×

Unending Love- 84

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet anayetokea familia ya kimaskini na Anna anayetokea familia ya kitajiri. Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana na kuahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo yake moja kushindwa kufanya kazi.

Jafet anaamua kujitolea figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, baadaye wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet kutokana na umaskini wake wakidhani hana hadhi ya kumuoa Anna.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William ambaye baadaye anampa ujauzito na kumkataa.

Anna anarejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa tena mpaka nchini India na Jafet anafuatwa Tanzania baada ya hali ya mgonjwa kuwa mbaya.

Jafet anapowasili India, japokuwa Anna alikuwa na hali mbaya, hali yake inaanza kuimarika kwa kasi na kumshangaza kila mmoja. Ndani ya muda mfupi tu, anapata ahueni kubwa ambapo baadaye anaruhusiwa kutoka hospitalini hapo.

Wanafunga safari ya kurejea Tanzania na hatimaye wanawasili jijini Mwanza kisha siku inayofuatia wanaelekea kijijini Rwamgasa, nyumbani kwa wazazi. Hilo wanalikamilisha na mwisho wanasafiri mpaka jijini Dar es Salaam kufuatilia uhamisho wa Jafet chuoni ambapo kijana huyo anamuandikia ujumbe mzito mpenzi wake wa chuoni hapo, Suleikha.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Baadaye, Jafet aliamua kupiga moyo konde na kumuita msichana mmoja aliyekuwa akiishi hosteli moja na Suleikha.

“Hee! Jamani Jafet! Si nilisikia umesafiri kwenda India? Umerudi lini? Karibu sana!”
“Nimerudi dada’angu, kuna jambo naomba unisaidie. Suleikha yupo hosteli?”
“Yupo, tena muda si mrefu alikuwa anakuzungumzia, amekumisije? Bila shaka atafurahi sana kukuona ngoja nikamuite,” alisema msichana huyo huku akigeuka na kutaka kuondoka kwa kasi lakini Jafet alimzuia.

“Hapana, shida yangu siyo kuonana naye kwa sababu nitaondoka muda si mrefu. Leo sijaja rasmi, naomba ukampe huu ujumbe lakini usubiri kidogo mpaka nitakapokuwa naondoka kama baada ya dakika kumi hivi ndiyo umpe,” alisema Jafet huku akimkabidhi msichana huyo bahasha ya khaki, jambo lililomfanya abaki amepigwa na butwaa.

“Nakuomba ufanye kama nilivyokwambia tafadhali,” alisisitiza Jafet kisha akaagana na msichana huyo. Kwa bahati nzuri, baba yake Anna naye tayari alikuwa ameshamaliza taratibu zote za uhamisho, wakaondoka pamoja mpaka kwenye maegesho ya magari ambako teksi iliyowaleta ilikuwa ikiwasubiri.

Yule msichana aliyepewa bahasha na Jafet bado alikuwa amesimama palepale akiwasindikiza kwa macho Jafet na baba yake Anna mpaka walipoingia kwenye teksi na kuondoka eneo hilo. Akaitazama ile bahasha aliyopewa kisha akashusha pumzi ndefu na kuondoka haraka kuelekea kwenye hosteli waliyokuwa wanaishi.

“Suleikha! Suleikha!” aliita msichana huyo na kumfanya Suleikha aliyekuwa amejilaza kitandani akichezea simu yake ainuke haraka.
“Vipi mbona unaniita hivyo? Kuna nini kwani?”
“Jafet amekuja.”

“Jafet! Mungu wangu, yuko wapi?”
“Ameshaondoka ila ame…” Suleikha hakusubiri rafiki yake huyo amalizie alichotaka kukisema. Kwa kasi kubwa alitoka na kukimbilia mpaka kwenye jengo la mapokezi lililokuwa jirani na geti la kutokea nje ya eneo la chuo, huku akiwa na shauku kubwa ya kutaka kumuona Jafet. Alijihisi kama yupo ndotoni.
Kwa jinsi alivyokuwa amemkumbuka, hakuona hatari kukimbia huku akiwa pekupeku kwani alihisi kitendo cha kwenda kutafuta viatu kitamchelewesha.

“Eti mmemuona Jafet hapa?”
“Ooh! Ndiyo! Wapo kwenye ile teksi kule inayotoka getini, sidhani kama utamuwahi,” alisema mwanachuo mwingine aliyekuwa amekaa chini ya kivuli cha mti, akijisomea. Suleikha alipooneshwa tu ile teksi, alizidi kutimua mbio na kukatisha kwenye bustani za maua huku akipunga mikono na kulitaja jina la Jafet.

