Ilipoishia wiki iliyopita;
Kwa jinsi nilivyomdadisi, alifanikiwa hadi kunieleza kuhusu mganga aliyesifika kwa kazi hiyo, aliyesema anaishi kijiji kimoja kinachopakana na Mkoa wa Mbeya. Kimoyomoyo nikajisemea huko ndiko nilitaka kwenda na kupanga siku iliyofuata kuanza safari!
Sasa endelea…
Nilizugazuga pale kwa muda hadi wakati wa kwenda kulala ulipofika, nikaingia chumbani kwangu nikiwa na mawazo mengi sana. Nia ya kutaka utajiri wa haraka ilikuwa imeharibu kabisa akili yangu, kwa sababu ndoto zote za kufanya kazi kwa bidii ili kufikia mafanikio niliziona zinachelewesha kufika kileleni ninakotaka.
Asubuhi na mapema niliondoka kama mtu ninayeenda kwenye shughuli zangu, nilifika kwenye kituo cha magari ya kuelekea huko kama nilivyoelekezwa jana yake. Nikakuta magari ya kizamani sana ya Land Rover 109 ndiyo yanapakia abiria.
Nikajipakia na baada ya saa moja hivi gari likawa limejaa na kuanza safari. Ulikuwa ni mwendo mrefu, hasa kwa sababu ya ubovu wa barabara. Ilituchukua saa kama sita hivi kufika kituo ambacho nilitaarifiwa kuwa hapo nitatakiwa kuchukua usafiri mwingine wa bodaboda au baiskeli.
Nilipata bodaboda kwa nauli ya shilingi elfu kumi na saa moja baadaye nikafika kijiji cha huyo mtaalam. Alinifikisha hadi nyumbani kwake ambako nilikuta watu wengi wakiwa wanasubiri zamu zao. Baada ya kutulia kidogo, msaidizi wa mganga aliniambia kuwa utaratibu wa pale ni kuandikisha majina na mzee anawaita watu kulingana na orodha aliyonayo ndani.
Nikajiandikisha na kwa vile watu walikuwa ni wengi, nikaamua kuzunguka zunguka kidogo pale kijijini ili kunyoosha viungo maana usafiri mrefu na kwenye njia mbaya ulinifanya ninyong’onyee kidogo. Kama ambavyo vijiji vingi vilivyo, hakukuwa na maeneo ya maana zaidi ya vilabu vya pombe na maduka machache yaliuza bia.
Jioni baada ya kuzunguka zunguka, nikarejea kwa mganga ambako niliambiwa pia kuwa chakula cha wateja hupikwa pamoja na huliwa bure. Saa mbili hivi tukala wali kwa maharage, msosi ambao ulikuwa mtamu sana, kitu kilichoashiria wapishi walikuwa ni akina mama miongoni mwa wateja kutoka mjini.
Siku hiyo sikufanikiwa kupata huduma lakini kesho yake majira ya saa sita mchana nikaitwa kwa mganga. Kufika kule alichukua karatasi nyeupe, akaniuliza majina yangu matatu na kuyaandika, kisha akachukua ubao mweusi, akaanza kuchora vitu ambavyo sivifahamu. Baada ya kama dakika kumi akainua sura yake na kuniangalia, akakohoa kama ishara ya kutaka kuzungumza.
Akaniambia ameona katika vifaa vyake nia yangu ya kutaka utajiri na kwamba nipo tayari kumtoa kafara mtoto wangu. Akaniuliza kama ni kweli, nami nikamkubalia kuwa ni kweli. Basi akarejea tena kwenye ubao wake akaendelea kuchora.
Awali nilitaka nimwambie kuhusu majaribio yale niliyofanya kwa yule mganga, lakini upande mwingine ukaniambia niache. Baada ya kuandika, akaniambia usiku nitatakiwa kuoga maji ya dawa na kufukishwa ili kuuweka mwili wangu katika ulinzi salama, maana kazi ninayotaka kuifanya inaonekana kuwa na vikwazo vingi.
Usiku nikafanya kama nilivyoambiwa na mganga na nilienda kulala nikiwa nimechoka sana. Kesho yake asubuhi na mapema nikakodi bodaboda na kuanza safari kuelekea Makete. Nilifika huko majira ya kama saa nane hivi, nikaingia chumbani kwangu, nikalipia chumba kwa siku tatu, kisha nikaaga kuwa ninaondoka kurudi kwetu.
Kwa kuwa ilikuwa bado mapema, nilipata usafiri hadi Njombe, ambako nilichukua basi hadi Makambako na baadaye nikapata lifti kwenye gari dogo ambalo saa mbili usiku, tulifika Iringa. Nilipata chumba kwenye hoteli moja iliyo katikati ya mji.
Nikiwa nimelala kama saa nane usiku, ghafla nikahisi joto kali chumbani na kwa uzoefu wangu wa Iringa, kipindi kile ni cha baridi. Haraka nikaamka, nikasikia harufu ya moto, nikavaa suruali haraka nikatoka nje. Kulikuwa na moshi mwingi pale kwenye korido, sikuona chochote!
Je, nini kilitokea? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kweli katika toleo lijalo.