Chemical; Mi’ Mgumu, Navaa Kigumu na Naimba Ngumu!

Chemical.

Na IMELDA MTEMA| GAZETI LA IJUMAA| IJUMAAA SHOWBIZ

Kwa hapa Bongo, unapowazungumzia wasanii wa kike wanaofanya fresh kwenye Hip Hop, jina la Chemical haliwezi kukosekana. Mdada huyu jina lake kamili ni Claudia Lubalo na hana siku nyingi sana kwenye game lakini fasta limemkubali na kumzoea.

Showbiz ilifanya mahojiano maalum na msanii huyu anayesumbua na wimbo wake uitwao Mary Mary ambapo amefungukia mambo mbalimbali kama unavyoweza kusoma hapa chini;

Showbiz: Mambo vipi Chemical, hivi ni kwa nini ulichagua kufanya Hip Hop na siyo muziki mwingine kama wanavyofanya wasichana wenzako?

Chemical: Unajua kwenye kitu chochote ili ufanikiwe, lazima ufanye tofauti. Nilipoamua kufanya muziki, niliona wasichana wengi wanaimba lainilaini, mimi nikaona nifanye Hip Hop na utofauti huo umenifanya nifike hapa nilipo.

Showbiz: Mtaani wanakusema kuwa, Hip Hop imekufanya uwe kama mwanaume kitabia na kimavazi pia, huoni kwamba hilo ni tatizo kwako?

Chemical: Ujue mimi nafanya muziki mgumu, hivyo sioni tatizo kuishi kigumugumu. Mavazi ya kiume wakati mwingine yananisaidia niwapo studio kwani muda mwingi niko na wanaume na kuna wakati tunalala huko, sasa wakiniona hivi wanajua mimi ni mgumu na siingiliki kirahisi.

Showbiz: Sasa huoni kukaa kidumedume kutakukosesha mwanaume wa kukuoa?

Chemical: Naamini kwa sasa nitakosa mwanaume wa kunichezea tu lakini naamini kwa hivihivi nilivyo naweza kupata wa kunioa.

Showbiz: Kwa hiyo unaamini siku moja na wewe utavaa shela na kuitwa mke wa mtu?

Chemical: Kabisa yaani naamini siku nikivaa shela nitapendeza sana.

Show-biz: Wazazi wako wanasemaje kuhusu wewe kufanya muziki huo ambao umekufanya uwe mgumu?

Chemical: Haikuwa rahisi sana mimi kufanya muziki, walinigomea lakini kwa kuwa ni kitu ambacho nilikuwa nakipenda, wenyewe wakaniacha na sasa wananipa sapoti.

Showbiz: Wapo wanaosema kuwa muziki unaofanya haulipi, unaishia kupata umaarufu tu, kwako unalizungumziaje hili?

Chemical: Siyo kweli kwa sababu, huwezi kufanya kitu ambacho hakikulipi. Hip Hop inalipa kama ilivyo miziki mingine.

Showbiz: Hufikirii kuja kufanya muziki laini baadaye?

Chemical: Ukiwa mwanamuziki unaweza kuimba vyovyote ila kwa sasa nafanya ngumu.

Showbiz: Mbali na muziki, nini ambacho unakifanya?

Chemical: Sasa hivi nasoma Chuo Kikuu cha Dar es Saalam, niko mwaka wa tatu nasomea mambo ya muziki.

Showbiz: Nakushukuru sana kwa ushirikiano wako na nikutakie kila la heri.

Chemical: Ahsante sana, nawe kazi njema!

 


Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment