The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness -24

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake.

Arianna anaokotwa na vikosi vya uokoaji na kurejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango na kwenda kuishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge, Mathare jijini Nairobi baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anauza kinyemela nyumba aliyoachiwa na wazazi wake na kutorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kipekee ya kukutana na mfanyabiashara mkubwa wa madini ya Tanzanite, Msuya ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba Arianna na Diego walikuwa ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba wawili hao ni wapenzi.

Uongo wao unafanikiwa na hatimaye wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya. Anatumia ujanja mkubwa na kusababisha wakutane kimwili usiku huohuo.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Japokuwa ndani ya nafsi ya Msuya alikuwa akijilaumu kwa kukutana kimwili na Arianna bila hata kuchukua tahadhari yoyote, upande mwingine alijipongeza kwani alichokuwa amekihisi tangu siku ya kwanza alipoonana na msichana huyo, hakuwa amekosea. Akajiapiza kuwa atafanya kila kinachowezekana ili kuhalalisha uhusiano wao.

Alikuwa ni kama amelamba asali na sasa alikuwa tayari kuchonga mzinga, hakukumbuka tena suala la kwenda kupima afya zao.

Msuya aliendelea kutafakari mambo kadhaa pale kitandani, huku hisia tamu za mapenzi zikipita ndani ya moyo wake, alijikuta akizidi kumpenda Arianna kutokana na mapenzi matamu aliyopewa usiku wa siku hiyo.

Muda mfupi baadaye, aliwaagiza wafanyakazi wake kuandaa kifungua kinywa cha kipekee kisha kwenda kumuamsha Arianna.

Sauti ya mlango uliokuwa ukigongwa ndiyo iliyomzindua Arianna kutoka kwenye usingizi mzito, akakurupuka na kujikuta akiwa amelala peke yake, akatazama huku na kule na kujinyoosha kwa uchovu. Akainuka na kwenda kufungua mlango.

“Za asubuhi Arianna,” mfanyakazi wa ndani wa Msuya alimsalimu kwa heshima ya hali ya juu, akamuitikia kwa uchangamfu ambapo alimwambia kwamba kifungua kinywa chake kipo tayari, achague kama aletewe chumbani au ataenda kulia ‘dining room’.

Arianna aliomba akaandaliwe sebuleni ili na yeye apate muda wa kuoga na kukiweka vizuri chumba chake, jambo ambalo mfanyakazi huyo alilikubali. Alipoondoka, Arianna alianza kukumbuka kilichotokea usiku na kujikuta akitabasamu mwenyewe.

Hakukumbuka Msuya aliondoka saa ngapi chumbani kwake kwani kitu pekee alichokuwa anakikumbuka ni kwamba walilala pamoja usiku baada ya mpambano mkali wa kirafiki, usio na refa wala jezi.

“Hapa umefika Msuya, nitahakikisha unazama kabisa kwenye penzi langu, mimi ndiyo Arianna,” alijisemea msichana huyo huku tabasamu pana likiwa limeutawala uso wake, harakaharaka akaenda kuoga kisha akarudi na kuanza kujiandaa kwa ajili ya kwenda kupata kifungua kinywa.

Alipofika sebuleni, alimkuta Msuya tayari ameshakaa mezani, akimsubiri. Akainuka na kumkumbatia kwa mahaba huku akimshukuru kwa ‘huduma’ nzuri aliyompa usiku uliopita.

“Kwani uliondoka saa ngapi? Mi nashtuka nakuta nimelala peke yangu,” aliuliza Arianna kwa sauti ya chini wakati Msuya akimsogezea kiti cha kukaa, akashindwa kujibu swali hilo zaidi ya kucheka kwa furaha.

Walipata kifungua kinywa pamoja huku wakizungumza kimahaba na kufurahi pamoja, ndani ya muda mfupi tu tangu walipofahamiana, wawili hao walikuwa tayari wameshazoeana utafikiri walifahamiana miaka mingi iliyopita.

