Penzi lisiloisha -053
Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.
Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.
Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.
Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.
Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.
Wazazi wa Anna wanamkataa Jafet baada ya kujua maisha yake halisi na kwa juhudi za mama yake, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini.
Anna naye anajikuta akianza kuzoeana na William, Mtanzania mwenzake waliyekuwa wakisoma naye chuoni nchini Marekani na kadiri muda unavyozidi kusonga mbele ndivyo wanavyozidi kuwa karibu na kufanya sana ngono.
Je, nini kitafuatia?
SONGA NAYO…
Japokuwa Anna alimdanganya William lakini mwanaume huyo hakuweza kudanganyika kwani kila alipomwangalia, dalili zote za mtu aliyekuwa mgonjwa au mawazo mengi zilionekana.
Kichwa kilimuuma mno, hakupenda kumuona Anna akiwa katika hali hiyo, hakutaka kuridhika, aliendelea kumlazimisha amwambie ukweli tatizo lilikuwa nini lakini msichanaa huyo alimwambia kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile, na alikuwa kwenye hali ya kawaida kabisa.
William hakutaka kujisumbua kuuliza maswali ambayo majibu yake yalikuwa ni uongo tupu, alichokifanya ni kuachana naye na kufanya mambo mengine. Anna hakubadilika, bado hakujisikia vizuri, muda mwingi alihisi kuwa na uchovu mwingi huku wakati mwingine akihisi kizunguzungu.
“Una mimba,” aliisikia sauti moyoni mwake, hakujua kama ilikuwa sauti yake au ya nani.
Sauti hiyo ikamtia hofu, alijaribu kuikatalia kwamba hakuwa na mimba lakini sauti ile iliendelea kusisitiza kwamba alikuwa na mimba, hivyo akaona ni bora kwenda kupima ili apate uhakika.
Hakutaka kwenda na William, alihakikisha siku aliyopanga kwenda kwenye hospitali iliyokuwa jirani William hakuwa nyumbani. Alitoka kimyakimya na kuelekea huko, alipofika, akaonana na daktari na kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea.
“Tatizo limeanza lini?” aliuliza daktari aliyempokea.
“Limeanza tangu juzi, nimejaribu kuvumilia lakini naona linazidi kila siku,” alijibu Anna huku akimwangalia daktari huyo usoni huku akiwa na hofu za wazi.
“Mbali na uchovu, unahisi kitu gani kingine?”
“Natapika.”
“Sawa! Kitu cha kwanza tutakachokifanya ni kupima mkojo wako, kama hatutobaini chochote basi tutatakiwa kukupima maralia pia,” alisema daktari yule na Anna kukubaliana naye.
Anna akapewa kikopo kidogo na kuelekea chooni. Alionekana kuwa na wasiwasi mwingi, sauti ile ambayo ilimwambia kwamba alikuwa na mimba haikuacha, iliendelea kusisitiza vilevile kwamba alikuwa na mimba hivyo alitakiwa kujiandaa kulea.
Alipofika huko, kabla ya kuchukua mkojo wake akasimama pembeni na kuanza kulia. Moyo wake ukawa kwenye maumivu makali, hakuwa tayari kuyapokea majibu yake kwamba alikuwa mjauzito.
Alikaa huko kwa dakika zaidi ya ishirini na ndipo akakifanya alichokifuata na kutoka kuelekea katika chumba alichokuwa daktari yule na kumpa mkojo wake uliokuwa kwenye kikopo ambapo akatakiwa kutoka ndani na daktari kufanya kazi yake.
“Mungu! Naomba nisionekana na mimba,” alisema Anna huku mashavu yake yakiendelea kulowanishwa na machozi.
Alikaa hapo kwa dakika arobaini na tano na ndipo alipoitwa tena ndani ya chumba kile. Aliposimama na kuelekea huko, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa nguvu, alitamani kuyakimbia majibu hayo, hakutaka kusikia kwamba alikuwa na mimba.
Alipoingia ndani ya chumba kile, daktari akauachia uso wake kwa tabasamu pana lililoonyesha ni kwa jinsi gani aliyafurahia majibu ya Anna, akamtaka kukaa kwenye moja ya viti vilivyokuwa mule ndani.
“Hongera sana,” alisema daktari yule huku tabasamu pana likiendelea kuwepo usoni mwake.
“Hongera ya nini?”
“Nimepima mkojo wako na vipimo vinaonyesha kwamba u mjauzito,” alisema daktari yule.
Badala ya Anna kufurahi kama alivyotaka daktari, akaanza kulia kitu kilichomshangaza hata daktari mwenyewe. Moyo wake uliingia kwenye majuto makubwa, hakuwa amefikiria kama kuna siku angepata mimba kama ilivyokuwa kipindi hicho.
Kichwa chake kikaanza kumfikiria William, mawazo hayakuishia hapo bali akaanza kuwafikiria wazazi wake, hakujua angewaambia nini, hakujua angeuficha wapi uso wake pale baadhi ya watu waliomfahamu kugundua kwamba alikuwa mjauzito, kwa kifupi, alijisikia aibu.
Hakutaka kubaki kliniki hapo, japokuwa daktari alimfariji kwa kumtaka kunyamaza, akasimama na kuondoka zake. Njiani, mawazo yalimjaa, kuna kipindi aliona ingekuwa bora kama angeitoa mimba hiyo lakini kuna kipindi kila alipowafikiria wanawake waliokuwa wakifa katika harakati za kutoa mimba, akajikuta akiachana na wazo hilo.
“Anna mpenzi! Una nini?” aliuliza William, wakati huo walikuwa nyumbani, muda wote Anna alikuwa akitokwa na machozi.
“William…”
“Nipo hapa mpenzi!”
“Ooppss…” akashusha pumzi ndefu.
“Niambie unaumwa nini! Niambie tu mpenzi, nipo kwa ajili yako, nipo tayari kukulinda kwa kitu chochote kile, jaribu kushea matatizo yako pamoja nami, unapokuwa na mawazo hivyo unaniweka kwenye wakati mgumu mpenzi! Niambie, mpenzi wako nipo hapa, una nini?” alisema William kwa sauti ya kubembeleza huku akiwa amemsogelea kabisa Anna.
“Nina….” alisema Anna, akanyamaza.
“Una nini?”
“Nina mimba…” alisema Anna na kuanza kulia tena.
“Unasemaje?” aliuliza William huku akionekana kuja juu.
“Nina mimba mpenzi! Nina mimba yako,” alisema Anna.
William akabadilika, akakunja sura, akawa kama mtu aliyepandwa ghadhabu, hata macho yake, yakabadilika, hakuamini kile alichokisikia kutoka kwa Anna, akauliza tena, jibu likawa lilelile kwamba msichana huyo alikuwa na mimba.
Je nini kitaendelea? Fuatilia katika Gazeti la Risasi Mchangan yiko siku ya Jumatano

