
MWANAMITINDO wa kimataifa wa Tanzania anayefahamika zaidi kwa jina la mdogo wa msakata kabumbu wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga katika Klabu ya Royal Antwerp ya nchini Ubeligiji aitwaye Happy Samatta, amezua jambo nchini Uturuki.
Ghafla tu, Happy amekuwa gumzo nchini humo baada ya kuwafunika wanamitindo mbalimbali na kuibuka kidedea kwa kuwabunia watu mbalimbali nguo; jambo ambalo limemfanya kujizolea umaarufu mkubwa.
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA kwa njia ya WhatsApp, Happy anasema kuwa, anamshukuru Mungu kwa hatua ambayo amefikia kwa sababu haikuwa rahisi kabisa yeye kufikia hapo alipo ndiyo maana kila kukicha anajitahidi kufanya vizuri kwenye kazi yake hiyo ya ubunifu na mitindo.
“Haikuwa rahisi na siyo rahisi kukubalika hata kidogo kwenye nchi nyingine, lakini kwa mimi naona wamenikubali sana na nimewatengenezea watu wengi sana mavazi na ninatarajia kufungua duka kubwa sana huku,” anasema Happy.
Happy anaongeza kuwa, anamshukuru kaka yake, Samatta kwa kumpa sapoti kubwa maana anafanya kazi yake vizuri na amekuwa ni tishio kwa upande wa ubunifu.
“Namshukuru sana kaka yangu, amekuwa akinisapoti sana katika hilo kwa sababu ni mtu ambaye anapenda niendelee kuwa bora kila siku na mimi najivunia kwa hilo,” anasema Happy.
STORI; IMELDA MTEMA, DAR