Baada ya kupata kifungua kinywa, Msuya alimuomba Arianna akaendelee kupumzika wakati yeye akienda kujiandaa kwa ajili ya kwenda kwenye shughuli zake za kila siku.

“Naomba nikakusaidie kukuandaa mume wangu kama hutajali,” alisema Arianna, Msuya akakosa cha kujibu zaidi ya kutingisha kichwa kuonesha kukubali alichoambiwa. Wakaongozana na kupanda ngazi kuelekea kwenye chumba cha Msuya kilichokuwa ghorofani.

Arianna alishindwa kujizuia kushangaa jinsi chumba hicho kilivyokuwa kizuri, kikiwa kimesheheni vitu vingi vya kifahari, kuanzia kitanda kikubwa cha kisasa mpaka makabati ambayo Arianna hakuwahi kuyaona sehemu yoyote.

“Hiki ndiyo kitakuwa chumba chako, kila kitu unachokiona hapa ni chako,” alisema Msuya, Arianna akafurahi sana na kumkumbatia tena Msuya, katika hali ambayo hakuna aliyeitegemea, wawili hao waligusanisha ndimi zao na kujikuta wakianza kuelea kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Kwa mara nyingine, wakajikuta wakikutana kimwili huku Msuya akionesha kufurahishwa mno na kila kitu alichokuwa anafanyiwa na Arianna. Baadaye, wote wawili walienda kuoga kisha Arianna akaanza kazi ya kumuandaa Msuya, ikiwa ni pamoja na kumchagulia nguo za kuvaa ambazo zilimpendeza sana.

“Wewe ni mwanamke wa kipekee sana Arianna, hata marehemu mke wangu hakuwa akinijali kama unavyofanya wewe, nakupenda sana na naahidi kukupenda kwa moyo wangu wote,” alisema Msuya, Arianna akamkumbatia na kumbusu mdomoni kisha wakatoka ambapo Arianna alimsindikiza Msuya mpaka kwenye maegesho ya magari.

Mwanaume huyo akachagua gari moja la kifahari kati ya mengi yaliyokuwa yamepaki, akaingia kwenye Jeep Grand Cherokee la kisasa na kuondoka taratibu huku akimpungia mkono Arianna ambaye alimsindikiza kwa macho mpaka alipotoka getini, msichana huyo akarudi chumbani kwake na kwenda kuendelea kupumzika, huku akijipongeza kwa jinsi mpango wake wa kumteka Msuya kimapenzi ulivyoonesha mafanikio ya haraka.

“Arianna, jana ulilala na Msuya si ndiyo?” bila hata salamu, Diego alimuuliza Arianna walipokutana asubuhi hiyo, kauli ambayo ilimshangaza sana Arianna kwa sababu alijua kwamba ilikuwa siri yake na Msuya.

“Usitake kunidanganya kwa chochote, usiku mimi nilikuja chumbani kwako wakati watu wote wamelala, nikafungua mlango kimyakimya na kuwakuta mkiwa mmelala, kwani hayo ndiyo makubaliano yetu?”
“Diego utasababisha mambo yote yaharibike. Kwani makubaliano yetu yalikuwaje? Si tunataka pesa si ndiyo?”
“Tunataka pesa ndiyo lakini lazima ujue kwamba nakupenda Arianna, usiuumize moyo wangu kwa makusudi.”

“Sasa Diego, wewe unataka mimi nifanyeje? Ndiyo kwanza tumehamia hapa nyumbani kwake na tayari umeshaanza kuleta wivu, unafikiri akitushtukia kwamba tuna uhusiano wa kimapenzi itakuwaje?” Arianna aliongea huku akionesha kukasirishwa na kitendo cha Diego kumuonea wivu.

Kijana huyo akaondoka huku wakiwa hawajafikia muafaka wowote. Ilibidi Arianna awe na msimamo mkali kwa sababu kama angeruhusu wivu wa Diego uendelee, maana yake ni kwamba wangeyarudia maisha yao yaleyale ya tabu, jambo ambalo hakuwa tayari kuona linatokea.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Leave A Reply