WAKATI serikali ikipinga ukatili dhidi ya watoto, Shida Mugabo (25), mkazi wa Kitongoji cha Nyamika, Kijiji cha Mwikoro Kata ya Buruma wilayani Butiama, Mara anadaiwa kuwafanyia unyama wa kutisha watoto wake wa kuzaa, Hamis (5) na Ali (3) kwa kuwafunga kamba mikononi kisha kuwachoma moto mikononi akiwatuhumu kuiba mboga ya kisamvu jikoni.
Walioshuhudia tukio hilo, walisema lilijiri hivi karibuni ambapo kabla ya tukio, mwanamke huyo aliondoka nyumbani saa 2 asubuhi kwenda msibani katika kitongoji hicho na kuwaacha watoto hao bila kuwaandalia chakula.
Walisema, mama huyo aliporudi jioni alikuta mboga hiyo aliyoiacha kwenye chungu imeliwa hivyo akawachukua watoto hao na kuwachoma moto licha ya kujitetea kuwa walifanya hivyo kutokana na njaa.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwikoro, Kundi Manyerere alipozungumza na gazeti hili kuhusu tukio hilo alisema kuwa, Shida na watoto wake walifikishwa ofisini kwake na majirani zake wakitaka mwanamke huyo achukuliwe hatua za kisheria kwa kuwafanyia ukatili huo watoto hao.
“Majirani waliwasikia watoto hao wakilia usiku kucha kutokana na maumivu makali ya kuchomwa moto bila kupelekwa hospitalini.
“Baada ya kumhoji Shida ofisini kwangu alikiri kuwachoma moto watoto wake kwa kisingizio kuwa, ana maisha magumu nyumbani kwake hivyo asingeweza kuchuma mboga nyingine kutokana na mzazi mwenzake aliyezaa naye watoto watatu kumtelekeza,” alisema kiongozi huyo.
Mmoja wa watoto hao, Hamis ambaye aliunguzwa kiganja cha mkono wa kulia, alilieleza gazeti hili kuwa, waliamua kula mboga kutokana na njaa kali kwa vile pia usiku wa kuamkia siku hiyo walilala na njaa.
Mwanamke huyo alifikishwa Kituo cha Polisi Kiabakari na kuachiwa kwa maelekezo ya kwenda kuwatibu watoto hao.
Hata hivyo, gazeti hili lilipoitembelea familia hiyo, liliwashuhudia watoto hao na mama yao wakila maembe na mapapai mabichi kama mlo wa mchana kutokana na kutokuwa na chakula.
Polisi Kiabakari wamethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema walimtaka mwanamke huyo kwenda kuwatibu watoto hao.