×

Wapendanao wanapaswa kuzitumiaje Krismasi na Mwaka Mpya?

happycouplemain.jpgNianze kwa kuwatakia heri ya Krismasi na Mwaka Mpya wasomaji wa safu hii. Najua kabla ya mwaka huu kufika, kila mtu alijiwekea malengo yake. Kuna ambao walipanga kuoana, kuchumbiana au kutambulishana. Mmetimiza ahadi yenu?

Katika makundi hayo yote, hapo waliofanikiwa kufikia hatua waliyojipangia lakini pia wengine hawakuweza kufikia malengo yao. Penzi sahihi ni lile lenye malengo. Mkiishi katika uhusiano ambao kila mmoja wenu anawaza lake, hakuna maisha.

Kwenye uhusiano lazima kuwe na malengo. Kwamba mmekutana ili muweze kutengeneza uhusiano wa aina gani. Wa muda mrefu au muda mfupi. Mnataka kuishia ‘uboyfriend na ugirlfriend’ au mnataka kuwa wachumba na baadaye ndoa?

Kwa wale ambao hawakutimiza malengo yao, katika kipindi hiki cha kuukamilisha mwaka huu 2015, ni kipindi cha kujitathmini. Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya ni nzuri kusherehekea lakini ndani ya sherehe hizo, mnapaswa kutafakari na mjijue mnakoelekea.

Tafuteni eneo tulivu ambalo litawawezesha kunywa, kula na kufurahi lakini kupata utulivu wa kujadili penzi lenu. Kwa kutumia lugha rafiki, lugha ya kuchombezana, kumbushaneni kule mlikotoka na ahadi mlizojiwekea kwa mwaka 2015.

Mkishakizungumza kile mlichopanga, jiulizeni nini kilikwamisha mshindwe kutimiza azma hiyo. Mkipata sababu, hata kama imetokana na tatizo la mmoja wenu, usiwe wakati wa kulaumiana. Pangeni mikakati itakayowawezesha kufanikisha jambo lenu kwa mwaka ujao.

Mkishapanga kufanikisha jambo hilo mwakani, wekeni misingi thabiti ya kulifanikisha. Wekeni mipango ya muda mrefu na hata muda mfupi. Mfano kama jambo lenu linahitaji hatua za kupiga, jadilini namna ya kuzipiga hizo hatua na kujipangia muda wa kulitekeleza.

Lazima mjue kama suala ni uchumba ili mfikie kwenye hatua ya kuchumbiana, mnapaswa kufanya nini? Kama ni kwenda kujitambulisha kwa pande zote mbili, mnapaswa kuanza na hatua gani? Mpo tayari kwa suala hilo? Hatua gani za awali mnapaswa kuzifanya kabla hamjafikia hatua hiyo? Mkipata jibu, anzeni utekelezaji.

Kama mnataka kufunga ndoa, je mmeshapanga namna ya kufanikisha tendo hilo. Mmeshawafahamisha wazazi wa pande zote mbili? Suala hilo mtalifanikisha ndani ya kipindi gani? Mwaka mmoja au miwili kama si mitatu?

Mkipata jibu ya kipindi husika, je mna kipato sahihi cha kuweza kufanikisha aina ya ndoa ambayo mnaitaka? Msilazimishe ndoa ya kifahari kama uwezo wenu ni mdogo. Ni vyema kama mnataka huo ufahari, mjipange kwanza nyinyi wenyewe kwa kujiimarisha kiuchumi ndipo mpange kuoana.

Kama hamhitaji mbwembwe, andaeni mikakati ya kufunga ndoa ya wastani ambayo mnaitaka. Itakayokuwa na bajeti mnayoimudu na wageni waalikwa mtakaoweza kuwahudumia.

Ndoa ni ya watu wawili. Suala la kuwashirikisha marafiki, kamati ni la ziada tu. Mnapaswa nyinyi wenyewe kuwa tayari na sehemu ya kipato kinachoendana na aina ya ndoa ambayo mnataka kuifunga. Msiwasumbue watu kwa michango wakati nao hawana uwezo huo. Utawalaumu bure kumbe wenzako hawana kitu na wana majukumu mengine.

Nyie muwe na mamlaka na ndoa yenu inayotokana na kipato chenu.Msiingie kwenye ndoa kwa kufuata mkumbo. Kufuata wenzenu wameoana basi na nyinyi muoane. Lazima muwe na malengo ya kweli, mpange namna ya kuyafanikisha kwa pamoja.

Hayo yote yanatimia kama pia wapendanao mnawaza jambo moja. Mna mipango nya kufika pamoja. Kama ukiona uliye naye hana mikakati uliyonayo na amekuwa akikukwamisha kila mwaka, huna sababu ya kuendelea naye.

Ni vyema ukasubiri mpaka pale utakapompata ambaye atakuwa sahihi kwako na mtapanga maisha yenu.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri ya kusisimua!

Leave a Comment