The House of Social Media
gunners X

Kubali umasikini, anzia hapo kuelekea kwenye utajiri!

0

Hakuna anayeweza kupinga ukweli kwamba, maisha ya sasa ni magumu, ugumu ambao kama mtu atabweteka na kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo, upo uwezekano mkubwa wa kujikuta anaingia katika maisha yasiyokuwa na mbele wala nyuma na ugumu huo wa maisha kuwa mara mbili yake.

Lakini licha ya ukweli huo, bado nafasi zipo wazi kwa watu kuingia katika ulimwengu wa mafanikio. Hii itatokea tu kama mtu ataamua kupambana ipasavyo na kuhakikisha haingii katika kapu la umaskini ambalo limejaa wengi hata wasiostahili kuwemo.

Wapo watu na afya zao, nguvu za kutosha pamoja na maarifa waliyopewa na Mungu lakini bado wameridhika kuishi maisha ya kifukara huku wakitegemea misaada kutoka kwa watu wengine ili kuweza kusogeza siku.

Hakika hii ni hatari sana na uhatari huo unakuja pale unapomuona mtu ambaye ana kila sababu ya kuwa miongoni mwa watu wenye mafanikio lakini yeye anaona hawezi kuwa hivyo huku akiwa na dhana kwamba, yeye ni miongoni mwa wale waliopangiwa kuishi maisha ya kimasikini.

Wapo wanaoamini kwamba, Mungu kaleta ulimwenguni watu wa sampuli mbili. Yaani kuna maskini ambao hata wafanye nini hawawezi kuwa matajiri na kuna matajiri ambao wao wamepangiwa neema ‘mwanzo mwisho’.

Watu wenye dhana hiyo potofu wapo huko mtaani, yaani wao wanaamini wameumbwa na umaskini na hawawezi kufanya chochote kitachoweza kuwabadilisha kuwa miongoni mwa matajiri. Wenye mawazo hayo ndio wale tunaowaona huko mtaani wakiishi maisha ya kimasikini kupitiliza.

Mtu kama ni kilema asiye na mikono wala miguu, anaweza kuwa sahihi akisema hana kitu anachoweza kukifanya akawa tajiri kutokana udhaifu aliokuwa nao lakini wewe ambaye umejaaliwa kuwa miongoni mwa waliojaaliwa kuwa na viungo kamili, nguvu pamoja na maarifa iweje uone uko sawa kuishi maisha duni?

Ifike wakati ukae chini na ujiulize sababu za wewe kuendelea kuishi maisha mabaya wakati wenzako kila siku wanapiga hatua mbele.

Huenda kuna sehemu unakosea hivyo ni vyema ukaibaini na kufanya mabadiliko ya haraka ili na uweze kuwa miongoni mwa wale waliotumia vizuri nafasi zao za kuletwa hapa ulimwenguni.

Kama unataka kutimiza wajibu wako wa kuletwa hapa ulimwenguni una kila sababu ya kufanya kazi kwa bidii bila kuridhika na hicho kidogo unachokipata sasa. Siku zote ota kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa duniani bila kujali kwa sasa uko katika nafasi gani.

Nasema hivyo kwa sababu, kuna wanaodhani kwamba kwa kuwa sasa hivi ni masikini watakuwa wamechelewa na uwezekano wa wao kuwa matajiri haupo tena. Lahasha!

Siku zote mbio za kuelekea kwenye utajiri huanzia kwenye mstari wa umaskini. Unachotakiwa ni kuukubali umasikini ulionao kisha kuanzia hapo uanze kupambana kuelekea kwenye utajiri.

Yaweza kuwa kama ndoto ya mchana kwa mtu fukara kuamini kwamba akiamua ipo siku anaweza kuuaga umaskini lakini niamini mimi, inawezekana!

Na hii inatokana na ukweli kwamba, matajiri wengi wakubwa unaowajua wengi wao walianzia kwenye mstari wa umasikini, wakauchukia na wakaamini kuwa wakipambana wanaweza na leo hii wapo kwenye ulimwengu wa watu matajiri.

Wewe unasubiri nini? Ni wakati wako sasa wa kubadilika. Kikubwa cha kuwa nacho ni hasira ya kufanikiwa. Yaani uwe na shauku kubwa ya kuwa kama hao wenye mafanikio makubwa.

Unapowaona, kuwasikia ama hata kusoma habari zao kuwa na wivu, wivu ambao mwisho wa siku utakufanya nawe kuwa kama wao.

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS

GLOBALBREAKINGNEWS100.jpg

Leave A Reply