×

Yanga yamnasa kiungo rasta, anakaba hadi kivuli

Musa Mateja na Willbert Molandi

MOTO umeanza Yanga kwani tayari imenasa jembe moja hatari kutoka AFC Leopards ya Kenya, huyo si mwingine bali ni kiungo Allan Kateregga ambaye kichwani amefuga rasta, jamaa anajua.

Kwa miaka mitano sasa tangu kuondoka kwa Athuman Idd ‘Chuji’ na hata Frank Domayo, Yanga imekuwa na tatizo la kiungo mkabaji lakini sasa inaamini Kateregga atakuwa mtu sahihi kwao.

Kateregga aliichezea Leopards dhidi ya Yanga, juzi Alhamisi katika nusu fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuiwezesha timu yake kushinda kwa penalti 4-2 yeye akipiga penalti ya tatu.

Mmoja wa mabosi wa Yanga anayeshughulikia usajili moja kwa moja kwa kuzungumza na mchezaji wakiogopa ‘kupigwa’ na wajanja, alisema wamezungumza na Kateregga ambaye anamaliza mkataba na Leopards mwisho wa mwezi huu.

“Katika ripoti yake, kocha wetu Lwandamina (George) alipendekeza asajiliwe kiungo mkabaji mwenye uwezo wa hali ya juu na kura imemuangukia Kateregga.

“Watu wengi wamekuwa wakiongea maneno mengi juu ya usajili wetu, sisi hatuna haraka sana zaidi tunajitahidi kufanyia kazi kwa makini mapendekezo ya kocha na benchi la ufundi.

“Kwa asilimia 100, nikwambie tu kwamba takribani wachezaji wote ambao wamehitajika na kocha wetu, hadi sasa tuna uhakika wa kuwasajili na hatufanyi kitu bila matakwa ya kocha.

“Yule rasta kiungo wa Leopards ametuvutia na tumeanza kuzungumza naye na mambo yanaenda vizuri, anamaliza mkataba mwisho wa mwezi huu hivyo tunaweza kumpata kama mchezaji huru,” alisema bosi huyo.

Yanga ina wachezaji wa kigeni saba ambao ni Haruna Niyonzima wa Rwanza, Amissi Tambwe (Burundi), Vincent Bossou (Togo), Justin Zullu na Obrey Chirwa (wote Zambia) na Thabani Kamusoko na Donald Ngoma wote wa Zimbabwe.

Ni Zullu na Chirwa ndiyo wenye mkataba na Yanga kwani wengine wote mikataba yao inaisha mwishoni mwa mwezi huu, hivyo Yanga ili imsajili Kateregga inapaswa kuachana na mmoja wa wageni hao.

Leave a Comment