ILIPOISHIA:
“Samahani Ambe sikuwa na maana hiyo,” Leila ilibidi ajisalimishe. “Nipe namba ya mkuu wa polisi aliyekutuma nimweleze kuwa nipo huku na sehemu gani ili atume polisi wa huku waje wanikamate.”
Ambe ambaye alitegemea kupata maneno matamu baada ya safari ndefu ya mateso ya kukatisha tamaa. Aliamini mpenzi wake hana mapenzi tena na yeye hata mwaliko aliomualika ulikuwa wa uongo ili kumkamatisha.SASA ENDELEA…
“Ambe…Ambe.. ni maneno gani hayo mpenzi wangu? Unayoniambia, kosa langu nini kukuuliza. Wewe ni mpenzi wangu, tumetoka wapi? Hivi yote ninayoyafanya kwako bado huoni jinsi gani ninavyokupenda?
“Nina muda gani nimekusubiri bila kujua upo wapi, nimekuwa muaminifu siku zote za maisha yangu kwa ajili ya mapenzi yako kwangu. Ambe umenikuta kama msichana bikira kwa uaminifu wangu kwako. Ni wewe peke yako unayeujua mwili wangu nimekuwa muwazi na mkweli kwako sijawahi kukufikiria jambo baya katika maisha yangu.
“Kauli yako imekuwa sawa na kuupasua moyo wangu kwa kisu butu tena bila ganzi ni maumivu kiasi gani? Maneno yako ni baridi kali katika damu yangu inayoweza kuigandisha na kusimamisha mapigo ya moyo, kwa maneno yako nayaona mauti mbele yangu.
“Nakuomba kitu kimoja kama nitakufa basi nakuomba unilelee mwanangu pia elewa ni mwanamke pekee niliyekupenda mapenzi ya kweli toka moyoni. Kama moyo ungekuwa unafunguliwa na kuyaona anayowaza mwanadamu ungeona, kama utakuta kuna baya lolote basi Mungu anigeuze kiumbe cha ajabu kisicho na thamani chini ya jua.”
Hebu angalia jinsi gani nilivyokuenzi baada ya kuelezwa umekufa, mtoto wako alikuwa amepewa jina la marehemu baba lakini nilipigana kiume kuhakikisha jina lako alipotei maishani mwangu hata mtoto wa kiume wa mwanao kama ningekuwa hai mpaka atakapopata mtoto ningemwita jina lako.”
Jina lako limekuwa farijiko ndani ya moyo wangu, kila ninaposikia mwanangu anaitwa jina lako huwa kama nakuona mbele ya macho yangu.
Kosa langu nini kukuuliza kuhusu kumuua baba? Mbona nilipanga kumuua tena kwa mkono wangu kwa kutamka mbele yako.
”Hata wewe uliniahidi kama baba angekwenda kinyume ungemuua, hivi ni mapenzi gani niliyokuonesha, nimeiba silaha za baba na kukupa wewe, nimekuwezesha kwa kila kitu. Hebu nieleze kosa langu nini? Au kunikuta nimelala pembeni ya kitanda cha baba ndiyo uniite msaliti?
“Kwa taarifa yako siku ile ndiyo nilipanga kumuua baba, lakini nilihofia kauli yangu niliyoitoa kwa mama na Ester ya kumuua baba. Huwezi kuamini siku ya kifo cha baba nilimrudisha nyumbani mama ili nimuue na kugundua nimefanya kosa hivyo kujipanga kumuua kwa njia nyingine.
“Bahati nzuri usiku wa siku ile baba aliuawa na watu wasiojulikana. Siwezi kukataa niliwaza ni wewe ndiye uliyepanga mpango ule. Sikushtuka kwa kuamini mpango wetu umekwenda kama ulivyopangwa. Kifo cha baba kiliniweka katika wakati mgumu wa kukana mi si muuaji kwani Ester aliamini kabisa mimi ndiye muuaji.
“Maswali yake nilimjibu kama ulivyonijibu kuwa ametumwa lakini mwisho wa siku nilijua maneno yangu yaliniponza. Kama nimekukosea naomba unisamehe ni wewe mpenzi ndiye uliyenipa uhuru wa kuuliza lolote, kama nitakuwa nimekwenda kinyume naomba muongozo wako mpya ili tufurahie penzi letu lililotutoa jasho la moyo.”
“Mmh!” Twambe alishusha pumzi ndefu kisha alisema.
“Kwanza napenda kukuomba radhi mpenzi wangu, maneno yangu yamekuwa sumu kali moyoni mwako. Baba yako sijui kifo chake kilisababishwa na nini ila taarifa niliipata na kuhudhuria mazishi ya baba mkwe wangu. Kwa maneno yangu niulaumu ulimi wangu na kuwa msaliti.
“Siku zote niliuapia moyo kukupa maneno matamu ambayo yatakuwa sawa na maji yanayoufanya udongo ulainike na mmea kustawi na muda wote kutawaliwa na tabasamu.
“Naomba unisamehe nami ni kiumbe siyo malaika nina upungufu huenda mawazo yangu yalinipeleka ndivyo sivyo. Inawezekana mapenzi yangu mazito ndiyo yaliyosababisha niyaseme haya kwako.
Ila moyo wangu hautachoka kukupenda kwa vile jicho langu baada ya kukuona liligeuka upofu, halikuona tena kingine chochote chini ya jua zaidi yako. “Moyo wangu ulikuchagua wewe hasa baada ya kujitoa muhanga kwangu na kuifahamu thamani ya upendo wako kwangu.
Mapenzi yako ya dhati yalinipa ujasiri wa kuweza kufanya lolote. Naomba unisamehe sana mpenzi wangu nakuapia sitakuumiza tena,” Ambe alipiga magoti mbele ya mpenzi wake.
“Hapana mpenzi wangu, huna kosa bali mimi nikuombe radhi kwa maneno yangu yaliyokuudhi,” Leila alisema huku akifuta machozi.
“Nimekusamehe ila naomba na wewe unisamehe.”
“Nimekusamehe mpenzi wangu.” Walikumbatiana kwa furaha na kufutana machozi kuingia ukurasa mpya baada ya fukuto la moyo na kuufanya moyo uvuje jasho la mateso ya mapenzi. Baada ya miaka miwili Ambe na mkewe walirudi nyumbani wakiwa wameongeza familia mtoto wa kike na kuhamia mkoa wa mbali na kuanza maisha mapya bila kuwa na wasiwasi tena wa moyo. Mabina naye aliendelea kuwa sehemu ya familia baada ya kupata jiko na kujenga familia yake.
Ambe na Leila kila wapotazamana waliachia tabasamu na kukumbatiana, kila mmoja moyo wake ulikuwa baridi baada ya mshikemshike wa mapenzi.
Mwisho