
Wakazi wa Kyiv wa rika zote – watu wazima na watoto – walielekea tena chini ya ardhi jana usiku wakati mji huo mkuu ukiendelea kulengwa na mashambulizi ya majeshi ya Urusi.
Baadhi, kama inavyoonyeshwa hapa, walishuka hadi kwenye vituo vya treni za mwendo kasi ambavyo vinatumika kama hifadhi ya muda.

Kiasi cha watu 15,000 wanajihifadhi katika vituo hivyo, meya wa jiji hilo amekadiria.
Baadhi walifanikiwa kulala huku wengine wakijaribu kuwaburudisha watoto wadogo.
Milipuko minne mikubwa ilisikika usiku kucha na kunaswa kwenye video na mashahidi, ingawa haijabainika malengo yalikuwa nini au kama kulikuwa na vifo.
Waandishi wa BBC wamesema milipuko hiyo inaweza kusikika kutoka ghorofa mbili chini ya ardhi katika chumba chao cha kulala.

