×

The angel of darknes – 27

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba wawili hao ni wapenzi.

Hatimaye wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya. Mapenzi kati ya Arianna na Msuya yanaanza kukolea, jambo linalosababisha Diego awe kwenye wakati mgumu sana kihisia kutokana na wivu uliokuwa ukimsumbua kila kukicha.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Usiogope, mimi nataka upone mapema ili mikakati ya harusi iendelee kama kawaida,” alisema Msuya, Arianna akawa hana cha kufanya zaidi ya kukubali kwa shingo upande. Alijua kama daktari huyo akimfanyia vipimo, ukweli kwamba hakuwa anaumwa bali madawa ya kulevya aliyokuwa anatumia ndiyo yaliyokuwa yakimfanya hivyo ungefahamika.

Daktari alifanya kazi yake, akamchukua damu, haja ndogo pamoja na vipimo vingine kisha akaaga na kuondoka kwa ajili ya kuelekea maabara na kuahidi kwamba angerejea muda mfupi baadaye.

Baada ya daktari huyo kuondoka, Anna aliendelea kuandamwa na mawazo huku akiwa na wasiwasi mkubwa kwamba kama Msuya akiujua ukweli anaweza hata kuahirisha mpango wake wa kumuoa.

“Lakini haya yote Diego ndiye anayeyasababisha,” alijisemea Arianna kwa sauti ya uchovu. Aliamini kwamba kitendo cha Diego kumuonea wivu mara kwa mara ndiyo kilichomtoa kwenye mstari na kujikuta akirudia tena kutumia madawa ya kulevya kwa kiwango kikubwa. Alitamani kujidhibiti lakini hakuwa na uwezo huo, akaishia kuijutia nafsi yake.

Baada ya takribani dakika arobaini, yule daktari alirejea akiwa na majibu yake, akamfuata Msuya ambaye naye alimfuata Arianna chumbani kwake, wakatoka pamoja mpaka sebuleni.

“Nimefanya vipimo kwa umakini mkubwa na kwa bahati nzuri Arianna huna tatizo lolote. Inaonesha ni uchovu wa kawaida tu kwa hiyo inabidi ujitahidi kula mlo kamili, kunywa maji mengi na kupata muda wa kutosha wa kupumzika,” alisema daktari huyo, Arianna akawa anatingisha kichwa kuonesha kuelewa kinachosemwa na daktari.

Kwa Msuya alishindwa kuelewa majibu hayo yalikuwa na maana gani kwani kwa mtazamo wake, alikuwa anaumwa na kama asipopatiwa tiba mapema, uwezekano wa kuwa na afya njema siku ya harusi yao ulikuwa mdogo.

“Dokta, umefanya kazi yako kwa umakini kweli?”
“Ndiyo bwana Msuya, umefanya kazi na mimi kwa kipindi kirefu nadhani unajua kwamba sina desturi ya kumpa mtu maradhi ambayo wala hana kama wanavyofanya madaktari wengi siku hizi,” alisema daktari huyo wakati akitoka kwenye jumba la Msuya.

“Sasa kwa nini anakuwa na hali ile? Wewe mwenyewe si umemuona?”
“Nimemuona ndiyo, hebu kwamba fanyia kazi nilichokwambia. Kama hali itaendelea kuwa hivyohivyo kwa siku mbili mfululizo utanipigia simu nije tena.”

“Sawa daktari, nataka apone haraka kwa sababu tupo kwenye mipango ya ndoa, nataka kumuoa si unajua nimekaa muda mrefu nikiwa mpweke tangu nilipofiwa na marehemu mke wangu,” alisema Msuya, daktari huyo akawa anampongeza kwa uamuzi huo aliofikia.

“Tena umepata mtoto mbichi kabisa, ameumbwa akaumbika haswaa,” alisema daktari huyo na kuwafanya wote wawili waangue vicheko. Akamsindikiza mpaka getini, wakaagana kisha Msuya akarudi ndani na kuwaita wafanyakazi wake.
“Mbona umewaita wote? Unataka kuongea nao nini?” Arianna aliyekuwa amejilaza kwenye sofa alimuuliza Msuya.

“Nataka niwape maagizo yaliyotolewa na daktari, nakupenda sana Arianna na sipendi kuona unateseka, lazima wakuhudumie vizuri ili upone haraka,” alisema Msuya. Tayari wafanyakazi wake wote walikuwa mbele yake ambapo aliwapa maagizo ya kuhakikisha Arianna anakula vizuri na kupata muda wa kutosha wa kupumzika.

Wafanyakazi wake walimuitikia kwa adabu kisha wakatawanyika kwenda kuendelea na majukumu yao. Arianna na mumewe mtarajiwa wakawa wanajadiliana kuhusu mambo mbalimbali jinsi ndoa yao itakavyokuwa.

“Ulisema unataka fungate tukalie wapi?”
“Sema wewe unataka twende sehemu gani ambayo utafurahi kufika.”
“Sijui sehemu yoyote nzuri, chagua wewe.”
“Nataka nikupeleke Miami nchini Marekani.”

“Marekani? Whaooo!”
“Utafurahi?”
“Nitafurahi sana Msuya, sijawahi kwenda ila nasikia kuzuri sana.”
“Kuzuri sana, nataka tukakae mwezi mzima,” alisema Msuya, wakawa wanaendelea kujadiliana mambo mbalimbali mpaka muda wa chakula cha jioni ulipowadia. Diego akaenda kujumuika nao kwa chakula cha usiku huku akionesha kutokuwa sawa kutokana na wivu uliokuwa ukiendelea kumfukuta ndani ya moyo wake.

Baada ya chakula cha usiku, Diego aliondoka kimyakimya kurudi chumbani kwake, jambo lililosababisha Msuya ahoji.
“Kaka yako yuko sawa kweli?”

“Yuko sawa, kuna jambo nimemsema mchana ndiyo maana amekasirika, huyo ndivyo alivyo inabidi umzoee tu,” Arianna alidanganya kwani hakutaka Msuya aendelee kumhoji zaidi kuhusu suala hilo.

Baadaye waliagana, Arianna akaenda chumbani kwake na Msuya akaenda chumbani kwake. Aliamua kumuacha apumzike siku hiyo ili awahi kupona.

Siku hiyo ilipita, kesho yake Msuya akawahi kuamka na kujiandaa kwenda kazini. Akampitia Arianna chumbani kwake na kumkuta bado amelala, akaaga na kuondoka zake huku akimsisitiza kuhakikisha anafuata maelezo ya daktari.

Alipoondoka tu, Diego aliyekuwa akichungulia kupitia dirisha ala chumbani kwake, alitoka na kuelekea chumbani kwa Arianna.

Msuya akiwa anakaribia kufika ofisini kwake, alikumbuka kwamba kuna kitu cha muhimu sana amesahau nyumbani kwake, harakaharaka akageuza gari na safari ya kurudi nyumbani kwake ikaanza.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Leave a Comment