Hali ya sitofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.
Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Nyuma ya kila kitu, kuna mwanaume mmoja mwenye sura mbaya, tena akiwa ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, (DCP) Dickson ndiye ambaye anafanya mauaji hayo pasipo kugundulika. Kazi yake ni kununua machangudoa na yeyote atakayemgundua, humuua kikatili na kuondoka zake. Polisi wanachanganyikiwa, wanamtafuta muuaji, wanamkosa kwani anaonekana makini hasa kwenye kufuta alama za vidole vyake.
Hali ya hofu inaendelea kutanda jijini Dar es Salaam.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Hakukuwa na amani tena, hali iliyokuwa ikiendelea ilimuogopesha kila mtu, wanawake wengi wakaogopa, idadi ya machangudoa waliokwenda kujiuza usiku ikaanza kupungua na wengi kubaki vyumbani mwao wakipumzika.
Idadi ya wanawake mfululizo waliouawa ilimtia hofu kila mmoja, upelelezi ulikuwa ukiendelea kila siku lakini hakukuwa na mafanikio yoyote yale, yaani hata ile miili waliyokuwa wakiichukua na kwenda kuipima kwa lengo la kuona alama za vidole, hawakufanikiwa kuona chochote kile.
Hawakujua ni wapi pa kuanzia ila kwa sababu kila kona polisi ndiyo walionekana kufanya uzembe mkubwa kwa kutokumpata muuaji huyo, walichoamua ni kuwatuma polisi wa kike watatu, wapelelezi waliokuwa mahiri kwenye mapigano, warembo ambao kazi yao ilikuwa moja tu, kuhakikisha muuaji anapatikana haraka iwezekanavyo.
“Subira…” aliita mkuu wa kituo cha polisi Magogoni.
“Ndiyo mkuu!”
“Hii kazi ni yako na wenzako, hakikisheni kila kitu kinakwenda sawa na muuaji anapatikana, sawa?”
“Sawa mkuu!”
“Nenda na wenzako, nitawataarifu wakuu juu ya mpango huu kabambe…” alisema mkuu huyo wa kituo.
Wasichana wanne waliandaliwa kwa kufanya upelelezi huo. Kwa kuwaangalia, walionekana wasichana warembo ambao wangeweza kumtega kila mwanaume aliyepata nafasi ya kuwaona.
Kulikuwa na msichana aliyeitwa Subira, huyu alikuwa msichana mwembamba, mwenye sura ya Kitusi, aliyevutia ambaye alipendezeshwa na umbo namba nane alilokuwa nalo. Subira alipenda kuzifunga nywele zake kwa kibanio na mara nyingi sana alipenda kuvalia suruali.
Mbali na subira, kulikuwa na mwanamke mwingine aliyeitwa Happy. Alikuwa msichana mrembo, aliyejaajaa ambaye kwa nyuma, alijazia vilivyo. Hakuwa mzuri wa sura lakini umbo lake lilikuwa matata mno.
Msichana wa mwisho alikuwa Tatu. Huyu alikuwa mzuri wa sura, hakuwa na umbo kubwa sana, alikuwa wa kawaida lakini kila alipotembea, kiuno chake kilionekana vilivyo. Mwili wake ulinyambulika vilivyo, kwa juu alikuwa mpana kidogo lakini kiuno chake kilikuwa chembamba na chenye kutamanisha.
Hao ndiyo wasichana waliotakiwa kufanya kazi hiyo, walitakiwa kujigawa, mmoja alitakiwa kusimama Kinondoni-Makaburini, mwingine na Sinza-Ambiance na wa tatu alitakiwa kukaa Sinza-Mori.
Hawakutaka kuwapeleka wasichana hao sehemu nyingine kwani hizo ndizo pekee zilizokumbwa na matukio ya mauaji tofauti na zile za Buguruni na Mbagala ambapo napo huko kulikuwa na ongezeko kubwa la machangudoa.
Wakati mipango yote ikiendelea, pasipo kujua, Kamanda Dickson hakupata taarifa kabisa. Hakufanyiwa hivyo makusudi ila taarifa nyingi zilizopelekwa ofisini kwake kwa njia ya maandishi, hakuwa akizisoma, bado kichwa chake kilikuwa kimechanganyikiwa na muda mwingi hakuwa mkaaji ofisini.
Taarifa ya wanawake hao watatu iliandikwa, iliwekwa mezani kwake lakini hakuwa na muda nayo, kilichomkosesha amani ni msichana Hadija tu ambaye aliamini kwamba alimuona kule chumbani walipokuwa.
Japokuwa hakuwa amekamilisha suala zima la kumpata Hadija lakini mwili wake haukuweza kutulia, bado uliwaka moto, ulikuwa kwenye matamanio makubwa ya kuwa na mwanamke karibu yake, hivyo alichokifanya, kama kawaida yake ni kwenda Kinondoni kwa ajili ya kununua changudoa.
Alipokaribia huko, idadi kubwa ya wanawake waliokuwa wakijiuza ilikuwa mbele yake, walisimama pembeni kabisa ya makaburi huku wakijaribu kuyasimamisha magari binafsi yaliyokuwa yakipita. Mavazi yao yalikuwa yenye mitego, nguo fupi, zilizoacha mapaja wazi na hata suruali za kubana.
Machangudoa hao walipoliona gari hilo, Volkswagen nyeusi, wakaanza kulisogelea huku wakitembea kwa mikogo kumvutia mtu aliyekuwa ndani ya gari hilo. Walipolikaribia, Dickson akashusha kioo cha gari lake na kuanza kuwaangalia wasichana hao.
“Wewe mrembo sogea huku,” alisema huku akimuita msichana mmoja, mzuri wa umbo, alijaajaa, hata nyuma, alivutia.
“Mimi?”
“Ndiyo! Mbona unaogopa?” aliuliza Dickson.
Msichana yule akasogea karibu ya gari lake na kumwambia aanze kugeukageuka ili amthaminishe vizuri, msichana huyo akafanya hivyo. Dickson akabaki hoi, kila alipomwangalia msichana yule, alichanganyikiwa, kwa umbo, alionekana kumzidi mpaka Pamela mwenyewe.
“Unaitwa nani?”
“Princess Allure,” alijibu msichana yule.
“Mmh! Hayo majina yenu shida sana, inakuwaje sasa?”
“Nakusikiliza wewe tu, mpaka asubuhi au shoti taimu?”
“Mpaka asubuhi!”
“Jiwe mbili,” alijibu msichana yule.
Mule garini alipokuwa, kulikuwa na giza hivyo ilikuwa ngumu sana kuuona uso wake. Alipokuwa akizungumza na msichana yule, hakuweza kugundulika japokuwa kichwani hakuwa na kofia yake kama kawaida.
Walipokubaliana malipo ya shilingi laki mbili, akamwambia msichana yule aingie ndani ya gari, akafanya hivyo na kuanza kuondoka kuelekea katika nyumba ya wageni pasipo kujua kwamba msichana yule aliyembeba hakuwa changudoa, alikuwa Happy, msichana aliyepelekwa hapo kwa ajili ya kukamilisha upelelezi wake wa kumgundua muuaji wa machangudoa. Kwa Dickson, msichana yule alionekana kuwa changudoa kama wengine, hivyo hakuwa na wasiwasi.
Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.