“Nasikia kama kuna mtu anakuita, ni nani?” baba yake Anna alisema na kumuamuru dereva kupunguza mwendo, jambo ambalo alilitii kwani bado hawakuwa wametoka nje ya geti la kuingilia chuoni hapo.
“Dereva twende! Twende tu.”

“Hapana Jafet, huoni mwenzio anakuita huku akilikimbilia gari? Halitakuwa jambo jema kuondoka, dereva simama tafadhali,” alisema baba yake Anna, kauli iliyomfanya Jafet ajiinamie chini na kukosa cha kujibu.

Sekunde chache baadaye, tayari Suleikha alikuwa ameifikia ile teksi, akawa anahangaika kufungua mlango wa nyuma, upande aliokuwa amekaa Jafet, akawa anagongagonga vioo. Kwa shingo upande, Jafet alifungua mlango na kutoka nje, msichana huyo akamkumbatia kwa nguvu huku maneno mengi yakimtoka.

“Jamani mpenzi wangu! Siamini kama umerudi salama, mbona ulikuwa unataka kuondoka bila kuonana na mimi? Ooh! Ahsante Mungu kwa kunirudishia mume wangu,” alisema Suleikha huku machozi ya furaha yakimtoka.

Jafet alibaki kimya kama amepigwa na shoti ya umeme. Kwa maneno aliyokuwa anayasema Suleikha, ilionesha moja kwa moja kwamba hakuwa ameusoma ujumbe alioandikiwa na Jafet muda mfupi uliopita.

“Vipi Jafet! Uko sawa kweli, mbona kama haupo hapa kimawazo?” alisema msichana huyo kwa mshangao baada ya kupata mapokezi ambayo hakuyategemea kutoka kwa Jafet.
“Kuna matatizo mpenzi wangu ndiyo maana nilikuwa nataka kuondoka bila hata kuonana na wewe.”
“Matatizo gani tena mpenzi,” alihoji Suleikha huku akizidi kumkumbatia Jafet na kumbusu kimahaba.

akuna jambo ambalo hakuwa akipenda kuliona kama kumuona mpenzi wake huyo akiwa hana raha moyoni mwake. Hakujua kwamba kwa wakati huo, yeye ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya kumfanya Jafet awe kwenye hali hiyo.

“Mama anaumwa nyumbani, hivi ndiyo tunaelekea huko,” ilibidi Jafet adanganye.
“Ooh! Pole sana mpenzi wangu, naomba basi tuwasiliane kwa simu kwa sababu tayari umesharudi Tanzania. Namba yako si ni ileile?” Suleikha aliuliza huku na yeye akibadilika na kuvaa uso wa huzuni, akionesha kuguswa mno na ule uongo wa Jafet.

Jafet akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye lakini akikwepesha macho yake. Wakiwa bado wamesimama palepale, baba yake Jafet na dereva teksi wakiwa wametulia ndani ya gari wakiwatazama, yule msichana aliyepewa ujumbe wa kumpelekea Suleikha alifika eneo hilo huku na yeye akitweta kuonesha kwamba alikuwa akikimbia kumfuata Suleikha.

“He! Kumbe mmekutana?” alisema msichana huyo na kusababisha Jafet amgeukie, akamuona bado ameishika ile bahasha mkononi, akaonesha ishara akimtaka ampe, jambo ambalo yule msichana alilitii, akamkabidhi Jafet bahasha yake.

“Suleikha!”
“Abee mume wangu.”
“Naku…penda sa..na m…mpenzi wa..ngu…” alisema Jafet kwa kubabaika huku akionesha kwamba kuna jambo zito alikuwa akitaka kumwambia Suleikha lakini alikosa ujasiri.

“Nakupenda pia Jafet! Basi nisikucheleweshe mpenzi wangu, nenda kashughulikie matatizo ya mama tutawasiliana,” alisema Suleikha na kumuachia Jafet, akarudi ndani ya gari akiwa ameshika bahasha yake huku machozi yakimmiminika mithili ya mtu aliyepokea taarifa za msiba.

Alipoingia kwenye teksi, baba yake Anna alimwambia dereva awashe gari, taratibu wakaondoka eneo hilo huku Suleikha na yule rafiki yake wakiwapungia mkono mpaka walipopotea kwenye upeo wa macho yao.

“Usilie Jafet! Jikaze, wewe ni mwanaume, sote tumepitia huko,” alisema baba yake Anna huku akimpigapiga Jafet mgongoni, kitendo kilichosababisha azidi kulia kwa uchungu. Alijikuta akiwa katika wakati mgumu mno kihisia, hakujua afanye nini kwa wakati huo.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Jumatano.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

3 Comments

  1. Be strong and make decisions,,, true lov is btn two ppo,,, think of how yu feel wen ur with anna and wen with suleikha,, then that feeling wil direct you to whom yu love the most btn the two

Leave a Comment