×

Chongo!-14

Ilipoishia wiki iliyopita
Wakambeba na kumkimbiza katika gari la polisi lililokuwa linasubiri majeruhi. Mara moja dereva akapiga moto na safari ya hospitalini ikaanza.
Sasa endelea…

Gari lilikwenda kasi sana na dakika kumi baadaye, walikuwa wakiingia katika viwanja vya hospitali ya IMTU ambako walisimamisha gari mapokezi. Mhudumu aliyekuwepo alitoka haraka na kulisogelea lile gari la polisi.

“Kuna majeruhi mwingine tumemleta,” alisema dereva akimwambia mhudumu huyo, ambaye naye aligeuza shingo kama vile anawaonesha kitu kwa ishara, nao walipogeuka, wakawaona manesi wanne wakiendesha machela kulielekea gari la hospitali hiyo linalotumika kuwabeba wagonjwa.

“Wale wagonjwa mliowaleta kwanza wanaondolewa kupelekwa Muhimbili, hali zao ni mbaya,” alisema mhudumu huyo, akiwazungumzia Noel na mzee Masta ambao ndiyo waliokuwa wakipakiwa kwenye gari hilo. Askari dereva aliwatazama kwa huruma halafu akamgeukia mhudumu na kumtaka kuleta machela haraka ili amchukue majeruhi.

\Machela ikaletwa haraka, Bata akapakizwa na kukimbizwa chumba cha upasuaji. Haraka akachukuliwa vipimo, kifua, kichwa, mbavu, miguu na kila sehemu. Akiwa bado amepoteza fahamu, madaktari wakagundua kuwa kijana huyo hakuwa amevunjika wala kuumia sehemu yoyote, zaidi ya mshtuko uliosababisha kupoteza fahamu.

Akaondolewa na kupelekwa wodini ili apumzike hadi hapo atakapoamka. Saa sita za usiku ndipo Bata aliposhtuka kutoka katika usingizi mzito, kichwa chake kilikuwa kizito sana. Akashangazwa na harufu ya madawa iliyokuwa wodini humo, akakizungusha kichwa chake kuangalia.

Akabaini alikuwa hospitalini amelazwa. Akajikagua mwili mzima lakini hakuona chochote kilichosababisha alazwe, hata hivyo hakupata mtu ambaye angeweza kumweleza chochote, akaamua kulala hadi kesho yake atakapozungumza na madaktari.

Asubuhi daktari wa zamu akamweleza kwa kirefu kilichotokea na kumfahamisha kuwa wenzake wawili aliokuwa nao ndani ya gari, walikuwa wamehamishiwa katika hospitali ya Muhimbili, kwani hali zao zilikuwa mbaya.

Bata alisikitishwa sana na suala hilo, akalazimika kumweleza ukweli daktari huyo kuwa wawili hao walikuwa ndiyo walezi wake na haelewi maisha yake yatakuwa vipi. Dokta alimhurumia, akamshauri aende Muhimbili hospitalini akawaone ili ajue sehemu ya kuanzia. Akatoa noti ya shilingi elfu kumi na kumpatia.

Bata alitoka hospitalini akiwa mzima kabisa, akaenda kituo cha daladala na kupanda basi la kuelekea Kariakoo na alifika Muhimbili kama saa nne hivi asubuhi. Kwa kuwa yule daktari alikuwa amempa karatasi lenye maelezo ya jinsi ya kuwapata wagonjwa wake, alikwenda hadi mapokezi na kuwapatia kile kikaratasi.

Mhudumu wa pale alimtazama, halafu akamwelekeza Moi na bila kusita, Bata akafuata maelekezo hadi alipofika kwenye jengo hilo, akamfuata nesi aliyekuwa amekaa kwenye dawati, akiwa na makaratasi mengi mbele yake. Akamsalimia na kumweleza shida yake.

Nesi akamwelekeza kwa mtu mwingine ambaye alipomfikia, naye alimweleza shida yake. Mtu huyo akamwelekeza katika wodi ambayo wagonjwa wake hao walikuwemo. Bata akaifuata wodi hiyo huku mwili wake ukiwa unatetemeka kwa hofu, hakujua angewakuta wakiwa katika hali gani.

Tofauti na alivyotegemea, wodi ile ilikuwa kubwa, yenye wagonjwa kila upande, tena wawiliwawili. Alisimama mlangoni kwa muda akiangalia kama angeweza kuwaona kwa mbali, lakini hakuwaona.

Akalazimika kusogea ili atazame vizuri, ukizingatia alikuwa na jicho moja. Akaangalia upande mmoja akikagua kitanda baada ya kitanda. Baada ya vitanda kadhaa, akagundua kuwa wodi ile ilikuwa ni maalum kwa ajili ya watu waliopata ajali, maana alikutana na watu wamekatika mikono,miguu, wameungua moto na ajali zingine mbalimbali.

Hili lilimtisha sana, lakini hakuwa na budi, alijikaza ili aweze kuwaona Noel na mzee Masta, watu ambao aliamini waliletwa duniani kwa ajili ya kumsaidia. Hadi anamaliza upande mmoja wa wodi hiyo hakuwa amewaona.

Akarejea tena kuangalia upande wa pili, kwa umakini zaidi, lakini tena hadi alipomaliza bado hakuweza kuwaona. Wagonjwa wote walikuwa wamekaa kwenye vitanda vyao kwa kuwa ulikuwa ni muda wa kusalimiana na ndugu zao, hivyo suala la huenda wengine walikuwa wamelala halikuwepo.

Mapigo ya moyo ya Bata yakaanza kudunda kwa kasi, hofu ikamuingia. Wamekwenda wapi? Alijiuliza kwa muda mrefu bila kupata majibu, lakini baadaye sana, akapata wazo la kwenda kuuliza kwa yule nesi aliyemwelekeza.

Alipomfikia akamweleza kuwa wagonjwa wake hajawaona. Nesi wala hakushtuka.
“Si wale walioletwa asubuhi hii wakiwa wametoka IMTU?” nesi alimuuliza kijana huyo, ambaye alionekana kuchanganyikiwa. Bata akajibu kwa kutingisha kichwa.

Nesi huyo akashika kidude kinachoendesha kompyuta iliyokuwa mbele yake, akabonyeza bonyeza vitufe kadhaa na akaelekeza macho yake kwa umakini kusoma kilichoandikwa ndani.

Leave a Comment