JUHUDI za kumpata Catarina ili apelekwe wodini kuonana na Kevin zimegonga mwamba, binti huyo ni mgonjwa mahututi, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili chumba cha wagonjwa mahututi. Baba yake Kevin ameshtuliwa sana na habari hizi kwani mara ya mwisho alipomwona Catarina alikuwa mzima wa afya, iweje awe mahututi?
Katika mazungumzo na baba yake anaelezewa jinsi tatizo hilo lilivyotokea, ingawa mwisho wa siku hakutaja aina ya ugonjwa uliokuwa ukimsumbua, kwa pamoja wakaondoka nyumbani hadi hospitalini kwa lengo la kumwona Catarina, hali aliyomkuta nayo ilimsikitisha sana mzee Mdoe, Catarina alikuwa amelala kitandani akiwa amezungukwa na mashine, pamoja na kwamba damu ilikuwa ikidondoka kuingia kwenye mishipa yake, mwili wake ulionekana ‘mweupe’ sababu ya upungufu mkubwa wa damu.
Wakiendelea na maongezi likaingia kundi la madaktari na wauguzi, hapo ndipo mzee Mdoe akalazimika kuaga ili aende chumbani alikolazwa mwanaye, moyo wake ukiwa umejawa na huzuni nyingi.
Baada ya kuondoka ndipo daktari aliyeonekana kiongozi wa watu walioingia wodini alipowaambia wazazi wa Catarina kuwa mtoto wao alikuwa amepatwa na aina ya saratani ya damu iitwayo Acute Myeloid Leukaemia, zilikuwa ni habari mbaya mno kwao, mama yake Catarina akaporomoka chini kama mzigo!
SONGA NAYO…
KUNDI la madaktari likamuwahi mama yake Catarina na kumnyanyua hadi kitandani ambako alilazwa na kitanda kunyanyuliwa miguuni ili damu nyingi ielekee kwenye ubongo, alipatwa na mshtuko sababu ya taarifa aliyopokea, Dk. Robert Rwezaura akasogea karibu na kuanza kumpima kwa kutumia kifaa kitwacho Stethoscope ambacho hutumika kuusikiliza moyo.
“It is just a neurogenic shock, keep elevating the lower side of the bed, she will be back to normal.” (Ni mshtuko tu uliotokana na habari tuliyompa, endeleeni kunyanyua kitanda sehemu ya chini, atarejea katika hali ya kawaida!) aliongea Dk. Rwezaura.
Dakika ishirini baadaye mama alizinduka na kukuta kitanda chake kimezungukwa na madaktari pamoja na mumewe, akaanza kulia akimlilia mwanaye maana alifahamu saratani ulikuwa ni ugonjwa usiopona, hivyo mwanaye Catarina angekufa, fikra hizo peke yake kwa mwanaye pekee zilimuumiza mno, hakuwa tayari kabisa kumpoteza Catarina.
“Bora nife mimi!”
“Nani amekuambia Catarina anakufa?”
“Najua saratani haiponi!”
“Hayo ni maneno ya zamani, pumzika tu mama, tuachie sisi na Mungu tuone kinachoweza kufanyika, sayansi imebadilika sana hivi sasa!” Dk. Rwezaura alimalizia.
Akamtaka mzee David aambatane naye ofisini kwake ambako wangeongea vizuri juu ya tatizo la mtoto wake, hicho ndicho kilichotokea, Dk. Rwezaura na kundi lote la madaktari pamoja na mzee David wakaongozana hadi ofisini kwake mita kama hamsini hivi kutoka chumba cha wagonjwa mahututi.
“Mwanao ana Acute Myeloid Leukaemia!”
“Ni nini hiyo daktari?”
“Ni Saratani ya Uboho au Bone Marrow kwa Kiingereza, sehemu ya mfupa ambayo hutengeneza chembechembe nyeupe za damu au kwa Kiingereza White Blood Cells, badala ya kutengeneza chembechembe imara hutengenezwa ambazo ni dhaifu na laini ambazo hufa na kujaa kwenye Uboho, jambo ambalo husababisha hata chembechembe nyekundu za damu zisitengenezwe na kusababisha mgonjwa kupatwa na upungufu wa damu wa mara kwa mara pamoja na kuugua magonjwa mengi kwa kukosa kinga, si unajua kwamba chembechembe nyeupe za damu ndiyo askari wa mwili?” Dk. Rwezaura alimuuliza mzee David.
“Ndiyo!”
