×

Aunt Lulu, huko ni kujirahisi kulikopitiliza!

1LULU Mathias Semagongo ndilo jina lake halisi, lakini watu wa burudani wanamfahamu zaidi kama Aunt Lulu. Ni binti mmoja mdogo aliyezaliwa mwaka 1987.
Historia yake inaonesha ni binti aliyekuwa na kipaji, kwani katika umri mdogo, tayari alikuwa mtangazaji wa kipindi cha watoto kilichokuwa kikiendeshwa na redio ya kwanza binafsi nchini, Radio One, kilichoitwa Watoto Show.

Binafsi nilimfahamu kuanzia mwaka 2006, alipokuwa mmoja kati ya washiriki wa shindano lililosisimua enzi hizo, la kusaka wanenguaji wenye vipaji, lililoitwa Kimwana Manywele Twanga Pepeta, ambalo liliratibiwa na Mtangazaji Maimartha Jesse.

Huenda kwa sababu ya umri, utoto au kutoshiriki aina f’lani ya maisha, mwili wa msichana huyu ulikuwa mwembamba ulioshiba, ambao haukuwashangaza wengi alipofanikiwa kuibuka kidedea katika shindano hilo na kujipatia zawadi ya gari dogo la kutembelea.

Ni kuanzia wakati huo, ndipo jina lake likaanza kupaa kwa umaarufu, kwani sasa alikuwa memba mzuri katika viwanja vya starehe vya Kibongobongo, Mango Garden, Msasani Club, Leaders Club, Msasani Beach Club, Travertine, Equator Grill, Bahama Mama na vingine vingi vya aina hiyo.

Aunt Lulu pia amewahi kufanya kazi ya utangazaji wa televisheni katika vituo kadhaa, ingawa sikumbuki kumuona akikifanyia kazi kipaji chake cha kunengua na hivi sasa, pia ni muigizaji wa filamu.

Lakini wakati wengine wakipata umaarufu unaobebwa na kazi zao, Aunt Lulu ni miongoni mwa wasichana wengi wa Bongo wenye majina makubwa yanayotokana zaidi na skendo kuliko shughuli zao.

Unamsikia zaidi akiandikwa kuhusiana na wanaume anaohusiana nao kimapenzi na mara kadhaa, akijisifia kuhusu umbile lake linalohusisha makalio yake makubwa!
Mambo mengine yanaweza kuwa ‘kipaji’ kingine alichobarikiwa, lakini baadhi ya matamshi yake yanatoa taswira halisi juu yake, kama hivi karibuni alipoeleza kuwa anatamani kukutanishwa na mwanamuziki nyota wa DRC, Koffi Olomide, kwani ana mzuka naye kimapenzi!

Kwamba hapo awali, aliwahi kusikia kuwa mkali huyo wa Ekotite, anapenda wanawake wenye makalio makubwa, hivyo anaamini akikutana naye, hachomoki!

Hisia huwa hazizuiliki, lakini kauli zinathibitika. Nina uhakika, kama angetaka, isingekuwa jambo gumu kwa Aunt Lulu kumfikia Koffi, siku ile alipokuja Bongo na kufanya shoo yake pale Escape One. Kama mwandishi au msanii, alikuwa na fursa kubwa.

Kwa sisi wengine tunaopenda tafsiri zaidi ya moja kwenye sentensi, tunadhani lengo lake la kuongea na waandishi na kuwaeleza kuhusu hilo, ilikuwa ni kama tangazo kwa wanaume wote wanaowahitaji wanawake wenye makalio makubwa.

Kwamba wasipate tabu, yeye yupo ‘singo’, wakati wowote anapatikana. Maana kama angekuwa ni mwanamke mwenye mpenzi wake, sidhani kama angediriki kutoa tangazo hilo.

Binafsi ninajua kuwa mastaa wengi wa kike wanafanya sanaa kwa lengo la kujiweka sokoni mikononi mwa wanaume, lakini sidhani kama inapendeza inapofikia hali kama hii, ya kujinadi waziwazi.

Hata kama makalio hayo siyo ya Kichina kama tunavyoambiwa, bado haileti heshima kwa msanii kujirahisi kwa namna yoyote hadharani, kwani wapo watoto wenye maumbile kama hayo ambao ni mashabiki wake, wanapata picha gani kuhusu miili yao?
Mambo kama haya yanaporipotiwa, yanawafanya watu wengine washindwe kukataa wanaposikia sifa zingine zisizofaa zinazotolewa juu yake kuhusiana na makalio hayo!
Aunt Lulu, huko ni kujirahisi kulikopitiliza. Jaribu kujiangalia upya, sawa ee?

Leave a Comment