×

Chongo!-16

Ilipoishia toleo lililopita
Mtu huyo akampita na mbele kidogo akaingia ndani ya jengo hilo lenye ghorofa kumi. Alimtazama hadi alipoingia ndani ya lifti na kupanda juu, akimuacha Chongo akiwa ametahayari! Sasa endelea…

Akili ya Chongo ikawa kama imepoteza network, ilivurugika kwa sababu aliikumbuka sura ya mtu huyo, lakini hakuweza kujua alipomuona. Hata hivyo, aliamini kuwa mtu huyo atatoka nje ya jengo hili, akaamua kusubiri hadi atakapotoka, hata kama itakuwa ni usiku.

Lakini ambacho Chongo hakukifahamu ni kwamba jengo hilo lilikuwa na mlango mwingine wa kutokea chini ya ardhi, ambako kulikuwa na eneo la maegesho ya magari ambako mtu aliyemuona aliutumia kuondoka.

Ilipofika saa kumi na mbili jioni, watu wakianza kupungua katika mtaa huo wa Samora, Chongo akajiridhisha kuwa mtu wake asingeweza kumuona kwa siku ile, akajipanga kumfuatilia siku zinazokuja.

Alikwenda kila siku na kuweka viatu na bidhaa zake eneo hilo ili kumsaka mtu aliyemsahau, lakini hakuweza kumuona licha ya kujipa kazi hiyo kwa mwezi mzima. Hatimaye akaacha kufuatilia eneo hilo, akaendelea na kazi zake zingine katika kujitafutia maisha.

Maisha yake yaliendelea kubadilika hatua kwa hatua na yeye akawa miongoni mwa vijana waliokuwa wakifahamika sana katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake. Jina lake likavuma na wengi walimzoea kwa jina la Chongo badala ya Bata.

Biashara ya mitumba ilimkaa vizuri, akajiwekea akiba benki na hatimaye akapata mtaji wa kutosha kuweza kununua mwenyewe marobota ya nguo na viatu. Akapata banda zuri mtaa wa Kongo. Akajitanua vizuri kabisa.

Siku moja akiwa katika mgahawa mmoja Kariakoo akipata chakula cha mchana, akaja binti mmoja wa umri unaokaribiana na wake na kukaa pembeni yake. Wakasalimiana vizuri. Wakiwa katikati ya milo yao, msichana huyo akadai kumfananisha.

“Kuna kaka mmoja alikuwa anakaa jirani yetu, lakini ndugu yake alipata ajali akafariki, tangu wakati huo hatukumuona tena, umefanana naye sana,” alisema msichana huyo na kumvutia Chongo.

Baada ya maswali mawili matatu, wakaelewana. Huyo aliishi karibu na Noel, yule kijana aliyejitolea kuishi na Bata baada ya kumuokoa kutoka katika hatari ya kufa. Chongo alifurahi sana!

Walizungumza mambo mengi sana yaliyopita, msichana huyo akimfahamisha Chongo kilichoendelea baada ya msiba, kwamba kulitokea ugomvi mkubwa miongoni mwa ndugu zake ambao waligombea mali za marehemu.

Mwisho wa siku, wakaenda hadi kwenye eneo la biashara la Chongo ambalo lilimvutia sana msichana huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Elina. Wakakaa pamoja hadi jioni biashara ilipofungwa, wakaondoka pamoja hadi Sinza alikokuwa akiishi Chongo.

Siku hiyo waliachana majira ya saa tatu wakati Elina aliporudi nyumbani kwao, lakini wakiwa wamejenga urafiki mkubwa kwa muda huo mfupi. Elina alionekana kuvutiwa zaidi na kijana huyo, akivuta kumbukumbu zake nyuma jinsi alivyomuonea huruma baada ya kupata simulizi ya kilichomtokea.

Aliporudi nyumbani kwao, aliwasimulia ndugu zake kuhusu kukutana kwake na mtu ambaye hawakufahamu alipo tangu ulipotokea msiba ule mkubwa. Kila mmoja alifurahi kusikia habari hizo mpya, hasa walipoambiwa kuwa alikuwa ni mtu anayejitegemea, tena akifanya biashara nzuri tu ya mitumba.

Mawasiliano baina ya wawili hao yalikuwa makubwa mno, wakitumiana ujumbe karibu kila wakati, wakipigiana simu kusalimiana. Ndani ya wiki moja, wakawa wameshaanzisha uhusiano wa kimapenzi na kila mmoja akavutiwa isivyo kawaida na mwenzake.

Baada ya kama mwezi mmoja hivi, wikiendi moja Elina alikwenda nyumbani kwa Bata akiwa ameongozana na msichana mwingine rafiki yake. Walizungumza mambo yao mengi ya kimaisha, kila mmoja akichangia kilichojadiliwa.

Ghafla, msichana huyo, ambaye aliitwa Jully alibadili aina ya mazungumzo pale alipomwambia Bata kuwa yeye alikuwa akimfahamu sana, tena tangu akiwa mtoto.
“Ulinifahamia wapi?”

“Shule, wewe tulisoma wote primary,” msichana huyo alitoa jibu ambalo lilimchanganya Bata, kwani hakukumbuka kama aliwahi kwenda shule.Je, msichana huyo ni nani na nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Leave a Comment