×

Kuzimu Na Duniani-9

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Nashangaa, sina usingizi wala sitaki kulala. Sijui kuna nini? Chumba nakiona kizito sana. Lakini jioni nilikwenda kanisani, mchungaji akaniambia nina majaribu mazito sana mbele yangu, nijitahidi kumwomba Mungu.”

Nilishtuka mwenyewe kwa maneno hayo ya mke wangu. Kwangu yaliashiria kwamba, kiroho mchungaji wake alijua kuna jambo ndani ya familia yangu.
SASA ENDELEA MWENYEWE…

“Ungelala ili ijulikane moja, kesho tutaendelea na mambo mengine,” nilimwambia.
Lakini kabla ya kulala, akaniangalia na kusema: “Lakini na wewe mbona kama ulikuwa unaweweseka ukiwa usingizini halafu unaota ndoto za ajabuajabu?”

“Ni hali tu! Kwani wewe hujawahi kuweweseka?” nilimjibu na kumuuliza.
“Nimewahi lakini wewe zaidi. Halafu nikawa nasikia kama sauti za wanawake zikikupongeza. Ilikuwa nini?”

Nilishtuka sana kusikia hivyo kwani kama unakumbuka ndugu mwandishi ni kweli wale wanawake walinipongeza kwa kazi nzuri ya kupindua gari. Lakini nilijiuliza, inawezekana kweli kwamba, mtu akusikie upo kwenye ndoto unazungumza halafu akawasikia na unaoongea nao?!

Nilikataa moyoni lakini nikasema kama ni kweli, basi mke wangu atakuwa anapewa ujumbe kupitia nguvu kubwa ya Mungu.

“Hapana, labda wewe ulisikia watu wakizungumza kwenye redio ya jirani. Yaani mimi niote ndoto halafu wewe uwasikie ninaoongea nao? Inawezekana kweli?” nilimuuliza.
“Ndiyo na mimi nashangaa, nimesikia kabisa wanawake wakisema kukupongeza nikajiuliza sana. Mtu anaweza kuwasikia watu wanaoongea na mtu anayeota ndoto?!”
“Ndiyo maana nimekwambia mke wangu wewe ulisikia watu wa kwenye redio ya nyumba ya jirani. Unajua ukweli wote kwamba huwezi kuwasikia watu wanaoongea na mtu anayeota ndoto, sasa wewe hushangai?”

“Nashangaa. Lakini je, na wewe kwenye ndoto hakuna wanawake waliokuwa wanakupongeza kwa jambo lolote?”
“Sijawaona.”

Basi, tulilala mpaka kunakucha. Siku hiyo mimi nilichelewa kuamka tofauti na kawaida yangu saa kumi na moja na nusu mpaka kumi na mbili kamili. Mke wangu alipoamka alianza kusali. Hali ile ilinipa shida sana. Niliota ndoto eti napita mtaani halafu kuna watu wakaanza kunikimbiza.

Nilikimbia mpaka nikafika wakati miguu ikaishiwa nguvu, nikaanza kutembea kwa kasi huku wale watu wanaonikimbiza wakiwa wameshika mapanga na mikuki wakinikaribia.

Ili kukwepa kuuawa, niliamua kusimama na kuwageukia, nikanyoosha mikono ya kusalimu amri, kwamba niko chini yao. Walinikamata, wakanichukua mpaka kwenye tanuri la moto kwa ajili ya kunitupia humo. Sasa wakati wanataka kunirusha, nilipiga kelele nikiomba msamaha lakini nikiwa silijui kosa langu kwao.

Walinikatalia, wakaanza kuhesabu moja, mbili, ile wanataka kusema tatu ili wanirushe sasa, nilishtuka kutoka usingizini mpaka nikakaa kitandani. Nikawa nahema, macho nimeyatoa pima. Mke wangu akanishika mkono na kuniuliza kuna nini! Nilimwambia ndoto.

“Ndoto imefanyaje mume wangu?”
“Nimeota ndoto mbaya sana.”

“Umeotaje kwani?” aliniuliza mke wangu huku bado akiwa amenishika mkono mmoja. Nilikuwa bado nahema sana mpaka nikashindwa kuzungumza. Mkono mmoja nilijishika kifuani nikihema kwa kasi.

“Umeotaje kwani mume wangu?” aliniuliza tena mke wangu. Alionekana kuwa na shauku kuu ya kutaka kujua.

“Nimeota nakimbizwa na watu wenye mapanga na mikuki.”
“He! Huyo ni shetani na ameshindwa katika Jina la Yesu,” alisema mke wangu kwa sauti ya kukemea, nikasikia kama nachomwa moto mwili mzima.
“Ikawaje sasa?” aliniuliza tena mke wangu.

“Sikukubali, nikaanza kukimbia, wakawa wananikimbiza. Nilifika mahali nikawa nimechoka sana sasa, nikaamua kutembea lakini wao waliendelea kunikimbiza, ikabidi nisamame na kuwageukia, nikawaomba samahani. Wakakataa, wakanishika na kutaka kunirusha kwenye tanuri la moto. Sasa wakati wamenibeba juujuu wakihesabu moja mbili mpaka tatu ili wanirushe, ilipofika mbili ndiyo nimejikuta nimeshtuka.

“Pole sana, nadhani kuna wabaya. Na mimi nimeamka nikaanza kusali na kukemea kwa ajili ya familia yangu. Ni shetani tu mume wangu, lakini ameshindwa katika…kabla hajamaliza Jina la Yesu, niliziba masikio kwa vidole ili nisisikie kwani niliamini yale maumivu ya moto muda ule yalitokana na yeye kusema hilo jina la Yesu.

Lakini licha ya kuziba masikio, bado nilisikia maumivu makali sana. kumbe kinachochoma si kusikia jina bali hata likitajwa jirani na wewe pia tosha. Nikasema kwa sauti mamaaa! Mke wangu akasimama, akanishika mabegani.
Itaendelea wiki ijayo.

“Nini tena jamani?”
Kilichoendelea hapo sikumbuki, nika kama nilipoteza fahamu lakini nilipokuja kuzinduka, nilimwona mke wangu akilia kwa uchungu huku akiwa amepiga magoti na kulalia kitandani kwa upande wa kifuani huku akisali.

Alipobaini nimezinduka, alikaa na yeye kitadani, akaniangalia kwa macho yenye huruma na wasiwasi kisha akasema:
“Unajua saa hizi ni saa ngapi?”

Niliangalia saa nikabaini ni saa sita na dakika kumi na mbili mchana. Nilishtuka sana, nikaangalia nje kwa kutoamini, nikamtajia muda kama alivyoniuliza. Akaniuliza tena.
“Unajua kilichotokea kwako?”

Je, nan wewe msomaji unajua kilichotokea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave a Comment