×

Mwanamke Alivyomfanya Zezeta Kaka Yangu- -35

“Tangu lini mtu akakaa kwenye banda la mbwa?” Yule mwanamke akadakia huku mwili wake ukitetemeka.

“Lakini mama kwa nini unajitetea? Huyu ndiye mlalamikaji.” Kamanda Matwanga akawa kama anataka kugeuka, asiende kwenye banda.

Je, kaka yao atakuwa wapi? Fuatilia…

“Kamanda tafadhali sana twende kwenye lile banda kwa kuwa ile sehemu ndiyo ambayo nimeambiwa huwa huyu mwanamke anapofichia watu.” Nilisema kwa ujasiri mkubwa kwa kuwa nilishuhudia akipeleka chakula siku nilipolala katika nyumba hii nilipofika kumtembelea kaka wakati anaugua.

Mama yule aliniangalia kwa jicho lenye hisira. Mwili wake ukimchunguza alikuwa anatetemeka dhahiri. Naamini hata Inspekta Ben Mtwanga aliligundua hilo na mara moja akaamuru:

“Haya askari twendeni kwenye banda la mbwa.”

Wote waliondoka huku yule mwanamke alionesha woga, mimi nilijipa moyo kwamba kule ni lazima tutamkuta kaka yangu Edgar Ugonile.

Lile banda la mbwa lilijengwa kwa umahiri mkubwa kwa sababu kulikuwa kumetenganishwa kati ya chumba cha mbwa na chumba kingine ambacho mpaka wakati huo hatukujua kina nini.

Banda lilikuwa kubwa na kwa familia za kimaskini ungeweza kuiita nyumba kwa sababu mtu mzima aliweza kuingia na kusimama na hata kitanda kimoja kingeweza kukaa kama kingeingizwa.

Kwa kweli katika chumba cha mbwa kulikuwa na mbwa mkubwa ambaye wakati huo alikuwa akibweka sana baada ya kuona watu wakilizunguka banda lake.

“Hiki kibanda inaonesha kuna chumba kingine. Mlango wa kuingilia chumba hicho upo wapi?” aliuliza Kamanda Mtwanga.

Kimyaa.

“Mama nakuuliza wewe, au kuna mtu mwingine anayejua mazingira ya hapa? Mlango wa kuingilia upo wapi?” Akarudia kuuliza.

Kwa kuwa nilikuwa na kiherehere na kwa kuwa niliwahi kumuona akiingia katika chumba hicho, niliingilia kati huku moyo ukienda mbio.

“Afande chumba hicho mlango wake uko nyuma,” nikajikuta naropoka.

Ile kusema hivyo kundi lile la watu likazunguka banda na kukuta kweli kuna mlango, tena wa mbao.

“Mama ufunguo wa chumba upo wapi?”

“Sina umepotea… sijui upo wapi… lakini chumba hicho kina pumba tu za mahindi.”

Jibu hilo lilitaka kumtibua Kamanda Mtwanga, akaandika kwenye kijitabu chake, kisha akamuangalia kwa macho makali mwanamke yule.

“Kwani vyumba vyote nilivyotembelea na kukagua nilikuuliza kilichopo ndani? Wewe mwanamke usitubabaishe,fungua hiki chumba.”

“Jamani humo hakuna ki….”

Kabla hajamaliza alichotaka kusema Kamanda Mtwanga akaamuru mlango ufunguliwe kwa kuvunjwa!

“Askari, vunja mlango.”

Askari wawili wakakunja miguu yao na kuikunjua kwa pamoja ‘bha, wakapiga teke kwa pamoja ule mlango, ukafunguka.

Kwa kuwa chumba kilikuwa kidogo, waliingia askari wawili ndani na yule mganga wetu ambaye alikuwa akimwaga unga fulani mweupe na tukasikia sauti ya mtu akilia.

“Kuna mtu?” akauliza kamanda wao.

“Siyo mtu, watu,” akajibu mmoja wa askari waliokuwa ndani ya chumba kile.

