×

Unending love-63

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila William kujua chochote na mipango ya wazazi wake kumtoa ujauzito kihalali kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yanamsumbua inafanikiwa lakini matatizo mengine ya figo yanazuka upya na kusababisha asafirishwe mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Akiwa hospitalini hapo, Anna anaanza kuwasumbua wazazi wake akishinikiza Jafet atafutwe mahali popote alipo na kupelekwa hospitalini hapo. Kazi hiyo inafanyika na hatimaye Jafet anaenda kuonana na Anna hospitali, anamuomba msamaha ili warudiane lakini Jafet anashikilia msimamo wake.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Naomba turudiane tuishi kama zamani, sijawahi kupenda kama ninavyokupenda Jafet.”

“Its too late Anna, im now dating Suleikha!” (Umechelewa sana Anna, tayari nipo kwenye uhusiano wa kimapenzi na Suleikha) alisema Jafet, kauli iliyosababisha Anna aanze kuangua kilio kwa sauti kubwa, kiasi cha kuwashtua wazazi wake waliokuwa nje, ikabidi waingie wodini kutaka kujua kulikoni.

“Kuna nini tena jamani?”
“Mama mi nampenda sana Jafet lakini mwenyewe hanitaki,” alisema Anna huku akilia kama mtoto mdogo.
“Sasa ndiyo ulie? Mbona unatutia aibu we mtoto?” alisema mama yake Anna huku akionesha kukasirishwa na kitendo kilichofanywa na mwanaye.

“Roho inauma mama, nampenda sana Jafet,” alisema Anna huku akiendelea kulia, ikabidi wazazi waitane nje kwenda kujadiliana nini cha kufanya.
“Tutafanyeje mume wangu?”

“Wewe ndiyo useme tufanye nini kwa sababu uliyataka.”
“Jamani mume wangu tutaendelea kulaumiana mpaka lini?”

“Unafikiri kama usingefanya hila za kuwatenganisha haya yote yangetokea?”
“Tulishakubaliana kuacha kulaumiana mume wangu, mbona unataka tuwe tunaenda mbele na kurudi nyuma kila mara? Tunachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kuangalia mbinu za kumsaidia mtoto wetu,” alisema mama yake Anna huku akionesha kukasirishwa na lawama alizokuwa anatupiwa na mumewe, baba yake Anna akashusha pumzi ndefu na kumtazama mkewe.

“Jafet mwenyewe inaonekana bado ana kinyongo na Anna na tayari yupo kwenye uhusiano na mtu mwingine, unafikiri itakuwaje?”
“Cha msingi tunachotaka kwa sasa, hata ikibidi kumlipa tufanye hivyo lakini aendelee kuwepo karibu yake.”

“Kukaa tu karibu yake haitoshi, si umemsikia mwenyewe anavyomlilia?”
“Sasa unafikiri tutafanyeje mume wangu? Basi jaribu kuzungumza naye wewe. Kama aliweza kukubali kutoka chuo na kuja mpaka hapa naamini atakuelewa,” alisema mama yake Anna na kumuachia mumewe mzigo huo wa kuzungumza na Jafet.

Akafungua mlango wa wodi na kumpa ishara Jafet atoke, harakaharaka akatii alichoambiwa na kutoka mpaka pale baba yake Anna alipokuwa amesimama, akamuonesha ishara kwamba amfuate. Taratibu wakawa wanatembea kwenye korido za Hospitali ya Muhimbili huku kila mmoja akiwa kimya kabisa.

Walipofika sehemu tulivu, baba yake Anna alimuomba Jafet wakae kwenye viti vilivyokuwa pembeni, jambo ambalo alilitii.

“Najua unaniheshimu ndiyo maana umekubali wito wangu wa kukutoa chuoni na kukuleta hapa,” baba yake Anna alivunja ukimya, Jafet akawa anatingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana na alichokuwa anaambiwa.

“Kwa mara nyingine nakuomba sana unisaidie jambo moja ambalo wewe unaweza kuliona kama dogo lakini lina maana kubwa kwenye maisha ya Anna,” alisema na kumtazama Jafet usoni.