“Mwanao hana askari wa kulinda mwili wake sababu ya hii saratani, hii inamfanya kuugua mara kwa mara magonjwa yanayosababishwa na bakteria, pili damu yake inapungua kwa sababu chembechembe nyekundu hazitengenezwi, hilo ndilo tatizo linalomsumbua mwanao, majibu yameonyesha hivyo!”
“Inasababishwa na nini daktari?”
“Hakuna anayeweza kuelezea vizuri chanzo cha saratani, madaktari tunatumia neno Idiopathic, ingawa yako mambo yanayoweza kuchochea mtu akapata saratani kama matumizi ya kemikali, ulaji wa vyakula kama nyama, kukosa mazoezi, matumizi ya sigara nk.”
“Kuna tiba au ndiyo mwanangu atakufa?”
“Zipo tiba za aina mbili, ya kwanza ni ya kutumia mionzi na ya pili ni ya kupandikiza uboho mwingine kwenye mifupa yake, hii kwa kitalaam tunaiita BMT, yaani Bone Marrow Transplant, akishapandikiziwa uboho mwingine tatizo hufika mwisho na chembechembe huanza kutengenezwa kama kawaida!”
“Huu uboho wa kumpandikizia unapatikana wapi?”
“Lazima apatikane mtu wa kuutoa, yaani kwa Kiingereza anaitwa Donor, huyu atajitolea uboho wake ili mgonjwa awekewe!”
“Nipo tayari kuutoa wa kwangu hata kama mimi nitakufa baada ya hapo.”
“Hauwezi kufa!”
“Nipo tayari, ikishindikana mimi mama yake atatoa ili mradi tu mtoto wetu apone!”
“Kitakachofanyika ni kumpeleka Hospitali ya Saratani ya Ocean Road, huko ndiko wataamua nini cha kufanya!”
“Hakuna tatizo.”
“Basi yalikuwa ni hayo tu, nitafanya taratibu za kuwasiliana na Hospitali ya Ocean Road na kuandika barua ili kesho mhamishiwe huko.”
“Nashukuru sana.”
Mzee David aliondoka ofisini kwa DK. Rwezaura na kurejea chumba cha wagonjwa mahututi ambako alimwelezea mke wake kila kitu, kwamba Catarina alikuwa na nafasi ya kupona kama angetibiwa ipasavyo, sababu saratani yake ndiyo ilikuwa katika hatua za mwanzo, mama yake Catarina alifurahi mno na kuahidi kama alivyosema mume wake kwamba alikuwa tayari yeye mwenyewe kutoa uboho wake hata kama ingemgharimu maisha yake lakini Catarina arejee katika hali yake ya kawaida.
Kilichofanyika hapo ni maandalizi ya Catarina kuhamishwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenda Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, taratibu zilipokamilika siku iliyofuata asubuhi mgonjwa alipakiwa juu ya machela yenye matairi kupelekwa nje ambako gari la wagonjwa lilikuwa likisubiri.
***
Mzee Mdoe alipofika chumbani kwa Kevin alitafuta maneno mazuri ya kumweleza mtoto wake ili aelewe lakini haikuwezekana, Kevin alihisi baba yake alikuwa akimdanganya, akaanza kulia kwa nguvu akishinikiza Catarina aletwe! Wakajaribu kadiri ya uwezo wao wote kumtuliza lakini haikuwezekana, mchana kutwa alishinda akilia na ndivyo ilivyokuwa usiku mzima bila kula hata chakula.
Dk. James Mabula aliyekuwa akimshughulikia alipopewa taarifa hizo, haraka sana alikwenda chumbani kufanya mazungumzo na Kevin pamoja na wazazi wake, bado aliendelea kushinikiza Catarina aletwe, Dk. James na mzee Mdoe walipopelekana pembeni na kujadiliana walifikia uamuzi kwamba Kevin achukuliwe kwa kutumia kiti cha matairi mpaka chumba cha wagonjwa mahututi alikokuwa amelazwa Catarina ili akamwone.
“Kevin!” Daktari aliita.
“Naam.”
“Ukweli ni kwamba Catarina ni mgonjwa na amelazwa hapahapa Muhimbili!”
“Ndiyo.”
“Tulikuwa tunahofia kukueleza habari hizi lakini sasa tumeamua tukupeleke wodini alikolazwa ukamwone, hawezi hata kuongea.”
“Naomba nikamwone hivyohivyo alivyo!”
Je, nini kitaendelea? Watamkuta? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.