The House of Favourite Newspapers

Walioishi ardhini-2

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Tulipozama tena umbali uleule tukasikia sauti zikisema; ‘jamani hatujafa, tuko hai.’ Tulizitambua sauti hizo ikabidi tuite majina ya wale waliofukiwa kama ndiyo wenyewe. Mimi nilimwita Joseph, akaitika, nikarudia mara tatu, naye akaniita Mussa. Ndipo tukatoka nje kwenda kutoa taarifa kwa uongozi wa mgodi.”
WIKI HII INAENDELEA…

Mussa, mmoja wa vijana wawili walioingia mgodini na kusikia sauti ya mmoja wa wachimbaji, anaendelea kusimulia:

“Tulivyotoa taarifa hiyo, uongozi wakawachukua wachimbaji wengine kuingia ndani kuhakikisha kama jambo tulilolisema lina ukweli wowote! Walioingia, wakatoka, wakathibitisha kwa uongozi, lakini bado hawakuamini.

“Wakaingia wengine tena kwa mara ya mwisho ili kujiridhisha zaidi, nao walitoka wakiwa na majibu kama ilivyokuwa taarifa yetu. Hapo ndipo uongozi ukakubali na tukaanza kazi ya kuwaokoa ndugu zetu.

WATOLEWA WAKIWA DHAIFU
“Tulifanya kazi hiyo usiku na mchana kwa kushirikiana na wachimbaji wote mpaka ilivyofika majira ya saa 11 alfajiri ya Jumatatu, Novemba 16, (mwaka huu) tukawa tumewaokoa na kuwakimbiza katika Hospitali ya Kahama wakiwa hawana majeraha, lakini afya zao zilikuwa dhaifu sana.

“Unajua kuishi katika shimo lenye urefu wa mita 115 kwa muda wa siku zote hizo (41) bila kula wala kunywa maji halisi ni jambo ambalo lilitushangaza sana kutokea kwa tukio hili katika mgodi huu. Kweli Mwenyezi Mungu anaweza kila jambo kwa viumbe wake.

“Sisi kutokana na kuokoa maisha ya wenzetu hawa tunaiomba serikali kutukumbuka kutokana na ushujaa tuliouonesha katika jambo hili. Angalau tuweze kujisikia kama mashujaa. Tunajua hakuna yeyote atakayeweza kutulipa bali Mungu mwenyewe.”

WAATHIRIKA WENYEWE
Baada ya kuzungumza na mashuhuda hao, Uwazi lilifika Hospitali ya Wilaya ya Kahama na kufanikiwa kuzungumza na walioathirika na tukio hilo ambao ni Joseph Burure (42), Amos Hangwa (25), Msafiri Gerald (38), Chacha Wambura (54) na Onyiwa Kado (55) ambaye alifariki dunia hospitalini hapo Jumapili iliyopita:

Burure: “Siku ya tukio, ndani ya shimo tulikuwa watu sita ambao sisi tulikwenda kuwaokoa wenzetu waliokwama baada ya shimo kutitia. Lakini wakati tumemaliza shughuli ghafla gema la ukuta wa mgodi lilianguka na kuziba mlango wa kutokea.

“Tulitaharuki sana, tulichojua ni vifo vinafuata kwetu. Kila mmoja alilia kivyake. Tulimwomba Mungu tukio lile liwe miujiza kwetu, yaani atufanyie lolote la ajabu tutoke.
“Pale mahali tulipokuwa ni padogo sana, naweza kusema ni Mungu tu ndiye anajua. Ilikuwa ni mahali ambapo kati yetu hakuna aliyeweza kusimama wala kunyoosha miguu. Tulivyokuwa tumekaa ni hivyohivyo.”

WAANZA KULA MENDE, VYURA
“Bahati nzuri tulikuwa na maji na baadhi ya vyakula lakini tulivitumia vikatuishia nadhani ndani ya siku mbili tu. Nasema nadhani kwa sababu kule hatukuwa tunajua siku imeisha au giza limeingia wala jua kutoka.

“Njaa ilipozidi, ndipo tukashauriana tuanze kula magome ya miti iliyokuwa ndani ya shimo (angalia picha ya magogo chini). Lakini pia tukaona tule na mende, vyura na wadudu wengine lakini kabla ya kuanza kula vyakula hivyo tulimwomba Mungu kwanza ili vyakula hivyo visituletee madhara kiafya.

“Kweli, Mungu alisikia sala zetu kwani tulipokuwa tunakula vitu hivyo tulishiba kama vile tumekula vyakula vya kawaida.”

MMOJA AFIA SHIMONI
“Baada ya siku kadhaa, huenda ni ya 15 tukiwa bado ndani ya shimo, mwenzetu wa sita, Khamis Spana alituomba tusali sala ya kumuaga kwani alisema mwisho wa kuishi kwake umefika. Wote tukamwomba Mungu kwa ajili yake. Wakati anakata roho alituambia Mungu atatusaidia sisi tutatoka tu.

“Baada ya kifo chake, zilipita siku kadhaa, huenda ni tatu hivi, mwili wa marehemu Spana ulianza kuoza na kutoa harufu. Ilibidi tufunge kutokula kwa muda usiojulikana maana tulikuwa hatujui dakika, saa wala siku tutakapokufa. Pia tulifanya hivyo kwa ajili ya kumwomba Mungu apunguze ile harufu iliyokuwemo na kutuonesha njia ya kutoka katika shimo lile.

”Kweli, Mungu alisikia maombi yetu kwani ile harufu ilitoweka ghafla na tukaendelea kuishi tukiwa na matumaini ya siku moja kutoka.

HEWA YA AJABU
“Kilichokuwa kikitufanya tuamini ipo siku tutatoka ni kupata hewa nzuri na tulikuwa na uwezo wa kusikia sauti za watu nje. Na kila tulivyokuwa tukisikia tulikuwa tunaita watusaidie na kweli Mungu alitusaidia kwa kutuonesha njia watu wengine kuja kutuokoa kama vile.

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.