×

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa 37

ILIPOISHIA:

Baada ya Destiny kumaliza masomo yake ya uandishi wa habari katika Chuo cha Nothestern kilichopo huko Marekani, alikwenda kujiunga na Kampuni la Habari la Wend Production kwa ajili ya kupata uzoefu ambako huko alikabidhiwa kwa mwandishi wa habari mzoefu Criss Jacquiler.
Tambaa nayo…

KUTOKANA na mafunzo aliyoyapata kutoka kwa Criss Jacquiler, Destiny alijikuta akiipenda mno kazi ya uandishi wa habari ambapo baada ya muda wake wa masomo kumalizika alitakiwa kuondoka Marekani na kurudi Afrika kwa ajili ya kuitimiza azma yake ya kumbadilisha Mtima.
“Nitakukumbuka sana Criss.” alimwambia Criss Jacquiler siku anaondoka.
“Mimi pia Destiny.”

“Mungu akubariki kwa yote uliyonitendea.”“Akuongoze pia huko uendako.”
Ilikuwa ni siku ya huzuni kwa wawili hao, lakini ilikuwa ni lazima watengane, walikumbatiana huku machozi yakiwabubujika pia Chriss Jacquiler alimuimbia Destiny wimbo wa Chriss Brown uitwao Goodbye, usiku wa siku hiyo Destiny alisafiri kurudi Afrika tayari kuzianza harakati zake.

* * *
Wakiwa katika hatari ya kupigwa risasi na wanajeshi wa mpakani mwa Kenya na Somalia, Mtima na Abdulrahman walizidi kuyachapa maji ya Mto Afmadow huku mikononi wakiwa na silaha zao, waliendelea kuogelea hadi walipofika nchi kavu, upande wa pili wa mto huo ambako risasi zilizidi kurindima.

Hali ikawa tete kwa vijana hao ambao hawakupenda kufa kikondoo, wakaanza kukimbia kwa mtindo wa zigizaga kuelekea kwenye pori lililokuwa jirani na mto huo huku wakijibu mashambulizi, Mtima akizidi kukimbia mara alishtukia risasi ikimpata kwenye bega la mkono wake wa kushoto, akaweweseka huku akigumia maumivu kisha akaanguka chini.

Abdulrahman hakupenda kuona rafiki yake anafia kwenye uwanja wa mapambano, alichokifanya alianza kujibu mashambulizi akiwa anamlinda hadi pale Mtima alipokusanya nguvu, akainuka, kwa ujasiri mkubwa wakakimbia na kutokomea kwenye pori hilo huku risasi zikiwafuata nyuma bila mafanikio ya kuwapata.

Hiyo ikawa ponapona yao, lakini kutokana na mashambulizi pamoja na misukosuko waliyokutana nayo kweye mapambano hayo walitambua wakati huo vyombo vya usalama vilipania kuwaangamiza.

Walisisitizana kuwa makini, baada ya Mtima kupata unafuu katika jeraha lake la kupigwa risasi walipanga mipango ya kwenda kushambulia katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi kwenye kituo kikubwa cha kulea watoto wadogo waliozaliwa na matatizo mbalimbali ya ulemavu kiitwacho Jerusalemu Disabled Children Cares (JDCC), kilichokuwa kinatunza zaidi ya watoto elfu moja.

* * *
Kama kawaida ndani ya kituo hicho cha JDCC shughuli mbalimbali zilikuwa zinaendelea, wafanyakazi wakiwa bize kwa kuwahudumia watoto, wazazi pia walizidi kupishana wakiingia na kutoka kuwajulia hali watoto wao.

Kwa kutumia gari walilokodi Discover 2002, Mtima na Abdulrahman walivamia katika jengo la kituo hicho kwa kushitukiza, walinzi wakiwa hawana hili wala lile wakaanza kuwaua, baada ya kuhakikisha walinzi wote walikuwa wamepoteza maisha waliingia ndani na kuanza kuua watoto wasio na hatia, wazazi waliokwenda kuwajulia hali pamoja na walimu wao.

Vilio vikatapakaa kila kona, kila mmoja akikimbia huku na huko kuiokoa roho yake, lakini ukweli ni kwamba juhudi hizo za watoto na watu wengi hazikuweza kusaidia kitu, zaidi ya roho 300 za watu wasio na hatia ziliteketea.

Wakiwa wanaendelea kufanya mauaji katika kituo hicho, Mtima na Abdulrahman walivisikia ving’ora vya magari ya jeshi la polisi kwa mbali vikijongea eneo hilo, bila kupoteza muda, vijana hao walilidandia gari lao, Mtima akashika usukani kisha wakapotea eneo hilo.

Ndani ya muda mfupi tayari magari zaidi ya kumi yaliyosheheni askari polisi yalifika katika kituo cha JDCC, lakini tayari walikuwa wamechelewa, kina Mtima walikuwa wamekwisha tokomea kusikojulikana, walichoambulia ilikuwa ni miili ya marehemu na majeruhi waliozagaa kila kona.

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave a Comment