×

Nelly Muosha Magari wa Posta-17

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Nelly alipompagawisha vya kutosha Atu ambaye kutokana na vionjo vitamu vya kijana huyo alimuomba kama hatajali awe mtu wake wa kudumu. Je, baada ya Nelly kuambiwa hivyo alisemaje? Ungana nami katika uhondo huu usioisha hamu…

“Jamaaa yangu kwa sasa hayupo nchini kaenda kusoma Marekani, sina mtu ndiyo maana nakuomba kama hutajali uchukue nafasi yake,” Atu alimwambia Nelly.
Nelly alifurahi sana kupata habari hiyo njema alimkubalia Atu na kumwambia aonde shaka watakuwa pamoja lakini moyoni alijiuliza itakuwaje dada huyo aliyeelewa Nelly alikuwa mambo safi atakapobaini kumbe alikuwa kibarua aliyekuwa akimsaidia fundi ujenzi kubeba zege.

“Hili si litakuwa soo hili?” Nelly alijisemea moyoni.
Hata hivyo, alipanga kutumia ujanja wa hali ya juu ili Atu asigundue kama hakuwa na kazi na baada ya maongezi ya kusifiana walivyopeana raha yalipoisha walikwenda kuoga.

Baada ya kumalizika kwa zoezi hilo, walitoka mle gesti wakiwa wepesi ambapo Atu alitangulia nje na kumuacha Nelly akimalizana na mhudumu wa ile gesti.
Wawili hao waliondoka pale gesti kila mmoja akiwa amefurahia walichokuwa wamekifanya bila kujali kama walikuwa na maradhi kwa sababu hawakutumia kinga jambo ambalo lilikuwa hatari.

Nelly alikuwa akielekea Tandika, walipofika kituo cha daladala, kijana huyo kabla ya kuagana na Atu aliyekuwa akielekea karibu alitaka kumpatia shilingi elfu tano lakini msichana huyo alikataa.

Hata hivyo, kabla ya Nelly kupanda gari walipanga kukutana tena siku ya Ijumaa jioni kisha kijana huyo akapanda kwenye daladala la Tandika akiwa mwenye furaha kufuatia kujiburudisha na Atu baada ya kumkosakosa Doreen.

Alipofika Tandika breki ya kwanza ilikuwa nyumbani kwa fundi Yassin kwa nia ya kumpa mchapo wa kilichojiri akiwa na Atu na kumshukuru kwa sapoti ya hela alizomtumia.

Bahati nzuri alipofika kwa fundi huyo alimkuta akiwa amesimama kibarazani, Nelly aliyekuwa na furaha alimshukuru fundi wake kwa kampani nzuri aliyompa na kumweleza kila kitu kilichojiri na Atu.

“Mi nilijua tu yule mtoto asingechomoa maana wewe ni mtaalam wa vimwana wakali,” fundi Yassin alimwambia Nelly wakaishia kucheka.

“Kaka siyo siri, mtoto nimemkubali na yeye kanikubali vilevile yaani kanifagilia kinona kwamba hakuwahi kukutana na mtu kama mimi, hata hivyo kwa mambo niliyomfanyia ana haki ya kutoa ufagio,” Nelly alimwambia fundi Yassin, wakacheka.

Fundi Yassin alipogundua mkewe angesikia maongezi yao ya kipuuzi alimwambia Nelly kwamba siku iliyofuata wataongea kwa kirefu ili ampe mchapo wote ndipo kijana huyo ambaye alikuwa kalewa kwa mbali alimuaga lakini akakumbuka harufu ya pombe ingemuumbua kwa wazazi wake.

Baada ya kubaini hivyo, alikwenda kwenye genge la kijana mmoja wa Kimakonde aliyezoeleka kuitwa Chinga aliyekuwa akichelewa kufunga biashara yake akamwambia ammenyee tango.

Kwa kuwa Chinga huyo alikuwa akifahamu kwamba tango linakata kilevi pamoja na harufu akamtania kwamba alikuwa akiogopa so kwa washua wake nini, Nelly akacheka na kumwuliza alijuaje!

