×

Nilitaka Kumuua Mwanangu Mara 3, Leo Ananisaidia!-12

Ilipoishia wiki iliyopita
Ili kujiokoa, nikajikuta nikiruka kutoka juu ya paa la nyumba huku nikipiga mayowe. Nahisi nilipoteza fahamu kabla ya kuanguka chini maana sikukumbuka kilichotokea.
Sasa endelea…

Nilikuja kuzinduka nikiwa nimelala kitandani hospitalini, mwili wote ulikuwa na maumivu na sikuweza hata kujitingisha. Kichwa chote kilikuwa kimefungwa bandeji na macho yangu hayakuweza kuona mwanga.

Nilitambua kama nilikuwa hospitali kutokana na harufu ya dawa na mpishano wa watu. Katika hali hiyo ya kutoona wala kutingisha kiungo chochote cha mwili wangu, nilikaa kama siku tatu ndipo nikaanza kufumbua macho. Kila nilipojaribu kufungua kinywa na kusema chochote sikuweza.

Daktari alipokuja siku ya tatu na kuniona nikiwa nimefumbua macho alifurahi sana, alijaribu kunisemesha, lakini sikuweza kumjibu. Aliniuliza kwa ishara kama ninasikia, nikamjibu ndiyo.

Basi akanifahamisha kuwa pale nilipo ni katika hospitali ya mkoa wa Iringa na nilipelekwa pale wiki mbili zilizopita baada ya kuanguka kutoka katika paa la nyumba na baadaye kushambuliwa na watu kwa kudhaniwa mwizi.

Nilishangaa sana, kwa sababu nikakumbuka kuwa kilichonifanya nianguke ilikuwa ni kukimbia moto uliokuwa unawaka katika nyumba ya wageni niliyofikia na hata nilipokuwa kule juu ya paa, niliwaona watu wengi wakisaidia kuzima moto.

Mshangao wangu kutokana na maelezo hayo ulionekana kumfikia yule daktari, ambaye hata hivyo hakujali. Alinihudumia na kuondoka. Nilikaa kama mwezi mzima ndipo nikaanza kupata hisia za kuinua baadhi ya viungo kama mikono na miguu. Miezi mitatu baadaye ndipo nikaanza kuzungumza.

Ingawa ilikuwa naongea kwa tabu, nilifanikiwa kumpata tena yule daktari wa siku ile na kumwuliza jinsi nilivyopelekwa pale. Aliporudia kunieleza kuwa nilianguka juu ya paa na watu kuanza kunipiga kwa kudhaniwa mwizi, ndipo nilipotaka anifafanulie.

Aliniambia kuwa inadaiwa niliiba vitu katika nyumba niliyokuwa nimepanga na nikajaribu kutoroka kwa kutoboa paa la nyumba, lakini nikateleza na wenye nyumba kufanikiwa kunidhibiti baada ya kusikia kishindo.

Kwamba kwa sababu hiyo, watu wengine walinipiga hadi polisi waliponiwahi na kuniokoa na kunipeleka pale hospitalini.Simulizi ile ilinishangaza sana maana sijawahi kuiba katika maisha yangu hata mara moja. Katika miezi yote hiyo, hakuna ndugu yangu yeyote aliyekuwa na taarifa za nilipo na bahati mbaya, sikuwa na kumbukumbu ya namba ya simu ya mtu yeyote wa karibu.

Yule daktari aliniuliza kama ninaweza kuhitaji msaada wowote, nikamweleza hali halisi ya maisha yangu, nikamweleza kuhusu mtoto wangu ambaye alikuwa hajui kilichonitokea. Mwaka mmoja nilikaa hospitalini, nikaruhusiwa kutoka.

Lakini nilikuwa siwezi kutembea, nilitakiwa kuwa na kiti cha magurudumu. Kwa msaada wa wasamaria, nikatoka na kwenda benki niliyokuwa naweka hela, nikajieleza sana na baada ya uchunguzi nikafanikiwa kupata hela, kiasi kama milioni tatu zilikuwa kwenye akaunti yangu.

Zikanisaidia kununua baiskeli na kufanya nauli. Nilifika Dar na kumfuata mke wangu, ambaye aliponiona, akasema hicho ndicho kitu nilichokuwa nakitafuta na nimekipata. Akakataa kunisaidia chochote zaidi ya kunipandisha gari nirudi kwetu Tabora.

Nikarudi Tabora na hela ile iliisha mapema sana. Nikaanza maisha ya tabu kwani hata ndugu zangu hawakunipa msaada wowote, walisema nilipokuwa na hela niliwasahau.

Bahati nzuri mtoto wangu aliendelea vizuri na masomo na alipopata kazi, akanitafuta na kuanza kunisaidia. Amenichukua na sasa ninaishi nyumbani kwake hapa Dar es Salaam, ninajuta sana kwa tamaa yangu, kwani imeharibu maisha yangu yote.

Sina uhakika kama mama yake hakuwahi kumweleza nilivyotaka kumuua, kama atakuwa anajua, nipo tayari kwa adhabu yoyote atakayonipa, lakini niseme tu ninamshukuru sana Mungu kwa yote, kama ningerudisha nyuma maisha yangu, ningekuwa mtu mwema kwa mwanangu!

Leave a Comment