×

Nelly Muosha Magari wa Posta-19

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale sharobaro Nelly alipoulizwa na fundi Yassin alijisikiaje kufanya kazi ya ufundi ambapo kijana huyo alimwambia alijisikia vizuri kwani mtoto wa kiume hapaswi kuchagua kazi. Je, kilifuatia nini? Songa mbele na utamu huu…

“Kama ni hivyo, poa sana tena kadiri tutakavyokuwa pamoja nitakufundisha kazi kibao,” fundi Yassin alimwambia Nelly.

Kwa kuwa gari lilikuwa likienda kwa kasi, kufumba na kufumbua walifika Tegeta ambapo walipanda basi la kuelekea Kisauke na hawakuchukua muda mrefu wakawasili site.

Kama kawaida, fundi alipofika getini alibonyeza kitufe cha kengele na baada ya dakika kama moja geti likafunguliwa. Ingawa ilikuwa kawaida kufunguliwa na Anne, siku hiyo likafunguliwa na Doreen.

Sharobaro Nelly na Doreen walipokutanisha macho kila mmoja akaachia tabasamu lakini fundi Yassin kwa umahiri mkubwa alijifanya anaangalia nyuma ili wasibaini kama aliona jinsi walivyotabasamu.

“Shikamoo fundi?” Doreen alimwamkia fundi Yassin.
“Marahaba, hujambo Doreen?” fundi Yassin alimsalimia Doreen.
“Sijambo fundi!” Doreen aliitikia.

“Mambo yako?” Doreen alimsalimia Nelly na kuachia tabasamu pana lililoonwa tena na fundi Yassin lakini fundi alijifanya hakuliona.

“Nzuri, za hapa?” Nelly aliitikia salamu ya mtoto huyo wa kishua.
“Poa!” Doreen aliitikia ndipo fundi Yassin akamuuliza kama akina Zakayo na Haruni walikwishafika.

“Wamefika lakini siyo zamani sana wako kule ndani, nahisi watakuwa wameanza kazi,” Doreen aliyekuwa kafurahi sana kumuona sharobaro Nelly aliwajibu.

Baada ya salamu msichana huyo ambaye mpaka muda huo alikuwa hajafunga geti alilifunga kisha akaanza kutembea kuelekea ndani lakini kabla hajaingia aliangalia nyuma na kugongana macho na ya Nelly, wote wakatabasamu.

“Yaani huyu kijana kanivutia sana, nitafanya kila liwezekanalo lazima nifurahi naye tena leo sijui kama itapita na nilivyo na hamu we acha tu!” Doreen aliwaza akiwa amejibwaga sofani.

Wakati Doreen anawaza hivyo, kama vile waliambiana na Nelly naye alikuwa amepanga kufanya ukomandoo wake kuhakikisha anamchinja mtoto huyo palepale kwao ili kujenga heshima.

“Kumuacha mtoto kama huyu aliyeonesha dalili zote za kunikubali ni kosa kubwa kuliko hata walilofanya mafisadi waliokwepa kulipa kodi za makontena bandarini, huyu namhesabia kama siyo dakika basi saa lazima niwe nimempa mambo,” Nelly aliwaza.

Nelly aliyekuwa akiwaza mambo ya kuduu tu alishtuka baada ya kumsikia fundi Yassin akisalimiana na Haruni na Zakayo, kisha Zakayo ambaye alikuwa mkubwa kuliko akina Nelly alimsalimia Nelly kwa kusema;

“Vipi dogo za tangu jana?”
“Poa bro, vipi hali yako?”
“Mi nipo fiti, nilidhani leo hautakuja kwa jinsi ulivyochoka jana maana naona hizi kazi hujazizoea?” Zakayo alimtania Nelly.

Nelly alimwambia atazizoea kadiri siku zinavyokwenda, kwa kuwa walikuwa bado hawajasalimiana na Haruni walipeana hi kisha fundi Yassin alimwambia Nelly akaendelee na kazi aliyokuwa akiifanya jana yake.

Nelly aliyefikiria siku hiyo angepangiwa kazi nyingine, alipoambiwa hivyo alifurahi sana kwani alijua ingekuwa rahisi kupiga stori na Doreen na hata kuingia ndani kwao.

Baada ya kupangiana majukumu, Nelly alibadili nguo na kwenda kuendelea na kazi huku fundi Yassin na akina Zakayo wakiendelea na kazi ya kuweka marumaru ndani.

Kwa kuwa akili yake ilikuwa kwa mtoto mkali Doreen, kabla hata ya kuanza kazi aligeuza shingo na kuangalia dirishani si akamuona Doreen akiwa anamtazama kwa jicho linalosema ‘jamani wewe kaka na uzuri wote huo unafanya kazi ya ujenzi!’
Kitendo cha wawili hao kutazamana, walitabasamu kwa pamoja ndipo Doreen alimuuliza Nelly kama alifungua kinywa, kwa kuwa hakunywa hata maji alimwambia bado.

Msichana huyo alipojibiwa hivyo alimwambia Nelly aingie ndani kwa kupitia mlango wa uani ili amwandalie chai, Nelly bila woga akafuata maelezo na kwenda moja kwa moja kukaa kwenye sebule ya kishua.

“Vipi Yule dada mwingine sijui Anne hayupo?” Nelly alimuuliza Doreen.
“Unajua yule licha ya kwamba ni dada wa kazi baba anamsomesha chuo cha kompyuta kwa hiyo ameshaenda chuoni kwao mapema sana, hapa nimebaki peke yangu,” Doreen alimwambia Nelly.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo. Maoni, ushauri nicheki kupitia namba hizo hapo juu.

Leave a Comment