×

Joto la Mapenzi 52

ILIPOISHIA:

“Ha! Shemu, karibu.”
“Asante.”
“Mbona usiku?”

“Kuna ubaya mtu kuja kwao?”
“Hakuna ubaya, karibuni,” wakati huo jicho lake lilitua kwa Ambe aliyekuwa nyuma. Kama mwendawazimu alikurupuka na kwenda kumvamia.
“Wawooo bebiii.”SASA ENDELEA…

Sauti yake ilimshtua mama yake aliyekuwa chumbani hajalala na kutoka sebuleni naye na kushangaa ugeni wa watu wenye kanzu na mmoja akiwa mkwewe.
“Jamani karibuni.”
“Asante.”
“Naona ugeni wa usiku?”
“Ni kweli mama.”

“Haya karibuni, Koleta hebu muachie mwenzako ukaribishe wageni.“Mama wee wakaribishe, mi simuachi mpenzi wangu,” Koleta alisema akiwa bado amemlalia kifuani Ambe.“Haya jamani karibuni.”

“Asante,” wageni aliitikia kwa pamoja na kukaa kwenye makochi.“Karibu baba.”
“Asante mama, samahani kwa kukuvamieni usiku,” alisema mzee aliyechaguliwa kuzungumza.“Bila samahani hapa kwenu mna haki ya kuja muda wowote,” mama Koleta alionesha uungwana wa hali ya juu.

“Asante sana mama, naomba nizungumze mara moja na mwenzangu,” Ambe aliomba kuzungumza pembeni na Koleta.“Hakuna tatizo baba.”Ambe na Koleta walisogea pembeni kuteta:

“Mmh! Mpenzi wangu leo umenijia kivingine kama unataka tufunge ndoa ya mkeka nini?”
“Ni kweli hii ni ndoa ya mkeka.”
“Sasa utanioaje si nasikia mpaka usilimishwe uwe Muislamu?”

“Kikosi kilichokuja kimekuja kamili, hii ni sapraizi kwako na familia yako, sasa hivi unasilimishwa na kufunga ndoa baada ya ndoa tutaondoka nchini mimi na wewe na mtoto wetu kwa miaka miwili, tukirudi tutaishi maisha ya kawaida bila kujificha.”
“Mama anajua?”

“Wewe nenda kamwambie ukirudi njoo na jibu tumalize kazi, baada ya ndoa nitaondoka, baada ya wiki tutaondoka kwenda Afrika Kusini kuishi kuepuka longolongo.”

“Hakuna tatizo ngoja nikazungumze na mama japo najua hawezi kuwa na neno.”Koleta alirudi na kumweleza mama yake waliyoshauriana na mwenzake, mama yake naye hakuwa na pingamizi zaidi ya kuwapa baraka zote.

“Wanangu siwezi kuwaingilia kwa lolote mtakaloamua, nimeamini kila mmoja alikuwa na mapenzi ya kweli na mwenzake.

Ruksa kubadili dini na kuolewa na chochote kizuri ruksa.” Kabla ya yote Ambe aliwatambulisha wageni wake akiwemo mtu wa kumsilimisha na shehe wa kufungisha ndoa usiku ule. Mama Koleta aliwakaribisha kwa furaha na bashasha. Baada ya baraka za mama, Koleta alisilimishwa kuchagua jina la Leila kisha ndoa ilifungwa.

Baada ya ndoa Ambe na wageni wake waliondoka usiku uleule. Baada ya kuondoka Koleta alikuwa mwenye furaha kuliko siku yoyote katika maisha yake.
“Mama siamini kama nimeweza kuwa mke wa Ambe ilikuwa ndoto leo imekuwa kweli,” alisema huku akishika mikono kifuani.

“Kwa nini mwanangu?”
“Mama nimepitia mitihani mingi mpaka leo imekuwa hivi,” Koleta au Leila alisema huku akitazama pete ya gharama kidoleni mwake, aliibusu na kushukuru Mungu .
’Nimeamini mwenye subira hupewa alichokisubiri.”

“Lakini mbona ndoa yenyewe haina chereko?” Mama yake aliuliza.
“Mama sherehe ni mbwembwe muhimu ni hiki kilichofanyika, hata watu wengine hufunga ndoa kanisani na wapambe wao tu.”

