×

Julio: Ni fedheha kutoa sare na Simba

JulioKocha wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

Johnson James, Shinyanga
KOCHA wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amesema ni fedheha kwa timu yake kutoka sare ya bao 1-1 na Simba, kwani wapinzani wao wana idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni kuliko yeye.

Mwadui ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, juzi Jumamosi ilitoka sare ya bao 1-1 na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Julio alisema kuwa hakutegemea kupata sare katika mchezo huo kutokana na kikosi cha Simba kilivyo na wachezaji wengi kutoka nje ya nchi.

“Niseme ukweli sikutegemea kupata sare katika mchezo huu kwani nilitegemea kufungwa kutokana na Simba inavyocheza soka lakini kutokana na mimi kutoa sare katika mchezo huu ni aibu kwao,” alisema.

Julio alisema Simba haikutakiwa kutoa sare bali ilitakiwa kuondoka na pointi zote tatu katika mchezo huo. “Simba ina wachezaji wengi profesheno lakini hawajui kuwatumia, hivyo wanatakiwa kubadilika kwani mwenendo wa timu yao siyo mzuri.”

Hata hivyo, kabla ya mchezo huo Julio ambaye amewahi kuichezea na kuifundisha Simba, alisema timu yake ingeweza kuifunga Simba ambayo sasa haichezi soka la kuvutia.

Wachezaji wa kigeni waliopo katika kikosi cha Simba ni kipa Vincent Agban wa Ivory Coast, beki Juuko Murshid, straika Hamis Kiiza na kiungo mshambuliaji Brian Majwega wote raia wa Uganda. Wengine ni Emil Nimubona wa Burundi, Justice Majabvi wa Zimbabwe na Paul Kiongera wa Kenya.

Leave a Comment