KAMA kawaida ya kolamu hii kuwaleta mastaa mbalimbali na kuwabananisha mambo kadha wa kadha kuhusiana na maisha yao kwa ujumla, leo hii tunaye staa wa filamu Bongo, Wastara Juma ambaye amefunguka kama ifuatavyo;
Msomaji: Kwa nini kila siku unapenda kusema hakuna mwanaume mkweli kwako zaidi ya marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki,’ huoni huyo mpenzi uliyenaye atajisikia vibaya?
Wastara na Bond
Wastara: Bado sijaamua kuwa na mtu ‘serious’ ndiyo maana nasema hivyo sababu muda mwingi nipo mwenyewe, endapo akitokea mtu mwenye mapenzi ya kweli kwangu kama alivyokuwa yeye hutasikia nikiongea kauli hiyo.
Msomaji: Dada uhusiano wenu na Bond umefikia wapi kwani nimesikia mmeachana?
Wastara: Hilo swali lipo nje ya uwezo wangu, maana hivyo ni vitu ‘private’ unavyoelewa ndiyo hivyohivyo.
Msomaji: Dada Wastara nakupongeza kwa uigizaji wako pia nilivutiwa sana na filamu yako ya Mboni Yangu ila mbona sasa upo kimya sokoni tofauti na kipindi kile cha marehemu Sajuki ulikuwa hukauki?
Wastara: Soko la filamu hivi sasa halilipi kwa hiyo huwezi kutegemea upande mmoja, filamu sijaacha mwanzoni mwa mwaka ujao nitaachia filamu yangu ya Hapendeki na Faulo ila kwa sasa nipo bize na mambo mengine.
Msomaji: Nikupongeza kwa ujasiri wako wa kugombea ubunge, umejifunza nini baada ya kukosa nafasi hiyo na umejipangaje?
Wastara: Nimejifunza mengi ila miongoni mwa vitu vilivyonikwamisha sikuwa na pesa nyingi, nimegundua unatakiwa uwe na mkwanja wa maana pia uwe karibu na wananchi wa eneo lako inakuwa rahisi kukubalika.
