Maumivu makali ya tumbo (Acute Abdomen)-2
Wiki hii tunaendelea kuangalia magonjwa makali yanayosababisha maumivu makali ya tumbo;
APPENDICITIS
Huu ni ugonjwa wa kidole tumbo unaoshambulia sehemu iitwayo ‘Vermiform Appendix’. Tatizo hili huambatana na maumivu ya tumbo yanayoanza taratibu upande wa kulia usawa wa kitovu na kushuka chini upande huohuo. Maumivu makali hutokana na kidole tumbo hicho kupasuka.
Ni tatizo linaloweza kumpata mtu yeyote katika hali yoyote kutokana na kidole tumbo hicho kujaa uchafu na kushindwa kutoka hivyo kuziba na bakteria huanza kuzaliana.
Vipimo mbalimbali husaidia uchunguzi lakini kikubwa zaidi ni kipimo cha CT-Scan. Vipimo kama Ultrasound huenda visioneshe moja kwa moja. Vipimo vingine ni vya damu na upimaji wa daktari mwenyewe.
Matibabu yake ni upasuaji, ucheleweshaji unaweza kusababisha kidole tumbo kupasuka na hali ikawa mbaya hadi kupoteza maisha.
ABDOMINAL WALL HERNIAS
Hii ni ngiri ya tumbo ambapo sehemu mojawapo ya misuli ya tumbo inaachia nafasi na kusababisha matumbo kujiingiza hapo na kubanwa. Ngiri nyingi huwa hazina dalili hadi matumbo yabanwe ndipo mgonjwa anapohisi maumivu ya tumbo ambapo hayaishi.
Maumivu yanaweza kuwa kidogokidogo na hata ukitumia dawa unapata nafuu ya muda lakini wakati mwingine yanaweza kuchachamaa na kuwa makali sana na tiba yake ni upasuaji. Uchunguzi wa henia au ngiri ni rahisi kwani inaonekana.
ILEUS
Hii ni hali ya matumbo kusimama na kutofanya kazi, kwa kawaida muda wote matumbo huzungukazunguka, hii ni kwa binadamu wote, matumbo yanaposimama tunasema yamepooza hivyo mgonjwa hulalamika maumivu makali ya tumbo, kichefuchefu na kutapika na tumbo kujaa.
Chanzo kikuu ni kutoboka kwa utumbo, ugonjwa wa kidole tumbo, ugonjwa wa utumbo mkubwa, ajali za tumbo na kuharisha sana hasa kwa watoto wadogo.
Uchunguzi wake upo wazi kwa kusikiliza mingurumo ya tumbo ambayo haipo, tumbo linajaa. Mgonjwa atapata tiba ya kumsaidia arudi katika hali ya kawaida kama kumwekea mipira ya tumboni kupitia puani na tiba nyingine ambazo daktari ataona zinafaa.
INTESTINAL OBSTRUCTIONS
Hii ni hali ya kuziba kwa utumbo na kuzuia chakula kisipite kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Mgonjwa mwenye tatizo hili hupata maumivu makali ya tumbo yanayobana, kutapika, kufunga choo na wala hatoi hewa. Utumbo unaweza kuziba wote au kidogo. Chanzo cha kuziba utumbo kinaweza kuwa makovu ya upasuaji wa tumbo uliopita, uvimbe tumboni, henia au ngiri na matatizo mengine ya tumbo. Uchunguzi hufanyika katika hospitali ya mkoa ambapo vipimo mbalimbali vitafanyika.
MAUMIVU KATIKA VIUNGO VYA UZAZI
Mwanamke pia anaweza kupata maumivu makali ya tumbo upande wa chini na yanapokuwa makali jambo la kwanza linalochunguzwa ni uwepo wa mimba nje ya kizazi ingawa yapo maumivu mengine kama maambukizi ya kizazi na mirija na uvimbe.
USHAURI
Wahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.

