×

Chongo!-13

Ilipoishia wiki iliyopita
Akainuka kutoka katika kiti alichokalia akaingia ndani ya kontena, akaitega vizuri simu yake kabla ya kumpiga picha mbili tatu bila mwenyewe kujijua.
Sasa endelea…

Lakini ghafla akabadili nia ya kwenda, akapata wazo la kuwasiliana na shemeji yake, Jully. Baada ya kujuliana hali kwa kutoonana kwa siku kadhaa, hatimaye Bata akamuuliza kama simu yake ilikuwa na huduma ya ‘WhazAp’, alipokubali, akamtaka aitazame picha anayomtumia kama ataifahamu sura hiyo.

“Khaa, huyu ndiye huyo shemeji yako, yaani mpenzi wa dada yako waliofanya mipango wakuue,” ujumbe mfupi wa maneno ulisomeka katika simu yake, sekunde chache baada ya kutuma picha hiyo kwa Jully. Moyo wake ulilipuka paa, akapeleka macho yake haraka kwa mtu huyo, lakini bahati mbaya alishatoweka, hakujua ni wapi alielekea.

Akainuka na kuangalia mitaa miwili mitatu, lakini hakuweza kuona sura ya mtu huyo. Hasira zikamwingia, kitu ambacho kilimshangaza kidogo Elina, ambaye baada ya kumuuliza kinachomsumbua, Bata akamweleza wazi bila kupindisha maneno.

“Kumbe ndiyo huyu baba jamani, namfahamu huyu tena hadi ofisini kwake, niliendaga kuomba kazi kipindi kile nahangaikia ajira, anafanya pale kwenye lile jengo la pale mtaa wa Samora, linaitwaje sijui, lile refuu,” Elina alimwambia Bata, ambaye alirejesha nyuma kumbukumbu zake na kumuona akiingia kwenye jengo hilo la Exoz Mall.

Bata alifurahi sana kusikia habari hizo, kwake ilikuwa ni afueni kubwa, kwani kwa vyovyote, atampata na hivyo kujua ni wapi alipo dada yake na wanafanya nini. Elina alimhakikishia kuwa atamsaidia kwa kadiri atakavyomhitaji.

Hatua ya kwanza waliyofanya ni kesho yake kwenda kuhakikisha kama bado yupo katika ofisi hiyo. Aliyekwenda ni Elina ambaye aliporudi, alimwambia mwenzake kuwa jamaa huyo alikuwepo na alifanikiwa kuzungumza naye na kufahamu hata anapoishi.
“Ilikuwaje hadi ukajua anapokaa,” Bata alimuuliza akiwa amejawa na furaha isiyo kawaida.

“Nilienda pale kwa malengo, kwa hiyo hata mazungumzo yetu nikawa nimeyapangilia ili nipate nilichohitaji, nikamdanganya nakaa Gongo la Mboto,” Elina alimwambia Bata.

Bata alimwambia alikuwa amemsaidia sana, kazi iliyobaki ni ndogo ambayo alisema ataifanya mwenyewe. Kesho yake majira ya saa tisa alasiri, Bata alikuwa nje ya jengo la Axoz Mall. Akiwa amevalia nadhifu, kama kawaida na miwani yake nyeusi ya jua, aliweka chini pea zake mbili za viatu, kama alivyofanya siku zote.

Ilikuwa kama bahati, kwani nusu saa tu baadaye, Jerry alitoka akiwa ameshikilia mkoba wake mkononi, ishara kwamba alikuwa anatoka. Bata alimsindikiza kwa macho hadi alipokuwa umbali wa mita hamsini kutoka alipo, ndipo akachukua viatu vyake na kuanza kumfuatilia kimyakimya.

Jerry alitembea akikatiza mtaa wa Samora hadi alipofika kwenye mzunguko wa sanamu ya askari, akakata kulia. Kwa sababu ya wingi wa watu, Bata alimsogelea ili asije akampoteza hadi alipomuona akiingia kwenye teksi nje ya jengo la Benki lililopo Posta Mpya.

Teksi hiyo iliingia barabarani, lakini ikaishia kwenye foleni. Bata alienda hadi kwa vijana wa bodaboda waliokuwa wamepaki pikipiki zao mbele kidogo ya mtaa huo, akamfuata kijana mmoja wa umri wake.

“Sikiliza mshkaji wangu. Kuna mtu nataka nimfuatilie, yupo kwenye teksi hapo nyuma, nahisi anaenda Masaki kwa sababu ndiko anakokaa, nitakulipa tutakavyoelewana,” Bata alimwambia kijana huyo.

Dereva wa bodaboda alimtazama vizuri Bata, halafu akamwuliza “Kuna tatizo gani kwani na huyo mtu? Maana isije ikawa wewe mtu wa kazi ukaniponza.”

“Hapana mimi siyo mtu wa kazi, nafanya biashara ya kuuza viatu kama unavyoniona, huyo jamaa ninayemfuata alimpa mimba dada yangu mwanafunzi halafu akatoroka, yeye hanijui, nataka nijue anapokaa halafu nimletee pira,” Bata alimwambia kwa lugha ya vijana wa mjini.

Bodaboda akaamini na kumweleza malipo yake yatatokana na umbali watakaotumia na muda. Muda mfupi baadaye, teksi iliyombeba Jerry ikakatiza walipokuwa wamesimama.
Bahati nyingine nzuri kwao ni kwamba hakukuwa na foleni hadi walipovuka daraja la Salenda. Ndani ya muda wa saa moja, teksi aliyopanda Jerry ilisimama kwenye nyumba moja na yeye kushuka, akaifuata kengele, gari likageuza. Akina Bata walipitiliza na kwenda kusimama mbele zaidi, wakijifanya kuikagua pikipiki yao.

Ufunguaji wa mlango na jinsi Jerry alivyoingia, uliwafanya waamini kabisa pale ndipo alipokuwa anaishi. Nao wakageuza pikipiki na kutokomea!
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo

Leave a Comment