“Lakini tufanye sherehe baadaye.”
“Hata sisi tutafanya yetu tena kubwa sana.”
“Hakuna tatizo.”
“Hongera dada,” Ester alimpongeza Leila kwa kufunga ndoa.
“Asante mdogo wangu.”

“Hongera mama,” Junior naye alimpongeza mama yake.
“Asante mwanangu nina imani Mungu amepokea kilio changu, muda mrefu utaishi nyumba moja na wazazi wako wote.”

“Leila mwanangu umepata mwanaume mwenye mapenzi ya dhati kwako.”
“Hata mimi mama anajua jinsi gani nilivyokuwa nampenda.”
“Basi mmepatana.”

“Mama nimefurahi sana, furaha yangu haina kipimo.”
“Na kuondoka lini?”
“Baada ya wiki, nimeambiwa nijiandae.”
“Mmeshapata pa kwenda kukaa?”

“Anajua mwenyewe.”
“Mmh! Na mimi nitabaki na nani miaka miwili mingi.”
“Baada ya kutulia wote tutahamia huko.”
“Mmh! Hapo kidogo sawa.” Baada ya mazungumzo ya usiku mzima Leila alikwenda chumbani kwake kulala muda wote aliiangalia pete aliyovishwa na mume wake. Aliibusu na kusema:

“Asante mume wangu nitakupenda milele,” usingizi nao ulimchukua.

* * *
Wiki moja baada ya mipango yote kwenda kama ilivyopangwa Ambe alimchukua mkewe pamoja na mwanaye na kwenda kuishi Afrika Kusini. Baada ya kufika waliishi maisha ya mfalme na malkia kila mmoja alionesha mapenzi mazito kwa mwenzake. Wakiwa wanapunga upepo nje ya nyumba waliyonunua Leila alitaka kujua nani aliyemuua baba yake.

“Eti mpenzi nani alimuua baba yangu?” alimuuliza huku akimchezea nywele za kifuani ‘garden love’.
“Kwa nini unaniuliza hivyo?”

“Nilitaka kumpa zawadi.”
“Zawadi kwa ajili ya kuuawa baba yako?”
“Ndiyo mpenzi.”
“Ukiishampa zawadi?”
“Basi nitakuwa nimetimiza ahadi yangu.”
“Simjui.”

“Muongo niambie ukweli mpenzi wangu.”
“Sijui,” Ambe alimficha kwa kuamini huenda akajenga chuki na mkewe.
“Au wewe?”
“Umetumwa?”

“Na nani?”
“Nakuuliza umetumwa kunipeleleza?”
“Siyo hivyo mpenzi nilikuwa nakuuliza tu.”
“Unauliza nini, nimekujibu sijui bado unaning’ang’ania, haya nimemuua mimi wapigie simu polisi waje wanikamate au kesho nipande ndege nikawaeleze mimi ndiye Ambe ninayetafutwa kwa mauaji na kutoroka gerezani na pia nimemuua baba yako mzee Mtoe,” Ambe alisema kwa sauti ya ukali. “Mbona umekuwa mkali?”

“Sikiliza kukuoa siyo sababu ya kunikosea adabu, naweza kupotea na usinione tena katika maisha yako. Kwani mimi bila wewe nitapungukiwa nini? Hasa baada ya kukugundua wewe ni msaliti huna mapenzi ya kweli kwangu.”

“Ambeee,” Leila alibakia mdomo wazi asijue afanye nini.
“Usijifanye kushangaa mnafiki mkubwa, haya nenda kawaeleze mimi ndiye niliyemuua baba yako.”

“Samahani Ambe sikuwa na maana hiyo,” Leila ilibidi ajisalimishe.“Nipe namba ya mkuu wa polisi aliyekutuma nimweleze kuwa nipo huku na sehemu gani ili atume polisi wa huku waje wanikamate.” Ambe ambaye alitegemea kupata maneno matamu baada ya safari ndefu ya mateso ya kukatisha tamaa. Aliamini mpenzi wake hana mapenzi tena na yeye hata mwaliko aliomualika ulikuwa wa uongo ili kumkamatisha.
Je, nini kilifuatia? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo.

Leave a Comment