“Jamani niuze matango nisijue pia kama yanakata kilevi?” Chinga alimwambia Nelly, wakacheka.

“Tena kula na ndizi hii mbivu hakuna atakayekushtukia kabisa,” Chinga alimwambia Nelly na kumpa ofa ya ndizi moja mbivu.
“Na ndizi zinakata kilevi?” Nelly alimwuliza.

“Tena fasta,” Chinga alijibu kisha kumkabidhi Nelly tango alilokuwa amelimenya na kumwambia akipenda anaweza kula huku akitoweza kwenye chumvi.
Wawili hao waliendelea kupiga stori za hapa na pale na Nelly alipomaliza kula tango alimlipa Chinga shilingi mia mbili kisha akamuaga na kwenda kwao, ambapo aliwakuta wazazi wake wakiangalia runinga.

Baada ya salamu, baba yake alimuuliza habari za kazi aliyokwenda kuifanya akawaambia ilikuwa nzuri na kuwaelezea jinsi watu walivyokuwa wakijenga majumba ya kifahari pande za Madale.

“Kwa hiyo mwanangu na wewe leo umefanya kazi anazofanya baba Hadija?” mama yake Nelly alimwuliza kijana wake.

“Tena hapa nilipo hadi mgongo unaniuma kwa ajili ya kuchota mchanga, yaani tulipofika walinipangia kazi ya kuhamisha mchanga kwa kuuzoa na chepe,” Nelly aliwaambia wazazi wake ambao walicheka kwani hawakutegemea kama kijana wao sharobaro angeweza kufanya kazi hiyo.
“Lakini umeifurahia hiyo kazi?” baba yake Nelly mzee Reli ya Uhuru alimwuliza kijana wake.

“Sana tu, kwani nimeweza kufika eneo ambalo sikuwahi kufika, nimefahamina na vijana wawili mmoja anaitwa Zakayo na mwenzake anaitwa Haruni wanaomsaidia baba Hadija kazi, hata kesho nitaenda,” Nelly aliwaambia wazazi wake.

Baada ya kuzungumza na wazazi wake ambao hawakugundua kama kijana wao alikuwa ametoka kufanya mambo yasiyofaa na Atu na alikuwa amekunywa pombe, Nelly alikwenda chumbani kwake.

“Mama Nelly umemsikia mwanao mpenda usmati alivyosema kafanya kazi ya kuhamisha mchanga kwa chepe, kweli hiyo ni habari njema na huko ndiko kujifunza maisha,” baba Nelly alimwambia mkewe.

“Nami kaniacha hoi, nahisi leo alipewa kazi nyepesi, tusubiri siku atakayotuambia kabeba zege akituambia ataendelea hapo nitaamini kweli kaamua kujishughulisha,” mama Nelly alimwambia mumewe.

Kule chumbani Nelly aliendelea kumuwaza Atu hasa alivyokuwa akiyazungusha macho yake mazuri na alivyokuwa akihema, akajikuta akisema peke yake kwamba watakapokutana Ijumaa waliyokubaliana atampa mambo matamu zaidi.

Hata hivyo, kutokana na ulevi aliokuwanao kichwani hakuchukua muda mrefu alipitiwa na usingizi hata mama yake alipokwenda kumuamsha ili akale hakumsikia.

“Baba Nelly, kweli mwanao leo kachoka, nimemwita mpaka nikapata wasiwasi, nilipoingia kumwangalia yaani kalala fofofo,” mama huyo alimwambia mumewe.
“Ndivyo inavyotokea kwa mtu ambaye hajazoea kufanya kazi ngumu, muache akiamka atakula,” mzee Reli ya Uhuru alimwambia mkewe bila kujua Nelly licha ya kuchoshwa na kazi lakini zaidi ni kwa vile alitoka kumdungua kiumbe na pombe aliyokunywa.

Leave a Comment