×

Baba P… Baba Pili… Baba Pilima!-13

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA WIKIENDA:
Kulipokucha kabisa, ndiyo kwa mbali akapitiwa na usingizi. Mama Pilima wakati anaamka alishangaa kumwona mumewe bado kitandani wakati anavyojua, huwa anatangulia kuamka siku zote. Alimwamsha…
SHUKA NAYO MWENYEWE SASA…

“Baba Pilima…baba Pilima.”
Baba Pilima alishtuka na kumtumbulia macho mke wake…
“Mbona leo mpaka muda huu bado umelala, una nini mume wangu?”
“We mama Pilima aisee ni kiboko,” alisema baba Pilima huku akiendelea kumwangalia mkewe…

“Kwa nini mume wangu?”
“We tambua hivyo tu.”
Maneno ya baba Pilima yalimsumbua sana mke wake kiasi kwamba, muda huohuo aliwaza mambo yasiyopungua mia kidogo…

“Mh! Au amejua kitu? Lakini kama amejua kitu amejuaje? Mbona ni mambo ya siri sana?”
Alikuwa na shida ya shilingi elfu hamsini asubuhi hiyo lakini akashindwa kumwambia mume wake.

Dakika zilipita, mambo mengine yakaendelea huku baba Pilima akiamua kuingi mzigoni yeye mwenyewe.
Akiwa mjini, baba Pilima alishika simu yake akasachi namba ya baba Pili, akamwendea hewani…

“Haloo,” alipokea baba Pili…
“Mkubwa salama?” alisalimia baba Pilima…
“Salama bwana…nani?”

“Mimi naitwa Emmanuel, nimepewa namba yako na jamaa anaitwa Sudi, kuna biashara fulani alisema unaweza kunielekeza.”
“Sudi? Sudi…Sudi…Sudi…Sudi yule wa Kigamboni?”
“Sijajua anaishi Kigamboni au la!” alijibu baba Pilima…
“Wewe uko wapi?” aliuliza baba Pili…

“Kariakoo…”
“Na mimi nipo Kariakoo. Nipo hapa DDC, njoo basi tuonane ana kwa ana,” alisema baba Pili…
“Oke.”

Lakini wakati baba Pili akimsubiri baba Pilima aliamua kumpigia simu Sudi aliyemjua yeye ili amuulize vizuri kuhusu baba Pilima, lakini jamaa simu yake haikuwa hewani.
Mara, baba Pilima aliingia kwenye Ukumbi wa DDC Kariakoo na kumpigia baba Pili. Naye baba Pili alipoona simu hiyo, akaangalia geti kubwa na kumwona baba Pilima simu ikiwa sikioni huku akishangaashangaa, akamwonesha ishara ya mkono kwamba, yeye yuko pale.

Baba Pilima alitembea hadi pale, akavuta kiti ili kukaa huku akimpa mkono baba Pili na kusema…
“Naitwa Emmanuel.”
“Oke, karibu sana. mimi naitwa Mutu.”
“Oke sawa.”

Kabla baba Pilima hajaanza kusema ya uongo, simu ya mama Pilima ikaingia kwa baba Pili…
“Sore bwana Emmanuel, ngoja nipokee simu ya nyumba ndogo yangu…”
“Sawa…sawa…”
“Haloo mama Pilima…eee! una shida na shing’ ngapi? Oke…mimi nipo DDC Kariakoo, njoo basi nikupe,” alitiririka baba Pili…

“Oke…oke,” akakata simu baba Pili…
“Unajua bwana Emmanuel kuwa na nyumba ndogo ni gharama sana! Yaani huwezi kumwambia huna pesa. Si unataka kulinda uhusiano!” alisema baba Pili huku akimwangalia baba Pilima…

“Enhe, umesema umepewa namba yangu na Sudi?” aliuliza baba Pili akikaa sawasawa pale kwenye kiti huku akijiona ni mwenye bahati ya madili ya mjini.
Kabla baba Pilima hajajibu, naye simu yake iliita…

“Sore, ngoja nipokee simu ya shemeji yako…halooo…eee! Nipo Kurasini….kuna nini..? haya…sawa,” akakata…
“Unajua bwana Mutu kuwa na mke ni lazima utumie akili sana! Na ni lazima umdanganye kidogo. Haitakiwi akajua sehemu rasmi uliyopo…si mmeshajuana tabia,” alisema baba Pilima huku akimwangalia baba Pili…

“Enhe, ulitaka kujua kama namba yako nilipewa na Sudi wa Kigamboni siyo?”
“Eee!”
“Mimi sijui kama anaishi Kigamboni, ila nilikutana naye Sinza,” alisema baba Pilima na kukohoa kidogo.
Lakini sauti yake ilionekana kuwa nzito tofauti na alivyofika, huenda ni baada ya kuuona usaliti wa waziwazi wa mkewe mama Pilima…

“Oke. Lakini chamsingi nadhani si anakoishi Sudi, ni hilo unalotaka nikusaidie maana mimi nina dili na mambo mengi sana, nadili na madini, nadili na ngozi, nadili na mbao, ila tu sidili na madawa ya kulevya,” alisema baba Pili na kuangalia lango kuu.
Kwa baba Pilima hiyo ilikuwa kama kumsukuma mlevi maana alijiuliza sana aingie na gia gani kwa mwanaume huyo ili amuelewe…

“Mimi nina biashara ya madini, madini orijino kabisa. Sasa Sudi akanipa namba na kusema nikikupigia tukikutana unaweza kunisaidia.”
“Unayo hapo?”

“No! Yapo nyumbani, ila nilitaka tukutane kwanza, maana naweza kuyafuata muda wowote ule,” alisema baba Pilima. Kabla baba Pili hajasema kingine chochote, simu yake iliita…

“Sore bwana Emmanuel, nina mgeni nadhani kafika, acha nimwambie aingie huku ndani…”
“Sawasawa, aingie tu,” alikubali baba Pilima…
“Ee mama Pilima mpenzi wangu…geti kubwa..? Oke…sasa ingia ndani basi, ukiingia tu utaniona nimekaa na jamaa yangu mmoja ni mfanyabiahara,” alifunguka baba Pili.

Je, unajua nini kilitokea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda, siku ya Jumatatu.

Leave a Comment