliza kifungo chake cha kufungiwa michezo mitatu baada ya kupewa kadi nyekundu ya moja kwa moja.

 

“Tayari nimekamilisha maandalizi ya kikosi changu ambacho kipo tayari kwa ajili ya ushindi katika mchezo muhimu wa nusu fainali.

“Katika mchezo huu, ni lazima tupate matokeo mazuri ya ushindi kwa kuwafunga Lipuli ili tuingie fainali na tuchukue kombe na hilo linawezekana kwetu.

“Nafahamu Lipuli wameupania mchezo huu, tayari nimeshawaambia vijana wangu katika hilo, kikubwa nimewataka kucheza kwa nidhamu kubwa ya kushambulia na kulinda goli ndani ya wakati mmoja,” alisema Zahera.

 

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam.

Comments are closed.