“Ulipopata muda wa kuzungumza na Anna alikuwa anasemaje?”
“Alikuwa ananiomba msamaha na kutaka turudishe urafiki wetu kama zamani.”
“Nimemsikia akizungumzia kuhusu mapenzi, alikuwa anasemaje?” baba yake Anna aliuliza swali ambalo kidogo lilikuwa gumu kwa Jafet.

Japokuwa ni kweli awali wawili hao walikuwa na uhusiano wa kimapenzi, kutokana na mazingira aliyolelewa, alijitahidi sana kuishi kwa adabu ili kutoleta picha mbaya kwa wazazi wa Anna.“Sikia Jafet, kuwa huru kuzungumza na mimi kwa sababu sisi sote ni wanaume na mimi pia nimetokea hukohuko,” alisema baba yake Anna huku akimshika Jafet begani, akashusha pumzi ndefu na kuanza kumuelezea kwa undani.

“Sasa unafikiri ni jambo gani ambalo linakuzuia wewe kuwa naye kwa sasa?”
“Aliniumiza sana kiukweli na kubwa zaidi mimi tayari nimeanzisha uhusiano na msichana mwingine, Suleikha yule niliyekuja naye pale hospitalini.”

“Ok, sawa mimi nakubaliana na wewe lakini kama nilivyokwambia awali, tunahitaji sana msaada wako. Najua mwanangu akiwa karibu na wewe atatulia na hata haya matatizo yanayomsumbua yataisha haraka. Nakuomba basi hata umdanganye kwamba umemsamehe na kurudisha uhusiano wenu, tunataka kumuona akifurahi,” alisema baba yake Anna, kauli iliyomuacha Jafet njia panda.

Aliitafakari kwa kina kauli hiyo lakini wala hakupata majibu juu ya nini cha kufanya. Japokuwa Anna alikuwa amemkosea, kutokana na hali yaliyokuwa nayo, Jafet alikuwa tayari kumsamehe lakini suala la kurudisha naye uhusiano wa kimapenzi lilikuwa gumu sana kwake, hata kama ni kwa kujifanyisha kama baba yake Anna alivyoomba.

“Nitamwambia nini Suleikha? Nitafanya nini ili anielewe?”
“Wewe ni mwanaume Jafet, naamini ukikaa na kutulia utapata majibu, tafakari kwa kina, tunahitaji msaada wako, Anna anakuhitaji, vinginevyo atakufa huku tukimuona,” alisema baba yake Anna, Jafet akaomba muda wa kufikiria juu ya suala hilo.

Baada ya kumaliza mazungumzo, walirejea tena wodini ambapo walimkuta Anna akiwa na mama yake huku Suleikha akiwa anamsubiri Jafet mlangoni kama alivyomuelekeza.
“Vipi anaendeleaje?”

“Ndiyo kama hivyo unavyomuona, analia tu kama kapokea habari za msiba.”
“Anna, jikaze usilie mama, nisikilize mimi, usilie na kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Jafet kwa upole huku akimgusagusa Anna begani, kitendo kilichomfariji sana msichana huyo. Baba yake Anna akampa ishara mkewe kwamba watoke na kuwapisha wawili hao ili wazungumze, jambo ambalo alilikubali.

“Nakuomba utulize moyo wako Anna, ulichoniambia nimekuelewa na nakuomba unipe muda mfupi wa kutafakari kisha nitakujibu, wala usiwe na wasiwasi,” alisema Jafet, safari hii akionesha uungwana wa hali ya juu, jambo ambalo hata Anna hakulitegemea.

“Ahsante Jafet kwa kunipa japo nafasi ya kunifikiria, nipo chini ya miguu yako, nakuhitaji mwenzio,” alisema Anna na kutaka kuanza tena kulia lakini kijana huyo akatumia uwezo wake wa kipekee wa ushawishi aliojaliwa na Mungu, Anna akatulia, wakawa wanapiga stori za hapa na pale.

“Jafet humalizi tu? Nimechoka kusubiri nje,” Suleikha alisema huku akisukuma mlango wa wodi na kuingia ndani, akapigwa na butwaa kwa mkao aliowakuta wawili hao wamekaa.

“Jafeeet!” aliita Suleikha kwa sauti kubwa akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye gazeti la Risasi Jumamosi.

Leave a Comment