ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Kaikush alikuwa amepata hasira,” Faiza aliniambia.
“Ni ile hasira ya kuniacha mimi.”
“Na pia ameona ninatoroshwa.”
Baada ya kuzipita zile maiti nne hatukutembea mwendo mrefu tukaanza kuona mwanga kwa mbali.“Naona tumeukaribia mlango wa pango!” nikamwambia Faiza kwa matumaini. SASA ENDELEA…
“Utakuwa ni ule kule mbele, kuna mwanga.” Faiza akaniambia.
“Sasa tukazane tufike.”
Ingawa tulikuwa tumechoka, tulipogundua kuwa tulikuwa tumeukaribia mlango wa pango hilo tulipata nguvu.
Ikumbukwe kuwa wakati wote tulipokuwa tunatembea ndani ya pango hilo tulikuwa tunaongozwa na ule waya mweupe ambao ulikuwa umefungwa kiunoni mwa mmoja wa wale watu waliouawa.
Baada ya mtu aliyefungwa waya huo kuuawa na Kaikush, waya huo ulibaki vile vile na ndiyo tuliokuwa tunaufuata.
Kwa vile tuliongeza mwendo baada ya dakika chache tu tukawa tunauona mlango huo wa pango.
Nilitazama nyuma ili kuhakikisha usalama wetu kisha nikamwambia Faiza.
“Naona tumesalimika, yule jini amewaua wenzetu. Ameamua kutuacha.”
“Nasema ukweli kuwa sikutarajia kuwa tungeokoka,” Faiza naye alisema huku akitazama nyuma.
Tukaanza kupata hewa mwanana iliyopulizia miili yetu na kutupa faraja.
“Hewa pia imebadilika, ni tofauti na ya kule ndani,” Faiza akaniambia na kuongeza.
“Tukitoka tutahitaji muda wa kutosha wa kupunga hewa safi.”
“Sidhani kama utakapokuwa nje utashughulika na hewa. Ni kama mtu mwenye kiu, anapofika kwenye maji akinywa mara moja tu anasahau dhiki yote.”
Kutahamaki tukaona watu wanatufuata. Walikuwa polisi na askari wa jeshi la zima moto na uokoaji.
“Ndiyo nyinyi mliokuwa mnafuatiliwa humu ndani?” polisi mmoja akatuuliza.
“Ndiyo sisi,” nikamjibu.
“Wale askari waliowafuata wako wapi?”
“Kwani hakuna aliyetoka?” nikamuuliza.
“Hatujaona askari yeyote.”
“Tulikuta maiti za hao watu humu ndani. Bila shaka wote wameuawa.”
Askari hao wakatazamana kwa mshangao.
“Mkifuata huu waya hamtafika mbali mtakutana na maiti zao,” nikaendelea kuwaambia.
“Ndiyo sababu tulikuwa hatupati mawasiliano nao.”
“Ndani ya pango hili kuna jini linaloua watu. Sisi tumenusurika kibahati bahati.”
“Tuliambiwa kuna mwanamke aliyekaa ndani ya pango hili kwa miaka minne, ndiye huyu?”
“Ndiyo, ni huyu.”
Askari hao wakamtazama Faiza. Mimi nilikuwa nimeshamzoea. Bila shaka askari hao walimshangaa kutokana na nywele zake ndefu zilizokosa matunzo.
Vinyweleo vyake vya mwili pia vilikuwa vimerefuka kuliko kawaida. Isitoshe kwa sababu ya kutokutana na mwanga wa jua kwa muda mrefu, alikuwa mweupe kama Mzungu.
Askari hao walitutoa kwenye pango hilo. Tulikuta askari wengine kadhaa wakiwemo wananchi mbalimbali waliofika mapangoni hapo bila shaka baada ya kupata habari kuwa kuna watu waliopotea ndani ya pango hilo kwa siku kadhaa.
Pia kulikuwa na waandishi wa habari wa magazeti, redio na televisheni ambao walikuwa wakitupiga picha za mnato na za video.
Alikuwepo mkuu wa polisi wa wilaya ambaye alitufuata na kutuuliza maswali akitaka tumueleze nini kilichotokea ndani ya pango hilo.
Tukamueleza. Wakati huo waandishi wa habari walikuwa wametuelekeza kamera zao pamoja na kurekodi maelezo yetu kwa kutumia vinasa sauti, simu na kamera.
Wote waliokuwa wakitusikiliza walipatwa na mshangao kutokana na maelezo yetu. Maelezo ya Faiza ndiyo yaliyowashangaza zaidi.
“Umekaa ndani ya pango hili kwa miaka minne?” Mkuu wa polisi wa wilaya alimuuliza Faiza kwa mshangao.
“Ndiyo nimekaa kwa miaka minne,” Faiza alimjibu.
“Ulikuwa unakula nini?”
“Nilikuwa naletewa vyakula.”
“Na nani?”
“Na huyo jini aliyeniweka humo.”
“Itabidi baadaye utupe maelezo ya kina kwa sababu mkasa unaotueleza ni wa ajabu sana,” alisema mkuu yule wa polisi.
Kikosi kingine cha askari kikaingizwa ndani ya pango hilo kuhakikisha kama wale watu tuliosema wameuawa, wameuawa kweli. Askari hao waliambiwa kama watakuta maiti zao watoke nazo.
Baada ya mawasilino kufanyika, gari la wagonjwa la hospitali likawasili, waandishi wa habari na wananchi walikuwa wametuzonga wakituhoji maswali lakini polisi waliwaondoa.
Tukapakiwa kwenye gari la wagonjwa na kupelekwa Hospitali ya Bombo ya jijini Tanga.
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.
Well done. Lkn inabid mwape hao police mbinu ya kumshina kaikushi kbl hawajaingia pangoni.
Daaah kama mung hakupanga ufe hutokufa!