The House of Favourite Newspapers

Sitamanai Tena Kupenda, Niliyempenda Amenitenda!

0

Na Gabriel Ng’osha | IJUMAA WIKIENDA | XX-Love

NIANZE kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa nafasi hii adimu ya kuzungumza na wewe msomaji wangu wa XXLove. Yapo mengi yaliyotokea na kutuumiza mioyoni mwetu, lakini hatuna uwezo wala mamlaka ya kuamuru yasitupate. Poleni mashabiki na wadau wa muziki kwa kuondokea na Mwanamuziki Dogo Mfaume aliyefariki dunia wiki jana. Sisi tulimpenda ila Mungu amempenda zaidi.

Tukirudi kwenye mada ya leo, ni dhahiri shahiri kuwa, mapenzi yameendelea na yanaendelea kuwatesa watu wengi sana duniani, bila kujali taifa, dini, kabila, umri, cheo, elimu wala rangi maumivu yake ni yaleyale kwa maskini na matajiri. Hivyo ukiumizwa jifunze kuziongoza hisia zako katika kuhisi maumivu ya kawaida kwa sababu si wewe pekee uliyeumizwa. Kumbe kuna maafisa, walimu, mawaziri, marais, wafanyabiashara, majiniazi, wanasanyansi, watumishi wa Mungu na wengineo ambao nao wanakutana na maumivu ya mapenzi. Je, unapokumbwa na hali hiyo nini cha kufanya?

 

1: USIKATE TAMAA

Nauona moyo wako ulivyopondeka na kufa ganzi kwa sababu uliyempenda amekutenda. Naiona michirizi ya majeraha kwenye moyo wako kwa sababu ya mateso ya mapenzi, lakini yote hayo yasikukatishe tamaa na kuamini kuwa huwezi kupenda na kupendwa tena katika maisha yako.

 

2: USIJIONE DHAIFU

Usife moyo na kujiona huu mpweke usiye na thamani katika ulimwengu wa mahaba. Usijifanye kuwa dhaifu kama kinda la ndege aliyemwagiwa maji na kushindwa kuruka kwa sababu mama yake amemuacha.

3: MFANYE DARAJA

Wewe bado una thamani kwa mtu aliyeumbwa kwa ajili yako. Aliyekuacha si wa kwako bali alikuwa kama daraja la kukuvusha kwenda kwa aliyezaliwa kwa ajili yako.

4: MUOMBEE MEMA

Wala usimchukie aliyekutenda, kukuacha au kukuumiza. Muombee mema kwa sababu kwa alichokufanyia kama utakichukua kama elimu, kitakusaidia sana katika uhusiano wako mpya. Ninaposema mpya simaanishi unapoachwa basi kesho yake ukurupuke na mpenzi mwingine. Hapana, tuliza akili yako, jiulize sababu za kuachwa au kuachana kisha chukua tahadhari kwa mpenzi ajaye.

5: SIYO ULIYEUMBIWA

Amini nakuambia, aliyekutenda si uliyeumbiwa na Mungu kwa kuwa mwenye mapenzi ya dhati hayuko tayari kuona mpenzi wake akiumwa, akiteseka kwa ajili yake. Hawezi kuvumilia mpenzi wake akidharauliwa, akinyanyaswa na kila aina ya maumivu. Anayekupenda kwa dhati lazima atakupigania hata kama hana nguvu, basi atatumia njia mbadala kuhakikisha akupendaye unakuwa salama.

6: ONDOA CHUKI, JIFUNZE

Kuumizwa na uliyempenda kusikufanye ukawachukia wanaume au wanawake wote kwa sababu si wote wako hivyo. Cha msingi ni kujifunza kwenye maumivu hayo.

Katika hili wapo wanaoamini kuwa wanaoteseka zaidi ukilinganisha na wanaume. Inawezekana ni kweli kwa sababu wanawake huonesha moja kwa moja mateso yao hasa pale wanapokuwa hawana la kufanya. Ikitokea mwanamke akaumizwa na mumewe kisha akamtimua anapoishi, mwanamke asiyejielewa huanza kutangatanga, hali inayoonekana moja kwa moja kwa jamii. Hata wanaume wasiyotamani kupenda tena wapo ila tu kilio chao ni kama cha samaki kulilia kwenye maji.

Leave A Reply