×

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-30

ILIPOISHIA IJUMAA:
“Hello my darling…!” nikamwambia.
“Utarudi saa ngapi?” akaniuliza swali hilo kwa jazba.
“Kwa nini unaniuliza hivyo?”
“Kwa nini nisikuulize, mimi si mke wako? Unataka akuulize nani?”
SASA ENDELEA…

Ili kumtuliza nikajidai kucheka. Nilijua ni ile mimba ndiyo iliyokuwa inamsumbua.
“Nitarudi mchana nikimaliza kazi zangu.”
“Usichelewe mimi sijisikii vizuri.”
“Una nini?”

“Nimekwambia sijisikii vizuri. Mwili wangu uko ovyoovyo.”
“Nenda hospitali.”
“Siendi, nataka wewe uwahi kurudi.”
“Sasa nikiwahi kurudi ndiyo utapona mke wangu?”
Mke wangu hakukubali kushindwa, akanijibu.
“Ndiyo nitapona!”

“Sawa nitawahi kurudi ili upone.”
“Ukichelewa tutakuja kugombana!”
“Najua katika kipindi hiki sitakuwa na amani.”

Nilipomwambia hivyo akakata simu. Pengine maneno yangu yalikuwa yamemgusa kwa sababu yalikuwa na ukweli na ukweli unauma.

Sikudhani kama yeye mwenyewe alikuwa hajielewi kuwa amebadilika. Alikuwa akijielewa na alikuwa akielewa kuwa mara kwa mara alijisikia kugombana na mimi. Hivyo nilipomwambia ‘katika kipindi hiki sitakuwa na amani’ aliuelewa ukweli huo ndipo akakata simu.

Katika kipindi kile cha ujauzito wa mke wangu ilibidi nimvumilie sana na nifikirie juu ya hali yake. Vinginevyo tungekuwa tunagombana kila siku na nyumba ningeiona moto.
Ilinipasa nirudi mapema nyumbani kwangu kama alivyoniagiza mke wangu ili kuepusha shari.

Vile alivyoniambia anajisikia vibaya, bila shaka ilikuwa ni kwa sababu ya kutoniona karibu yake.

Wakati nikiwa katika mawazo ya mke wangu, waziri mkuu akanipigia simu. Kwanza nilishtuka kupata simu yake ingawa mara kwa mara alikuwa akitupigia simu na kutupa maagizo yake.
Lakini aliponipigia siku ile nilishtuka sana. Nilihisi kushtuka kwangu huenda kulitokana na lile tukio la usiku uliopita.

Nilipopokea simu yake nilimwamkia harakaharaka. Sikusikia kama aliniitikia. Nilisikia akiniambia.
“Hebu njoo hapa ofisini kwangu.”
Sikuweza kujua huyu mheshimiwa ambaye usiku wa jana yake nilikwenda kumchawia nyumbani kwake, alikuwa ananiitia nini.

Aliniitia masuala ya kazi au aliniitia ile kadhia ya jana?
Kwa jinsi nilivyoisikia sauti yake, nilipata wazo moja tu kuwa kulikuwa na kitu kilichomghadhabisha na hakukuwa na kingine zaidi ya kile kitendo cha jana usiku. Bila shaka polisi walishanigundua na wamemwambia.

“Meshack umenisikia?” Sauti ya waziri ikasikika tena ghafla na kuyakatiza mawazo yangu.
“Ndiyo nimekusikia mheshimiwa, ninakuja.”
Mwili wote ulikuwa ukinitetemeka. Muda uleule nikainuka kwenye kiti lakini nikakumbuka kuwa nilimuahidi mke wangu kuwa ningerudi mapema nyumbani. Sikujua huko kwa waziri mkuu kungechukua muda gani.

Nikarudi tena kwenye kiti na kumpigia mke wangu.
“Hello…!” mke wangu akapokea simu.

“Nimeitwa kwa mheshimiwa waziri mkuu, sijui nitachukua muda gani huko.”
“Sasa unaniambia mimi…inanihusu nini?” mke wangu akaniuliza kwa kunishangaa.
Kwa vile akili yangu ilikuwa imeruka kutokana na kuitwa kwa waziri mkuu, nikajiuliza kama nilivyofanya kumjulisha hivyo mke wangu ilikuwa sahihi au nilikosea. Nikaona ilikuwa sahihi.

“Si ulitaka nirudi nyumbani mapema, je, kama nitachelewa huko nilikoitwa si utakasirika?” nikamuuliza.

“Kwani umeitiwa nini?”
“Sijajua bado.”
“Nenda tu, kama utachelewa utanijulisha.”
“Sawa.”

Nikakata simu na kuinuka tena. Wakati natoka mle ofisini niligeuza uso nikaitazama tena ile ofisi. Nilihisi kama nilikuwa naagana nayo. Huenda nilikuwa naitwa kufukuzwa kazi.

Nilishuka ngazi taratibu huku nikiwaza. Maafisa wa wizara yangu niliopishana nao kwenye ngazi pia walinishangaa kuniona hivyo. Nilikuwa kama mgonjwa.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.

Kama ninaitwa kufukuzwa kazi, nilijiambia, nijiandae pia kufunguliwa mashtaka ya kufanya vitendo vile vya uchawi nyumbani kwa waziri mkuu.

Lakini mbali na hilo niliendelea kujiambia, ningewezaje kukabiliana na aibu mbele ya mawaziri wenzangu na mbele ya Watanzania?
Nikajihisi kuchanganyikiwa kiasi cha kupata wazo kuwa nisiende tena kwa waziri mkuu bali nikimbie.

Leave a Comment