×

Jini Mauti-13

JINI MAUTI

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Kwa nini mimi? Kwa nini Thomas amenikataa? Haiwezekani, ni lazima nimroge, ni lazima awe wangu kwa lazima…” nilijisemea huku nikilia darasani, hakukuwa na mtu aliyegundua hilo kwani niliegemea mezani.
SASA ENDELEA…

Mapenzi hayaeleweki na kamwe hayawezi kueleweka katika dunia hii. Wakati nikiwa silali, sinywi wala sili kwa ajili ya Thomas, cha kushangaza, yeye hakuwa akinipenda, alikuwa radhi kuona nikiumia na kulia lakini si kuwa naye.

Upande wa pili kulikuwa na kijana mmoja, aitwaye Mohammed ila hapo shuleni walipenda kumuita kwa jina la Mudi. Alikuwa mvulana wa kawaida sana, hakuwa mzuri na nilimuona kama watu wengine kumbe pasipo kujua, Mudi alikuwa amekufa na kuoza kwangu.

Aliwaambia rafiki zake kwamba alikuwa akinipenda zaidi ya msichana yeyote, niliposikia hivyo, hakika nilifarijika lakini tatizo likawa moja, yaani nilimpenda Thomas ambaye hakuwa na muda nami huku nikiwa simpendi Mudi ambaye kila siku aliwalalamikia watu kuhusu penzi lake kwangu.

Mudi hakutaka kuvumilia, alikuwa tayari kwa kila kitu, alichoamua ni kunifuata na kuniambia ukweli kwamba alikuwa akinipenda. Mimi nimkubali Mudi? Kivipi? Kwa nini niwe naye? Kila nilipojiuliza, nikakosa jibu kabisa.

Nilimtaka Thomas tu, aliyeniliza, aliyenifanya nisile vizuri wala nisilale vizuri. Baada ya kusikia kuhusu Mudi, nikapuuzia, sikutaka kumuweka akilini kabisa. Usiku wa siku hiyo ambao nilikuwa na mawazo mengi juu ya Thomas, nilimwambia bibi tulipokutana uwanjani kwamba nilitaka Thomas anipende, tena anipende zaidi ya mwanamke yeyote yule.

“Una uhakika hutaweza kufanya naye mapenzi hadi mfunge ndoa?” aliniuliza bibi, sikujua swali lake lilimaanisha nini.
“Kivipi?”
“Niambie kwanza.”
“Nahisi!”

“Kwa hiyo huna uhakika?”
“Kwani nikifanya naye kuna tatizo?”
Bibi alikuwa mwelewa, alielewa kwamba katika kizazi hiki hakukuwa na watu ambao wangekubaliana wawe wapenzi bila kufanya mapenzi. Mimi ndiye niliyeng’ang’ania kuwa na Thomas, alichokifanya ni kumfanyia madawa Thomas.

Aliniambia nijiandae, alitaka twende sehemu fulani, sikujua ni wapi, nikajiandaa, akanishika mkono na kuniambia nifumbe macho, nikafumba, akanisogelea kisha kunipaka unga fulani machoni, baada ya hapo, wote wawili tukapotea, tulipoibuka, tulikuwa chumbani kwa Thomas, alikuwa amelala chali.

Bibi akamfuata kisha kumuinua, akampakata na kuniita. Nikaanza kuwasogelea pale kitandani. Mapigo yangu ya moyo yalikuwa yakienda mbio, nilimpenda sana Thomas zaidi ya mtu yeyote yule, nilipomfikia, akaniambia nimpakate mimi, nikafanya hivyo.

Baada ya hapo akanipaka unga fulani mdomoni kisha kuniambia nimbusu, kweli nikafanya hivyo na kumbusu shavuni. Mapenzi yalinichanganya mno, baada ya kufanya hivyo, bibi akaanza kuongea maneno yake ambayo sikuwa nikiyaelewa, aliyaongea kwa muda wa dakika kadhaa kisha kuniambia tuondoke na asubuhi yake ningeyaona mafanikio makubwa. Tukaondoka.

Asubuhi nilipoamka, nikajiandaa kama kawaida yangu. Kumbuka nilikuwa kidato cha pili, sikuwa nimewahi kukutana na mwanaume kimwili, japokuwa niliona kila dalili za kufanya hivyo zikiwa zinaonekana.

Mama alijua kwamba nilikuwa malkia wa wachawi mara baada ya kukabidhiwa mkoba ule na bibi ila kilichomshangaza, mbona sikuwahi kuonesha dalili zozote kama nilikuwa mchawi? Alinichunguza mno lakini hakufanikiwa kuona chochote kile.
Nilipofika shuleni na kukaa kwenye kiti changu, ghafla nikazibwa macho na mtu ambaye sikumuona, alikuwa nyuma yangu, nilipogusa vidole vyake, havikuwa vya msichana, vilikuwa vya mvulana hivyo nikashindwa kugundua alikuwa nani.

Aliponiachia na kugeuka, moyo wangu ukapiga paaa, alikuwa Thomas. Uso wake ulitawaliwa na tabasamu pana, alionekana kuwa mwenye furaha mno, nilipoyaangalia macho yake yalionesha ni jinsi gani alifurahi kuniona.
Itaendelea wiki ijayo.

Leave a Comment