×

Julio atamba kumfukuzisha kazi Kerr

JulioKihwelu.jpg Kocha wa timu ya Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

Said Ally,

Dar es Salaam

WAKATI taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Simba zikidai kumpa mechi nne tu kocha wao, Muingereza, Dylan Kerr kuhakikisha anapata matokeo ya ushindi, kocha wa timu ya Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ametamba kuwa ataanza kumfungisha virago Mzungu huyo kwa kukifunga kikosi chake.

kochaDylanKerr.jpg Muingereza, Dylan Kerr.

Simba na Mwadui zinatarajia kukutana kesho Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ambapo Simba wataingia na kumbukumbu mbaya ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wao uliopita dhidi ya Toto Africans.

Julio, kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, ameliambia Championi Ijumaa kuwa, tayari ameshaandaa silaha zake za ushindi katika mchezo huo ambapo ataingia ili kulipiza kisasi kutokana na vitendo vya kutimuliwa alivyowahi kufanyiwa na viongozi wa timu hiyo.

“Nawaambia kabisa Simba tupo tayari kuwapa kichapo hiyo Jumamosi, maana wachezaji wangu wana uchu mkubwa wa kuona tunaifunga Simba na kuwaonyesha sisi tuna kiwango zaidi ya kikosi chao.

“Lakini pia mimi mwenyewe nitawaonyesha kuwa walinitimua kwa fitna tu, ingawa nina uwezo mkubwa wa kuifundisha timu hiyo kwa kukiongoza kikosi changu vema kabisa na kumfunga huyo Mzungu wao,” alijinadi Julio ambaye timu yake ina pointi 21 wakati Simba ina pointi 23.

 

Leave a Comment