SI umeisikia ngoma mpya ya Diamond Platinumz ya Utanipenda aliyoachia Ijumaa ya wiki iliyopita? Basi pata picha inagongwa ‘live’ pale Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live, Mbagala-Zakhem jijini Dar kwenye Sikukuu ya Krismasi, Desemba 25, mwaka huu.
Ndivyo mchongo ulivyo, Diamond ambaye atapiga shoo hiyo kubwa siku hiyo ya kufunga mwaka 2015 kwenye uwanja huo wa burudani, amepanga pia kutoa sapraiz special kwa kuitwanga live kwa mara ya kwanza ngoma hiyo kwa ajili ya mashabiki wake watakaojitokeza.
Vurugu mitandaoni
Tangu kuachiwa kwa ‘chupa’ hiyo, saa chache baadaye, gumzo la kufa mtu liliibuka kwenye makutano ya wengi kule mitandaoni kupitia WhatsApp, YouTube, Facebook, Twitter na Instagram zinakopatikana timu za kila aina, wakieleza kuguswa na mistari na video hiyo iliyotengenezwa na Godfather wa Afrika Kusini.
Kama hiyo haitoshi, wengi walitamani kumsikia Diamond au Chibu akitwanga ngoma hiyo live na mwisho wa siku ikabainika ni Dar Live pekee ndiyo kuna shoo ya karibu kwa sasa atakayotumbuiza msanii huyo na madensa wake mashuhuri.
Msikie Diamond
Licha ya kwamba hajawahi kuwaangusha mashabiki wake kwenye shoo tangu apate umaarufu takriban miaka sita iliyopita, lakini safari hii ameahidi kufanya mara mbili zaidi ya anavyofanya akiwa kwenye majukwaa mengine katika siku za nyuma
“Waje tu wengi, sijawahi kuwaza kuwaangusha watu wangu, najua Watanzania wanataka nini na nipo hapa kwa ajili ya kuwafurahisha wao na kuzidi kuipeperusha bendera ya Tanzania. Nitafanya zaidi ya huko nyuma, nataka kufunga mwaka kwa staili ya pekee.
“Hizo sapraiz nilishaahidi tangu mwanzo na siku zinavyozidi kwenda ndiyo mizuka inazidi kupanda, sitaki kuongea mengi, tukutane Desemba 25 pale Dar Live,” alisema Diamond.
Msagasumu naye ndani
Mkali wa Singeli, Msagasumu anakosa vipi kwenye shoo ya kibabe kama hiyo? Atatia timu na atakamua ngoma zake zote kali zinazotamba mitaani. Nyimbo kama Inaniuma Sana aliyomshirikisha lejendari Juma Nature, Huyo Mtoto, Shemeji Unanitega, Naipenda Simba na nyingine kibao.
“Wanangu wote tukutane pale Dar Live, itakuwa usiku wetu wote. Ngoma zote kali nitatwanga kama kawa, waje wengi turuke pamoja, tufurahi,” alisema Msagasumu.
Wakali Dancers nao wapo
Kundi linalosifika kwa sarakasi na kucheza muziki wa kila aina, Wakali Dancers, nalo litakuwa ndani ya nyumba siku hiyo kukinukisha na kupagawisha uwanja mzima kwa mashabiki watakaojitokeza. Wametamba kuwa itakuwa si ishu ya kitoto kwani wataonyesha mashabiki mbwembwe zao zote zikiwemo zile za kujiku-njakunja kwa staili kibao na kudansi ngoma za kisasa za ndani na nje ya nchi.
“Sina mengi ya kueleza kuhusiana na shoo baabkubwa tutakayoifanya Dar Live hiyo Desemba 25, michezo yote ya hatari itafanyika siku hiyo, kutoa burudani ndiyo zetu. Kwa atakayekosa atajilaumu, tutafanya kila kitu kwa ajili ya kufunga mwaka,” walitamba memba wa kundi hilo.