“Watu?” akauliza tena kamanda,

“Ndiyo afande.”

“Wako wangapi?”

“Wawili afande.”

“Watoe nje!”

“Wameng’ang’ania chuma afande, lakini tutawatoa tu.”

“Hawajang’ang’ania, hii ni dawa imewafanya wafanye hivyo,” alisikika mganga akiwaambia askari wale.

“Wewe unaitwa nani?” nilisikia sauti ya yule mganga, bila shaka alikuwa akimuuliza mtu aliyekuwa humo ndani ya lile banda. Hata hivyo, hakujibu lolote maana sikusikia sauti, labda kama aliongea kwa sauti ya chini sana. Nilikuwa na hamu na mimi niingie nikawaone watu hao lakini askari mmoja alinizuia.

Miongoni mwa askari tuliokuwa nao pale, mmoja alikuwa wa kike, mara baada ya kuthibitishiwa kuwa ndani ya banda kuna mtu, alimkamata yule mwanamke na kumwambia asimame mbele yake na kwamba alikuwa chini ya ulinzi.

“Wewe mwanamke, kwa kuwa humu ndani ya banda kuna watu, kuanzia sasa uko chini ya ulinzi, njoo usimame mbele yangu.”

“Jamani nisameheni,” akajitetea huku akitokwa na jasho.

Ilichukua sekunde kama kumi hivi, askari wale wawili wakiwa na yule mganga wetu kutoka ndani ya banda na mtu mmoja aliyekuwa na nywele ndefu, kucha ndefu na mwili mchafu, alikuwa amekonda sana na hata nguvu za kutembea alikuwa hana ndiyo maana walipokuwa wanamtoa walimbeba msobemsobe.

Mtu huyu alikuwa mzee kuliko kaka yangu, alikuwa amevaa suruali nyeusi na shati jeusi, nilimuangalia mkononi nikaona amefungwa hirizi kila mkono na kwenye enka, miguuni. Alikuwa anatisha, lakini alisikitisha pia.

“Huyu ndiye ndugu yenu?” aliuliza yule mganga tuliyekwenda naye pale.

“Huyu siyo kaka yangu… siyo huyu,” nilijikuta nikijibu, nikamfuata yule mwanamke, hata hivyo nikaisikia sauti ya kuamrishwa kutoka nyuma yangu.

“Tulia wewe,” kamanda alinifokea, nami nikanyamaza kusubiri huyo mtu wa pili kutolewa huku nikiwa na hasira na mara kwa mara nilikuwa nikimuangalia yule mwanamke mtesaji.

Hata hivyo, licha ya kuwa na hasira nilikuwa nikisali kimoyomoyo kwa ajili ya mambo mawili, moja ili hasira zangu zisivuke mpaka, nikampiga na kumuua yule mwanamke aliyemtesa kaka yangu pili kwamba huyo mtu ajaye awe kaka kwani wale askari baada ya kumbwaga yule wa kwanza na kumtupa nje ya banda karibu na tulipokuwa sisi, waliingia tena ndani kwenda kumtoa huyo wa pili.

Moyo wangu ulikuwa ukienda mbio kwani nilikuwa na wasiwasi kwamba huenda atakuwa kamhamishia sehemu nyingine au inawezekana alifariki dunia kweli kama alivyodai na huyo aliyekuwa ndani alikuwa mtu mwingine.

Hata hivyo, shaka yangu kwamba anaweza kunishtaki kwa kumkashifu niliiondoa kwa sababu tayari watu wawili walionekana kwake wakiwa wamefichwa kibandani.

Yule mganga wetu alisikika akimuuliza yule mtu aliyekuwa amebaki ndani jina lake lakini akawa hasikiki akijibu lolote. Alitoka na kwenda kuchukua kitu fulani kwenye mkoba wake wa dawa. Sikujua alichukua nini lakini nilihisi kuwa ni aina fulani ya unga.

Usikose kusoma muendelezo wa simulizi hii wiki ijayo.

Leave a Comment