“Ni huyo jini niliyewaambia, huyu mwenzenu anamfahamu. Anaua watu wote wanaofika hapa.”
“Umesema anakuja, yuko wapi sasa?” Mwenye bunduki aliendelea kuuliza huku akitazama kila upande. Bunduki yake alishaiweka sawa mikononi.
“Anatokea kwenye ile chupa inayojaa moshi. Hiyo milio mnayoisikia ni yake. Punde tu mtamuona. Mimi nakimbia,” nikawaambia.
“Unakimbia nini, acha aje hapa tumuone. Tuko wanaume watatu na tuna bunduki, tunaogopa nini?”
“Tulikuwa wanaume sita na wenzangu wote wameuawa, itakuwa sisi watatu?” nikajiambia kimoyomoyo.
SASA ENDELEA…
Ule moshi ukaanza kutoka ndani ya ile chupa na kusambaa mle chumbani. Yule mtu aliyekuwa na bunduki aliyeniambia “Tuko wanaume watatu na tuna bunduki, tunaogopa nini?” alianza kupiga hatua ili akimbie.
Lakini alipiga hatua moja tu akadakwa pale pale na Kaikush aliyeibuka ghafla kutoka katika ule moshi.
Kaikush aliikamata ile bunduki akaitupa chini. Faiza aliinama akaiokota na kumpa yule mwenzake. Yule mtu alikimbia nayo hadi katika eneo la mlango ambapo nilikuwa nimesimama. Akamgeukia Kaikush na kumuelekezea mtutu wa bunduki.
Alikuwa na moyo wa ujasiri kweli kweli. Alifyatua risasi akampiga Kaikush aliyekuwa amemng’ang’ania yule mwenzake akimfyonza damu.
Risasi ilimpata lakini haikumtoboa Kaikush aliyeonekana kutokuwa na habari yoyote kuwa alipigwa risasi.
Yule mtu aliyepiga risasi alipoona hivyo aliuvuta ule waya ambao walikuwa wamejifunga kwenye viuno kama mikanda. Aliuvuta ule uliokwenda kwa mwenzake. Aliuvuta kwa nguvu mpaka akauchomoa.
Baada ya hapo akaniambia.
“Tukimbie.”
Nikamshika mkono Faiza tukatoka katika sehemu ile na kumuacha mwenzetu akiuawa.
Tukaanza kukimbia kufuata ulipopita ule waya. Wakati nakimbia nilikuwa nimemshika mkono Faiza ambaye alikuwa nyuma yangu hatua moja. Mwenzetu aliyekuwa na bunduki ndiye aliyekuwa mbele.
Tulifika mahali tukasimama. Yule mwenzetu alipiga simu na kuwasiliana na aliyekuwa akiwasiliana naye. Alimueleza yale yaliyokuwa yamejiri ndani ya pango lile.
Wakati simu iko hewani tukaanza tena kukimbia kwa kuhofia kuwa Kaikush angeweza kutufuata.
“Kama mnaweza kuja, tunaomba mtufuate, hali si shwari,” mtu huyo alisema huku akikimbia.
“Nimechoka,” Faiza alisema baada kukimbia kwa umbali mrefu.
Akaongeza; “Siwezi tena kukimbia, niacheni.”
“Hatuwezi kukuacha hapa, jitahidi kidogo,” nikamwambia.
“Siwezi,” Faiza akasema huku akitweta.
Tukasimama. Msichana huyo akachutama na kuendelea kuhema kwa nguvu.
“Lile jini kama litatufuata linaweza kutukuta hapa na kutudhuru sote,” aliyeshika bunduki alisema.
“Huyu msichana hawezi tena,” nikamwambia.
“Mimi niacheni tu hapa hapa, siwezi tena kukimbia. Nitakufa,” Faiza akatuambia.
“Tukuache hapa? Lile jini likija je?” aliyekuwa na bunduki alimuuliza.
“Potelea mbali, kama litaniua na liniue lakini siwezi kuendelea kwenda mbele.”
Hapo hapo nikainama na kumuweka Faiza kwenye bega langu kisha nikainuka naye.
“Twende,” nikamwambia yule mtu aliyekuwa na bunduki.
“Utaweza kukimbia ukiwa naye?” akaniuliza.
“Nitaweza,” nikamjibu.
Tukaanza tena kukimbia. Amini usiamini niliweza kukimbia nikiwa na Faiza begani kwangu. Ile miguu iliyokuwa ikiniuma sikuisikia tena kuuma.
Sikujua ilikuwa ni kwa sababu ya nini lakini huenda ilitokana na taharuki tulilokuwa nalo ambalo liliifanya akili yangu izingatie zaidi jinsi ambavyo tutaweza kujiokoa.
Baada ya mwendo mwingine mrefu nilisimama. Sasa nilikuwa nimechoka. Mwenzangu naye akasimama.
“Nimechoka,” nikamwambia.
Mtu huyo alipiga tena simu akauliza.
“Mnakuja?”
“Tuko njiani,” sauti ikamjibu.
“Mko wangapi?”
“Tuko watu sita..polisi wawili, askari wa jeshi la zima moto na uokoaji wako watatu pamoja na mimi.”
“Fuateni waya ulikopita. Tutakutana njiani.”
“Lakini mko salama?”
“Mpaka sasa hivi hatuwezi kusema tuko salama kwa sababu mwenzetu mmoja atakuwa ameshauawa na sisi hatuna uhakika wa usalama wetu hadi sasa.”
“Huyo msichana bado mko naye?”
“Tunakuja naye.”
“Hebu mpe simu tumsikie.”
Faiza akapewa simu.
“Hallo! Akasema akiwa ameiweka simu kwenye sikio.
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Faiza.”
“Ni kweli kwamba ulikuwa unaishi humu ndani ya pango?”
“Ni kweli”
“Umeishi kwa muda gani?”
“Miaka minne”
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.